Adeladius Makwega
DODOMA
“Safari siyo kifo, huko tulikotoka kote salama.” Huo ni wimbo wa Safari Siyo Kifo uliotungwa na Mbaraka Mwinshehe na kuimbwa pamoja ya Orchestra Super Volkano ya Morogoro.
“Njoo mpenzi njoo, kwangu nyumbani njoo, wala usiwe na wasiwasi… utakalo nitakupa wee. usije lia ukashindwa mwenyewe.” Huo ni wimbo Njoo Mpenzi wa Atomic Jazz Band ya Tanga.
“Pesa pesa kaka maua, pesa umeumbwa na nani ehe, pesa unasumbua akili za watu kuangaika, kukupata wewe shida na ukipatikana ni matatizo…” Huo ni wimbo Pesa Maua wa Afriso Ngoma ya Dar es Salaam chini ya Uongozi wa Lovy Longomba.
Binafsi niliwahi kushuhudia onesho moja la Bendi ya Afriso Ngoma chini uongozi wa Lovy Longomba mwaka 1992 katika Ukumbi wa Kwetu Bar Mbagala Dar es Salaam.
Bendi zote tatu Ochestra Super Volkano, Atomic Jazz Band na Afriso Ngoma hazipo katika ramani ya muziki kwa sasa. Kutokuonekana kwa bendi hizo kuna sababu mbalimbali ikiwamo vifo vya wasanii hao, kukosekana kwa fedha za kuendesha bendi hizo na wasanii wengi kutegemea viingilio kwa hiyo hilo limefanya kushindwa kufanya maonesho mbalimbali na bendi kufa.
Wanamuziki wengi walichonufaika nacho ni pesa za vingilio tu katika kumbi za muziki huku wachache wakipata mirabaha ya kazi hizo mathalani familia ya marehemu Mbaraka Mwinshehe.
Kwa hakika makaburi ya wasanii hao waliofariki yamelaza viwiliwili vyao pamoja na malalamiko ya mapunjo ya haki za kazi zao sanaa walizozifanya wakiwa hai, watoto na wajukuu wa wasanii hao wamekuwa wakilithi malalamiko hayo kutokana na kazi za wazazi wao.
Swali ubaoni, ni je kuanza kugawiwa kwa mirabaha ya kazi za sanaa kunaweza kufuta machozi ya wasani hao?
Kwa hakika kupatikana kwa mirabaha hiyo kwa wasanii kunategemea mambo kadhaa kubwa ni je kazi hiyo ya sanaa imechezwa au kusikilizwa na wapenzi sanaa hiyo? Je mirabaha ni sandakalawe mwenye kupata apate?
Hayo ni baadhi tu maswali ambayo baada ya kutolewa mirabaha hiyo pengine kutakuwa na majibu.
Mwanakwetu pesa maua.
makwadeladius@gmail.com
0717649257
0 Comments