Jumapili ya Januari 23, 2022 niliamka mapema kidogo ili kuwahi misa ya kwanza ya siku hii. Kwa siku hii ukweli wa Mungu hadi nafika kanisani ilikuwa nimechelewa dakika 10.
Japokuwa nilichelewa dakika hizo kilichofanya nichelewe ni kunyesha kwa mvua kubwa usiku mzima kwa hiyo hadi alfajiri hiyo mvua kubwa ilikuwa ikinyesha na matope yalikuwa mengi, mwendo wangu ulikuwa wa uangalifu ili kuepuka kuanguka na kuvunja miguu.
Nilipokaribia ngazi za kanisani nilisikia wanakwaya wakiimba wimbo lakini kanisani kulikuwa giza bila ya kujua kulikoni. Akilini mwangu ilikuja hoja kuwa labda wanakwaya wanafanya mazoezi Padri kachelewa.
Wakati tukio kama hilo huwa ni jambo la nadra sana kulishuhudia, mtu unaweza kuzaliwa hadi kufariki na usishuhudie.
Binafsi nimeshuhudia mara mbili, mara ya kwanza ilikuwa Kigango cha Mkuranga miaka ya 1980s ambapo Padri alikuwa akitoka Parokia ya Mbagala, Parokia ya Kurasini au hata Parokia ya Mtakatifu Joseph na kwenda kusalisha huko. Hakukuwa na simu, mawasiliano yalikuwa ni barua tu. Habari za Padri kwa walei wake ilikuwa wajibu wa Katekista kupita parokiani.
Kila jumapili ya tatu ya mwezi Padri alikuwa anafika huko na kusalisha misa, Padri wetu wakati huo alikuwa Agustino Fernandese huyu alikuwa mchanganyiko wa Baba-Goa na mama-Mmamkonde. Nilifahamu hilo kwa kuwa Padri huyu hata alipofika hapo kusalisha alikuwa akikizungumza Kimakonde vizuri sana na Walei wengi ambao walikuwa Wamakonde, Wamatumbi na makabila mengine ambao walienda huku kufanya kazi kama watumishi (hawa walikuwa wazazi wetu)
Kuna wakati ilifika jumapili ya tatu ya mwezi tunamgonja Padri aje kusalisha muda ukawa unaenda Padri hatokei, ikabidi katekista asalishe ibada bila padri, hadi ibada inakwisha padri hajafika. Katekista wetu alipanda basi hadi Dar es Salaam kuulizia parokiani ndipo alipojulishwa kuwa Padri wetu alipata ajali ya pikipiki hii ilikuwa ni vigango vya Parokia ya Mbagala, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.
Mara ya pili ilikuwa ni Parokia ya Makere Kasulu-Jimbo Katoliki la Kigoma, Padri aliyepaswa kusalisha namkumbuka alikuwa Padri Balikumutwa, parokia hii ilikuwa na mapadri wawili huku wakipeana zamu, mmoja vigangoni mwingine parokiani. Padri wetu alipata dharura na kujisikia vibaya, baadaye Katekista alifanya mawasiliano naye kwa kuwa alikuwa anaishi hapo hapo, baada ya nusu saa alikuja kuendelea na misa. Hii ilikuwa mwaka 2000.
Kumbuka sasa mwanakwetu naingia kanisani Parokiani Chamwino Ikulu-Jimbo Katoliki la Dodoma, nyimbo inaimbwa, Padri simuoni kwa sababu ya giza lakini mishumaa inawaka, kuna taa moja kanisani yenyewe ni ishara uwepo Yesu nayo haiwaki lakini mishumaa mwanakwetu inawaka.
Waamini wapo lakini wachache kama watu 15-20 wanakwaya kama watano hivi, nikakaa katika benchi la katikati ambapo hiyo si kawaida yangu. Kwa kuwa sielewi kinachoendelea basi wimbo ukaisha akaamka dada mmoja kuelekea kwenye marufaa ya kusoma somo akasoma somo la pili kwa kutumia tochi ndogo, nadhani ilikuwa ya simu kwani mwanga wake ulikuwa hafifu.
Nikasema kumbe ibada imeanza na hili ni somo la pili? Kwa hiyo nikakaa mkao wa kusali. Msomaji wa somo alipomaliza, kwaya ikaimba wimbo wa kuelekea kwenye injili. Padri aliamka katika kiti chake kwa kuwa kulikuwa kiza nilishindwa kumuona awali, alipofika katika marufaa akachukua tochi yake akasoma injili huku vijana wahudumu wa misa wakimulika kitabu cha kusomea. Alipomaliza kusoma injili alianza kuhubiri.
Spika hazikuweza kufanya kazi, kwa hiyo mahubiri binafsi niliyasikiliza vizuri kwa sababu nilikuwa katikati ya kanisa, nadhani mtu wa mwisho ilikuwa vigumu kuyasikiliza kwa ufasaha. Misa ilifanyika vizuri huku kwaya wakijitahidi kuimba kwa sauti ya juu ambayo kidogo ilificha ule uhaba wa umeme kanisani.
Alisimama mwenyekiti wa parokia alizungumza kwa kirefu sana juu ya umuhimu wa kutoa zaka na kusisitiza kila mlei kutambua umuhimu huo, aliyasema hayo huku akitolea mfano parokia ya Nkuhungu ambayo alidai kuwa imefanya vizuri katika Jimbo katoliki la Dodoma kwa mwaka 2021. Hata mwenyekiti wetu alipotaka kusoma karatasi fulani ya nukuu ya maelezo yake alishindwa, ilibidi vijana wahudumu wamulike karatasi hiyo kwa tochi na akaweza kusoma.
Nikajiuliza moyoni ni kweli kanisa letu LUKU imekwisha? Sikupata jibu. Lakini kila muda ulivyokuwa unasonga ndivyo mwanga wa kupambazuka ulivyokuwa unasaidia walei kuonana kanisani.
Hoja ya kwanini leo tunasali bila umeme ilikuwa bado ipo kichwani na kwa umri wangu parokia haiwezi kukosa umeme kwa kuwa maandalizi ya misa/ibada ijayo yanaanza mara baada ya misa/ibada jumapili iliyotangulia kwisha. Lakini ikaja hoja kuwa labda umeme umakatika, nikalijibu hilo swali moyoni mwangu mbona nyumbani nimeacha umeme upo?
Padri alihitimisha misa hii kwa Amani ya Bwana.
Hadi ibada inamalizika hakuna umeme. Nje ya kanisa mvua kubwa ikinyesha.
Nilitoka zangu hadi Chamwino Stendi ili kumtumia pesa jamaa yangu mmoja. Nilipofika hapo simu yangu iliishiwa chaji, kwa hiyo nikamuomba kijana wa stendi aniwekee simu yangu kwenye chaji ilikuisoma namba ya ndugu huyu ambaye namtumia pesa
“Kaka umeme kwetu hakuna tangu jana, labda nikusaidie, toa lini yako uweke kwenye simu hii ndogo.” Aliniambia kijana huyu wakala. Nikamjibu sawa.
Hapo na mimi ndipo nikakumbuka kuwa hata kanisani umeme haukuwepo kisa umeme umekatika.
Nilituma pesa hiyo kwa jamaa yangu na mimi kuondoka zangu kurudi kwangu huko madongo poromoka. Nikiwa njiani nilikumbuka miaka ya 1980 huko vigangoni wakati tukisali ibada za usiku wa sikukuu ya Krisimasi huko tukitumia Karabai za kuazima, huku ibada zikiongozwa na Katekista.
makwadeladius@gmail.com
0717649257.
0 Comments