Na Hamida Ramadhani Dodoma
JUMLA ya Shilingi Milioni 57 zimetumika katika kununua Katoni 6000 za Barakoa (Maksi) na Vitakasa Mikono (Sanitaizer) Lita 6000 lengo likiwa ni kwenda kuwasaidia watoa huduma wa afya kwenye kampeni ya utoaji wa huduma za matone ya vitameni A kwa watoto ambapo watoa huduma kutoka mikoa 17 ya Tanzania bara na Zanzibar wanakwenda kunufaika
Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dkt. Ray Masumo ameyasema hayo leo wakati wa makabidhiano ya vifaa hivyo kwa wawakilishi kutoka Ofsi ya Rais Tamisemi na Ofisi ya Rais Muungano na Mazingira huku akielezea vifaa hivyo vitakwenda kuwasaidia watoa huduma ya afya waliopo mstari wa mbele katika kutoa huduma za afya hasa kwa upande wa watoto.
"Hapa tunakwenda kuwagusa watoa huduma ya afya wanauhusika na utoaji wa matone ya vitamini A na Lishe kwa Mtoto kwani malengo yaliyopo ni kuhakikisha ifikapo Mwaka 2025 watoto wote nchini wamefikiwa na huduma ya matone ya Vitamini A kupitia vituo vya afya vilivyopo hapa nchini Tanzania," .
Na kuongeza kuwa" Vifaa hivi vya kujikinga na UVIKO-19 vilivyotolewa na tasisi ya Chakula na lishe Tanzania kupitia shirika la kimataifa ya Nutrition International (NI) vinakwenda kuwakinga watoa huduma ya afya wakati wa kampeni ya utoaji wa huduma ya Matone ya Vitamini A nchini hasa kwa Watoto," amesema .
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Serikali Dkt,Aifello Sichalwe ambaye ndio aliyekuwa mgeni Rasmi kwa niaba ya Waziri wa Afya Dkt Dorothy Gwajima amesema vifaa hivyo vitakwenda kuwasaidia watoa huduma za afya walio mstari wa mbele katika kutoa huduma za afya nchini bila kuwasahau watoa huduma za afya ngazi ya jamii.
Dkt, Sichalwe amesema kutokana na changamoto ya UVIKO-19, Serikali inaendelea kuwapatia vifaa vya kujikinga na maambukizi ya UVIKO-19 watoa huduma waliopo katika vituo vya afya ili kuwawezesha kuendelea kutoa huduma za afya kwa ufanisi ikiwemo Kampeni ya utoaji wa Matone ya Vitamini A inayofahamika kama "Huduma ya Mwezi wa Afya na Lishe ya Mtoto".
Naye Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Kimataifa la Nutrition International Dkt, Daniel Nyagawa amesema wamechukua uamuzi wa kutoa vifaa kwa Serikali ikiwa kuunga mkono juhudi mbalimbali zinazochukuliwa katika kupambana na UVIKO-19 .
0 Comments