Adeladius Makwega
Dodoma
Januari 9, 2022 nilipokuwa narudi zangu kanisani, nikiwa natembea taratibu pembezoni mwa barabara, kwa kuwa Padri aliposema nendeni na Amani tu alipoondoka altareni mie niliimba mstari mmoja wa wimbo wa mwisho na kutoka nje kuwahi kwangu maana saa mbili kamili ya asubihi nilikuwa na ahadi na mgeni.
Kweli nilirudi kwa kuunga azimio, nikiwa njiani yule bodaboda aliyenibeba, ambaye nilikusimulia katika simulizi ya “Mcheza Kayamba Chamwino Ikulu” alinikuta njiani, sasa nilikuwa nakaribia Ofisi za Kijiji cha Chamwino Ikulu, aliniambia tena twende mheshimiwa! Nilimwambia asante sana, kwani hata kama ningalipanda bodaboda hiyo tena nilibaini kuwa yeye alikuwa akienda njia nyengine kuelekea Ofisi za Maji ya Chamwino na mie nikienda Magharibi ya eneo hilo.
Nilipokuwa nakaribia kwangu, jirani yangu mmoja, nilimkuta yu barazani na mkewe, niliwasalimu wakanjibu kwema. Wakasema karibu jirani tunapeta mahindi, nikawajibu asante. Vipi mnayapeleka mashineni? (Niliwauliza).Wakanijibu ndiyo lakini yamebunguliwa sana, karibu gunia tano zote.
“Jirani sogea karibu uone, yamebunguliwa kabisa hapa tumepeta kati ya gunia zote tano tulizohifadhi sasa zimebaki gunia tatu na tukienda kukoboa yatapungua zaidi.” Alisema Baba wa familia hiyo, mimi niliendelea kutoa pole.
Kwa kuwa majirani zangu wameniambia nitazame, niliingiza mkono na kuyachota mahindi ambayo yalikuwa hayajapetwa,, gafla nikapiga chafya tatu chaa, chaa chaa. Mara nikaona wadudu weusi wakiruka kutoka katika mahindi hayo, kweli mahindi yalibunguliwa sana.
“Debe zilizoharibika ni kama 12, thamani yake ni karibu kati ya shilingi120,000 na140,000 kwa bei ya shillingi 10,000 debe hii ni bei ya Chamwino. Nilipiga hesabu yangu nyingine kwa jirani yangu huyu ambaye ana familia ya watu kati ya 8-9, kwa siku wanakula kati ya Kilogramu tatu-nne za mahindi. Debe 12 kila debe linaweza kuwa na Kilogramu kati ya 16-17. Jumla kuu ni Kilogramu 204. Kilogramu hizo ukizigawanya na Kilogramu nne kwa siku utapata siku 51 ambayo ni miezi inayokaribia miwili na hapo kama hawajakula wali na vyakula vingine.” Wakati napiga hesabu hiyo nilimkumbuka Mwalimu Catherine (Mchaga) aliyenifundisha hesabu za Ankara darasa la nne pale Shule ya Msingi Mkuranga Mkoani Pwani.
Kumbuka nipo na majirani zangu. Jumamosi na Jumapili hii kulikuwa na giza kidogo kutoka na wingu, majirani zangu hawa wakasema labda mvua itanyesha, maana kuna dalili, tangu ilivyonyesha usiku wa kuamkia mwaka mpya hadi Januari 9 hakuna kitu.
“Nilipanda heka zangu kadhaa za mahindi, ile mvua ya mwaka mpya iliponyesha mbegu zilitoka vizuri, lakini kutokana na jua kuwaka mfululizo mbegu zilizochomoza zote zimeharibika, kwa hiyo natarajia kupanda tena mvua ikinyesha. Unajua zile mbegu nilizopanda ni zile mbegu ndefu za asili, kila mwaka huwa tunapanda kati ya mwezi wa 11 na 12. Wakati kama huu mahindi ya siku 90 huwa yanakaribia siku 45 -50 yanakuwa yamefikia urefu mzuri tu.”Alisema baba wa familia hiyo.
Jirani sisi tunatakiwa kupanda mbegu za kisasa na bei ya mfuko ni kati ya shilingi 8000-10,000 nadhani hilo linaweza kusaidia sana. Kuna wakati mvua ililleta shida kama hivi tukapanda mbegu ndefu, mvua ilikatika mahindi yakiwa mafupi mafupi, ulikuwa mwaka wa njaa lakini serikali ilitupatia mahindi ya msaada.
Ndugu huyu alisema kuwa Magufuli mtani wetu yeye alisema kabisa njaa ikija shauri yenu, mtunze chakula. Hivi mpaka sasa jirani, wamesema lolote? Niliulizwa swali hilo (Nilikaa kimya). Nikawatania ahaa nyinyi mpo jirani na mama, hapa hamuwezi kufa njaa.
Wakacheka sana, wakasema wewe acha ukonongo (acha uswahili). Nikaendelea, mkianza kupata tabu ya njaa hawatomwambia mtu, yeye atawaona kwa macho yake kwa kuwa ni jirani yenu.
Wakauliza kwani jirani yetu yupo? Nikasema kesho atakuwepo, nasikia atawaapisha Mawaziri wake wapya. Wakauliza swali lingine, Mbona ving’ora hatusikii? Nikawambia mtavisikia tu. Kuna ving’ora vingine vya kimya kimya, yule mkubwa.
“Magufuli Mungu amrehemu, yule alikuwa mtani wetu, kama kumroga tulimroga na akarogeka, ndiyo maana kila jambo alileta Dodoma. Sasa tunafanya mikakati na mama pia. Maana naye ni jirani yetu pia.” Alisema mama aliyekuwa akipeta mahindi hayo.
Niliwaaga ndugu hawa kwa kuwa nilikuwa na ahadi ya mgeni nyumbani kwangu.
Kweli nilipofika kwangu mgeni wangu ambaye ni Mkwere alikuwa kafika, huku akiniambia kuwa kaka asubuhi hii nimekuja kwako umeshatoka? Kaka una mitala? Nikamjibu nitoe wapi, mie pangu pakavu tia mchuzi, nitawalisha nini? Nilikaa naye chemba ndugu huyu kuzungumza naye kilichomleta.
Tulipokaa katika benchi tu, ndugu huyu alipigiwa simu, akasogea chemba na kuongea na aliyempiga kwa muda kidogo, nilipobaini ni mazungumzo marefu na mie niliinuka kwenda kupika chai angalau ninywe na mgeni huyu.
Chai ilichemka, nikapasha kiporo cha wali na maharagwe, nikakibeba hadi kwenye benchi hilo. Ndugu huyu Mkwere aliponiona nimerudi alikata simu yake ili tuendelee na mazungumzo. Nilimuuliza mbona unaongea kwa simu muda mrefu, una jimbo jipya? Alinijibu hapana, bali aliyempigia simu n babu yake akimuomba pesa.
“Babu anasema kuwa hali ya mvua inatishia njaa, huku akilinganisha na miaka ya nyuma kuliwahi kutokea uhaba wa mvua na kukawa na njaa moja kubwa sana. Watu wengi walifariki kwa kukosa chakula.”Alisema rafiki yangu Mkwere.
Wakati huo walikuwa wakilala katika vitanda vya kamba na juu wanaweka mikeka na wengine wanaweka ngozi za wanyama, ili wakilala kamba zisiwaumize. Hali ilikuwa mbaya ikabidi watu wakaanza kuchukua ngozi walizokuwa wakilalia wakazikatakata na kuzichemsha na kula ili kuepuka kufa na njaa hiyo.
Rafiki yangu huyu aliniambia kuwa Wakwere waliita njaa hiyo kama Njaa ya CHIJAMAKOZO, maana yake watu walikula ngozi walizokuwa wanalalia. Kwa kawaida iwe mkeka, ngozi na hata godoro linalolaliwa huwa linakojolewa. Kitendo cha Wakwere kula ngozi hizo, hashakumu si matusi Wakwere walikula mikojo yao. Mkojo ulilika kutokana na uhaba huo wa chakula wakati huo.
Nilimtania ndugu huyu waambie sasa hao Wakwere wachukue magodoro yao wayachemshe. Akacheka tu, tukaendelea na mazungumzo yetu na baadaye aliondoka zake.
Hoja yangu ya leo ni moja tu, mvua ndiyo hivyo tena, je tumejipangaje? je tutawapa wakulima mbegu bora za kisasa bure ili waweze kupanda mahindi baadae tusitaabike kutoa msaada wa chakula? Au mfuko wa maafa siku hizi umetunishwa? Siyo ule wa kuomba watu kuchangia? Hayo ndiyo maswali yangu kwa leo.
Sifahamu kama kabila langu (Wapogoro) kama wana utani na Wakwere, lakini Wakwere walikula mkojo. Kumbuka CHIJAMAKOZO inatokana na maneno mawili ya Kikwere CHIJA+MAKOZO, maana ya CHIJA ni KULA, MAKOZO ni MKOJO kwahiyo CHIJA MAKOZO ni KULA MKOJO.
Nakutakia siku njema.
makwadeladius@gmail.com
0717649257
0 Comments