MJUMBE wa halmashauri kuu ya chama cha mapinduzi (NEC) Taifa anayewakilisha mkoa wa Iringa Salim Abri Asas amewataka viongozi wa CCM kuwa makini na madalali wa siasa ambao wamekuwa wakiibuka kipindi cha chaguzi kwa lengo la kujipatia fedha kwa viongozi waliopo madarakani ama wagombea.
Huku akiwataka wana CCM kuelekea chaguzi za chama kujiepusha na rushwa kwani iwapo kila mmoja aliwajibika wanachama ndio ambao watatoa kura na kama kiongozi hukuwajibika basi subiri hukumu badala ya kufanya siasa za kuchafuana.
Akifungua kikao cha maalum cha Halmashauri kuu ya CCM wilaya ya Iringa vijijini katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo juzi ,Asas alisema kuwa madalali hao wa siasa wamekuwa wakiibuka kipindi cha chaguzi tu na miaka yote mine hawajapata kuonekana ila sasa wanakuja wakijua kabisa wanaweza kupata chochote kupitia siasa .
“ Ndugu wajumbe kila kiongozi wa CCM alipewa dhamana ya uongozi baada ya kusimama jukwaani na kuahidi kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM hivyo kwa wale waliotimiza wajibu wao vizuri madalali wa siasa hawatakuwa na nafasi ya kuwarubuni ila wale ambao hawakutimiza wajibu wao ndio watasikiliza maneno ya fitina na chuki kutoka kwa madalali hao” alisema Asas
Kuwa ni vizuri kila kiongozi ndani ya CCM mkoa wa Iringa kujitathimini ametekeleza vipi ilani ya CCM na yale ambayo waliahidi kwenye chaguzi yametekelezwa ila kabla ya kuchukua fomu ya kuomba tena nafasi kuwa na majibu ya yale uliyoahidi jukwaani wakati wa kuomba kura vinginevyo utahojiwa toka umechaguliwa ulikuwa wapi na umefanya nini katika utekelezaji wa ilani ya CCM .
Katika hatua nyingine Asas alisema jitihada kubwa zilizofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan katika ujenzi wa vyumba vya madarasa ni kubwa na kuwa wao kama wana CCM na watanzania wote wanajivunia sana jitihada hizo kwani leo shule zinafunguliwa kwa wanafunzi wote waliofaulu kwenda shule hakuna uhaba tena wa vyumba vya madarasa jambo ambalo ni la kupongeza sana serikali .
Alisema miaka mingine kwa kipindi kama hiki wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa pamoja na watendaji wengine wa serikali wakiwemo wakurugenzi huwa wanakimbizana na ujenzi wa vyumba vya madarasa lakini kwa mwaka huu hakuna tena kero hiyo na hata wao kama wadau wa maendeleo hakuna barua yoyote ambayo wamepokea kuombwa michango ya ujenzi wa vyumba vya madarasa ama madawati .
“ Ninani hapa amefuatwa kuombwa mchango wa vyumba vya madarasa naona hakuna hata mmoja sasa mnataka mheshimiwa Rais Samia atupatie nini hivi ndio anaanza tujiandae kwa mambo makubwa na mazuri mbele ya safari pia sisi viongozi twendeni kwa wananchi tukayasemee haya yote”
Asas alisema kuwa utendaji kazi mzuri wa Rais Samia na serikali ya awamu ya sita ndio ambao umepelekea wao kama viongozi wa siasa kutembea kifua mbele.
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Kalenga Jackson Kiswaga alisema kuwa pamoja na ujenzi wa miradi ya elimu ,Rais Samia amesimamia vema ujenzi wa miradi ya barabara ,maji na miradi mingine ambayo imekuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi .
Hata hivyo alishauri wajumbe wa kikao hicho wanapompongeza Rais Samia wasisahau kupongeza wabunge maana wabunge ndio ambao wanaomba miradi hiyo bungeni na Rais ,mbunge na diwani ni wote wanawajibika kuwatumikia wananchi na wote walichaguliwa kutekeleza ilani ya CCM .
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Iringa vijijini Costantino Kihwele aliwataka watendaji wa Halmashauri ya Iringa kuendelea kutekeleza miradi mbali mbali kwa kasi waliyoanza nayo na kuwa wao kama chama wanavutiwa na kasi ya utendaji wa viongozi wa Halmashauri hiyo .
0 Comments