NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
MKUU wa wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro Abbas Kayanda amewataka walimu kuzingatia miiko na taratibu za ualimu, kwani Mwalimu anatakiwa kuandaa maandalio ya somo (scheme of work na lesson plan) kabla ya kufundisha.
Kayanda ametoa kauli hiyo leo katika kikao kazi na Walimu wa sekondari na msingi kilichofanyika katika kata ya Katanga ambapo alisema kuwa wapo walimu wamekuwa wakifundisha kwa mazoea na kuwasisitiza kujikita kwenye miiko ya ualimu.
Alisema kuwa, walimu wanajukumu la kushirikiana na kupendana, kwani baadhi yao hawapendani kabisa na wengine wanatengeneza magurupu Shuleni, kitu ambacho kinajenga chuki ndani yao na kupelekea kuathiri utendaji kazi na kusisitiza kuacha tabia hiyo mara moja.
"Walimu mkiwa na upendo wa dhati wenyewe kwa wenyewe utapelekea kazi yenu kuwa nyepesi zaidi hivyo niwasisitize pendaneni upendo utasaidia kutatua changamoto zinazowakabili" alisema Kayanda.
Aidha Mkuu huyo wa wilaya aliwaagiza kutunza miundo mbinu ya madarasa kwa kushirikian na wanafunzi kwani Manispaa ya Moshi ilipokea kiasi cha fedha, Milioni 440 kutoka kwenye fedha za Uviko 19 na kupelekea kupata madarasa 22 yaweze kutumika kwa vizazi vijavyo.
Katika kikao hicho, Mkuu wa Wilaya aliwapongeza kwa kazi kubwa yanayoifanya ya kuunga mkono juhudi za Serikali pamoja na kuwepo kwa changamoto ndogo ndogo wanazopitia, lakini Serikali ni sikivu chini ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano, Samia Suluhu Hassan inaendelea kushughulikia changamoto hizo.
Aidha aliwapongeza kwa kufaulisha wanafunzi, kwani Manispaa ya Moshi imeshika nafasi ya nne Kitaifa kwa matokeo ya darasa la nne kwa mwaka 2021 na kudai kuwa kwa matokeo hayo ni dhahiri kuwa Walimu wapo kazini na kazi inaendelea.
Katika hatua nyingine aliwapongeza kwa nafasi ya kuwa Mwalimu kwani Ualimu ni heshima kubwa sana, .
Hata hivyo alimshukuru Rais kwa kutoa kiasi cha Milioni 470 kupitia Mradi wa Kuboresha Elimu Sekondary nchini (SEQUIP) kwa ajili ya Ujenzi wa Shule ya Sekondari, katika Kata ya Msaranga, Manispaa ya Moshi.
Pia aliwataka Walimi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya Ugonjwa wa Uviko 19 pamoja na kujiandaa na zoezi la Sensa linalotarajia kuanza mwezi Agosti mwaka huu.
Mwisho.





0 Comments