NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
MBUNGE wa Jimbo la Moshi vijijini mkoani Kilimanjaro, Prof. Patrick Ndakidemi amefanya ziara ya kikazi katika kata ya Old moshi magharibi na kujionea miradi ya maendeleo iliyotekelewa na inayoendelea kutekelezwa.
Mbunge huyo aliyeambatana na viongozi wa CCM kata na vijiji pamoja na viongozi wa serikali kuanzia kata, wenyeviti wa vijiji watendaji wa vijiji pamoja na wenyeviti wa vitongoji.
Prof. Ndakidemi alikagua ujenzi wa kalvati lililojengwa katika kijiji cha Tela kuzuia mafuriko pamoja na ujenzi wa choo cha zahanati ya Tela na ujenziwa jengo la maabara katika shule ya sekondari ya Maringeni.
Katika zahanati ya Tela, Mbunge alikagua ujenzi wa choo cha zahanati ambapo hadi sasa haujakamilika kutokana na kitendo cha mkandarasi kukatisha kazi ya ujenzi.
Hali hii imesababisha sintofahamu kwa kuwa ujenzi umechukua muda mrefu pamoja na ukweli kwamba fedha za ujenzi (million saba) zipo Halmashauri.
Akiwa katika Shule ya Sekondari ya Maringeni Mhe Mbunge alikagua Ujenzi wa jengo la maabara ambapo Halmashauri imechangia kiasi cha shilingi milioni thalathini limefikia katika hatua ya lenta na sasa ujenzi umesimama kutokana na uhaba wa fedha.
Aidha Mbunge huyo huyo alifanya ukaguzi wa udabuaji wa korongo la kwa Saning'o lililopo kijiji cha Mandala mnono kitongoji cha Saning'o ambalo utekelezaji wake ulitumia fedha za mfuko wa jimbo kwa kiasi cha milioni 3.
Pia alipata wasaa wa kuzuru korongo hilo na kuangalia namna kazi ilivyofanyika.
Mbunge huyo alipata pia nafasi ya kuhutubia mkutano wa hadhara katika Kijiji Cha Sanin'go ambapo alisoma ripoti ya miradi iliyogharimu zaidi ya Shilingi milioni 900 iliyotekelezwa katika miradi mbali mbali ya maendeleo katika kata hiyo pamoja na kuchukua kero mbalimbali za wananchi.
Prof. Ndakidemi aliwashukuru wadau wote wanaoshirikiana na serikali katika kusukuma gurudumu la maendeleo.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Old moshi magharibi Menyasumba Macha alimshukuru Mbunge kwa kuwatembelea na kukagua miradi ya maendeleo katika kata yake pamoja na kufanya mkutano wa hadhara.
Mwisho.
0 Comments