



************
Bodi ya Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imehimiza shule zinazonufaika na miradi inayofadhiliwa na Mfuko wa Elimu Nchini, unaoratibiwa na TEA kushirikisha wananchi wa maeneo husika katika hatua zote za utekelezaji wa mradi ili kuwa na utekelezaji wenye ufanisi.
Ushauri huo umetolewa kwa pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya TEA, Prof. Maurice Mbago na Mjumbe wa Bodi, Atupele Mwambene wakati wa ziara yao ya kutembelea miradi ya miundombinu ya elimu inayofadhiliwa na Mfuko wa Elimu katika mkoa wa Rukwa na Songwe.
Wasema wananchi wanapopata taarifa za utekelezaji wa miradi kupitia kwa Kamati za Shule, wawaklishi wao pamoja na viongozi wa Serikali za mtaa na vijiji wanakuwa tayari kushiriki kwa kuchangia nguvu kazi hivyo kuleta ufanisi katika utekelezaji na utunzaji wa mradi.
Miradi iliyotembelewa mkoani Rukwa ni ujenzi wa Bweni la wasichana katika Shule ya Sekondari ya Kichema iliyoko Manispaa ya Sumbawanga uliofadhiliwa kwa Shilingi Milioni 75, ujenzi wa nyumba za walimu katika Shule ya Msingi Muzi unaofadhiliwa kwa Shilingi Milioni 100 na nyumba za walimu zinazotumiwa na familia sita (Six in one) katika Shule ya Sekondari Kasanga uliogharimu Shilingi Milioni 145. Miradi hiyo miwili iko katika Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo.
Katika mkoa wa Songwe wametembelea mradi wa ujenzi wa madarasa matatu katika Shule ya Msingi Haloli iliyoko Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, uliogharimu Shilingi Milioni 60.
Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ni Taasisi ya Umma inayofanya kazi chini ya usimamizi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. TEA inaratibu Mfuko wa Elimu wa Taifa na Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF).
0 Comments