Header Ads Widget

KHANGA YA DHARURA

 


Adeladius Makwega-DODOMA.


Nilidamka mapema sana na kupata usafiri huo, huku basi lilikuwa limejaa sana, sikufahamu kwa nini siku hiyo usafiri ulikuwa mgumu mno, kwa kuwa hakukuwa na siti, kondakta wa basi hili alitupatia ndoo ndogo za ujazo wa lita kumi na kusigeuza chini juu na kukali, kwa sisi abiria nane na abiria mmoja ambaye alikuwa mtoto alipatiwa kipande cha gogo la kuzuia tairi lisirudi nyuma au kwenda mbele akakalia.


Basi hili lilienda kwa mwendo kama wa dakika 15 hivi likasimama. Kusimama huko kulikuwa kwa muda mrefu. Nilishangaa abiria wakishuka. Nilimuuliza abiria mwezangu ambaye alikuwa mkono wangu wa kulia kulikoni? Alinijibu kuwa gari limeharibika, wanalitengeneza.


Ulikuwa msimu wa mvua katika eneo hilo, Mungu bahati gari limeharibia katika eneo lenye makaazi ya watu, abiria wote tulishuka. Baadhi ya abiria walisema kuwa kuna chombo kinaitwa rejeta kinavuja kwa hivyo wanaendelea kuweka mambo vizuri ili tuweze kuendelea na safari.


Niliamua kujibanza kando ya nyumba moja jirani ambapo kulikuwa na watu kadhaa huku kwa kando kukiwa na na wafanyabiashara ndogo ndogo.


Nililikaa hapo, huku mfanyabaishara huyu akiuza mboga za majani, vitunguu na nyanya, niliuthaminisha mtaji ule ulikuwa kama wa shilingi kati ya 15,000-20,000/-. Nilimuuliza hapa biashara ikoje? Alinijibu kuwa yeyea anauza kila jumamosi lakini hapo amekuja kujificha mvua tu lakini hupanga kando ya barabara. Kwa siku anauza kati ya shilingi 5500-7000/-


Nikiwa hapo mara basi liligeuza na kurudi tulipotoka, huku abiria tukiwa tumebaka pale chini, wakidai kuwa wanaenda kuchomelea rejeta hiyo. Nikasema kimoyo moyo kuwa leo hapa tutakaa mno, mama huyu mfanyabishara akaniambia pole baba lakini watarudi tu mtaendelea na safari yenu.


Kwani kaka unakwenda wapi? Niliulizwa swali hilo na dada huyu. Nilimjibu huko niendapo, akasema si mbali kama limeharibika, hata ukirudishiwa nauli yako unafika mapema tu, nilimjibu ni kweli .


Kwani wewe ni kabila gani? Niliulizwa swali hilo na dada huyu . Nilimjibu kuwa mimi ni Mpogoro wa Mahenge, aha kumbe, wewe ni kaka yangu. Akisema kuwa yeye, baba yake ni Mluguru na mama ni Mpogoro. Nikasema ni kweli wewe ni dada yangu kabisa.


“Nilipokutazama tangu mwanzo nilidhani kuwa wewe ni Mhaya.” 


Nikamjibu hapana, huko hata wazazi wangu hawajawahi kufika.


Tukiendelea na mazungumzo hayo I, mara walifika wanafunzi watatu, wasichana wawili waliokuwa wamevalia sketi za rangi ya samawati iliyochujuka (maarufu kama bluu bahari), kati ya wasichana hawa mmoja alikuwa amevalai shati nyeupe na mwingine amevaa hijabu na mvulana alikuwa amevalia suruali rangi kama ya sketi za wasichana na shati jeupe.


Wanafunzi hawa walimsogelea dada huyu na kusema nao jambo katika lugha ambayo sikuweza kuitambua. Dada huyu alitoa kitu kama pesa na kumpa binti mmoja kwa njia ya kufutika. Akawaambia mbona hamumsalimii mjomba? Nilisalimiwa haraka haraka kwa shuruti hiyo.


“Kwanza unaniharibia Khanga zangu, sasa kila siku nitakuwa nanunua Khanga?”


Dada huyu mfanyabiasahra alimpa ufunguo binti aliyekuwa amevalia Hijabu na wao kuondoka zao. Huku mvua kubwa ikinyesha, niliwatazama, je madaftari yao hayawezi kuloa lakini nilidhani mabegi yao yalikuwa imara na thabiti, kuzuia mvua kulowesha madaftari yao.


NIlimuuliza dada huyu kuwa hawa ni wanawe? Alinjibu kuwa yule binti mmoja aliyevalia Hijabu ni binitiye wengine ni watoto wa jirani zake.


Nilimuuliza mbona unamkaripia mno? Na unataka kumyima Khanga, si kwa ajili ya dharura? Alijibu, dharura wapi, bado mdogo, labda mwakani.


“Zile Khanga, wanazitumia kutandika chini, wakiwa darasani maana hawana madawati. Hii sasa ni Kanga yangu ya pili kila siku inafuliwa hadi zinachujuka. Darasa lao  wapo kama 300, karibu wanafunzi 200 na ushehe wanakaa chini.”


Nikamuuliza tena dada ni kweli? Alinijibu.


“Masafu na Mtume!”


Kwa kuwa mimi ninayekuandikia matini hii kwa sehemu kubwa ya maisha yangu nimekulia maisha yanayozungukwa na waislamu wengi, japokuwa ni mkristu, nilibaini kuwa dada huyu jambo alilolisema ni kweli kabisa kwani anamaanisha Msaafu (Korani) na Mtume(Muhamad S.A.W), yaani akiapa kwa Korani na Mtume Muhamad S.A W.


Nilimuuliza jina la shule, alinijibu ni Shule ya Sekondari Kingo, ipo Kata ya Kihonda Manisipaa ya Morogoro. Nilimuuliza swali lingine, Je Mbunge ni nani maana tulikuwa kama tunakaribia Mvomero? Alinijibu ni Abood, Nilimuuliza Mkuu wa Wilaya? Alinijibu kuwa ni Bakari Msulwa.


Mmmmm nilikataa, nikasema Bakari Msulwa aliondolewa mwaka jana. Tena huyu mimi namfahamu ni kama kaka yangu, nimewahi kufanya naye kazi. Nikamwambia nadhani amerudishwa TBC ninamsikia akisoma taarifa za habari.


Basi itakuwa kuna Mkuu wa Wilaya mwingine alisema mama huyu na mimi nikamjibu naaam.


“Piiiiiiii, haya jamani twendeni , haya jamani twendeni.”


Tulihimizwa na kondakta wa basi hilo ili tuingie basini. Nilimuaga dada yangu huyu na mimi kuendelea na safari.


Nikiwa basini nilisema moyoni kuwa Wilaya ya Morogoro Mjini imezungukwa na misitu kadhaa, wanachoweza kufanya ni kufanya tathmini ya uhaba wa madawati ni kiasi gani, Waingie msituni miti ikatwe.


Wawaombe wafanyabiashara wakubwa wawaazime mbao na washirikishe vyombo vya ulinzi kama JKT na JWTZ watengeneze madawati. Kwa kutumia mbao za kuazima.


Ile miti ikishakatwa mbao wawarudishie wale wafanyabiashara waliowaazima.


Mbunge wa Morogoro Mjini anachoweza kufanya ni kutafuta vijana wa kufanya kazi hiyo na vitendea kazi kama misumeno ya moto niliamini kuwa Mheshimwa Abood hilo analiweza.


Mkurugenzi Mtendaji alipie gharama za mafuta na mashine za kukata miti hiyo, posho wanaofanya kazi hiyo, na alipie gharama ya vifaa vyote vya kutengeneza madawati hayo na fedha ya usafiri hadi katika kila shule zenye uhaba huo yakikamilika.


Lakini wilayani Morogoro namfahamu nani? Kama angekuwa bado Bakari Msulwa ni Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mjini ningempigia simu na kumueleza jambo hili kama alivyo muugwana angelifanyia kazi tu.


Lakini mwanakwetu mie namjua nani, pangu pakavu tia mchuzi?


Nilipitiwa na usingizi mzito, mara niliskia mzee unayeshuka Chamwino Njia Panda tumekaribia, sogea sogea baba!


Ahmadi ! nilishituka na kubeba begi langu mgongoni na kushuka zangu kuekea huko  madongo poromoka..


makwadeladius@gmail.com

0717649257

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI