Header Ads Widget

TET YAKABIDHIWA MIONGOZO YA KUFUNDISHIA ELIMU YA STADI ZA MAISHA KWA WALIMU WA SHULE ZA MSINGI NA SEKONDARI

 



Na Mwandishi Wetu.


TAASISI ya Elimu Tanzania (TET), imekabidhiwa miongozo  minne ya kufundishia Elimu ya Stadi za Maisha kwa kuzingatia Afya ya Uzazi, VVU/UKIMWI, Jinsia na Kuhusiana kwa Heshima kwa walimu wa shule za Msingi na Sekondari  nchini.



TET imekabidhiwa miongozo hiyo mapema leo tarehe 21/01/2022 Jijini Dar es Salaam na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) 


Katika hafla hiyo ya makabidhiano ya miongozo, Kamishna wa Elimu Dkt. Lyabwene Mutahabwa amesema, miongozo hiyo inafafanua kwa kina jinsi ya kujenga umahiri na maudhui ya Afya ya Uzazi, VVU na UKIMWI pamoja na Elimu ya Jinsia.


Amesema miongozo hiyo kama itatumiwa vizuri itasaidia kuboresha mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji na kuleta matokeo chanya.


Aidha amesema, Wizara ya Elimu kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania na kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI, itaendelea kusimamia na kuratibu matumizi ya miongozo hiyo.



"Kwa kushirikiana na wadau wa Elimu tutaendelea kudurufu na kusambaza miongozo hii ili kuwezesha fursa ya wadau wengi zaidi kupata nakala na kuzitumia katika kutoa Elimu iliyokusudiwa."Alisema Dkt. Lyabwene.


Aidha, Dkt. Lyabwene ameyashukuru mashirika  ya UNESCO, TACAIDS na Marie Stopes Tanzania kwa ushiriki  na mchango wao katika uandaaji wa miongozo hiyo na kutoa  wito kwa TET kuhakikisha miongozo hiyo inatumiwa na walimu wote wa shule za Msingi na sekondari nchini.


Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu TET, Mkurugenzi wa Mafunzo ya Mitaala Dkt.Fika Mwakabungu amesema kuwa,TET imeshiriki mchakato huo wa kusimamia uandishi wa miongozo hiyo ili kuboresha sekta ya Elimu kwa kujenga vijana wanaojitambua.



Naye Mwakilishi wa UNESCO, Prof Hubert Gijzen amesema kuwa, UNESCO inashirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuboresha Sekta ya Elimu na  kwa kupitia miongozo hiyo wanafunzi watanufaika na maarifa yatakayowasaidia katika masuala ya afya ya uzazi, ukatili wa kijinsia,stadi za maisha na masuala ya VVU.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI