Header Ads Widget

TAASISI BINAFSI NA WAKANDARASI WATAKIWA KUFANYA KAZI KWA WELEDI

Na Fatma Ally MDTV Dar es Salaam

Wakandarasi na Taasisi nyingine za sekta binafsi zimetakiwa kuzingatia weledi, maadili na uaminifu katika majukumu yao ili wanapotekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo iweze kuleta tija kwenye maisha ya Watanzania.

Kauli hiyo, imetolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati alipokua akifungua mkutano wa 21 wa wanachama wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) na kongamano la Biashara na Uwekezaji katika chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM) .

Amesema kuwa, Serikali inatambua mchango wa sekta binafsi katika kuleta maendeleo na kukuza uchumi nchini, ambapo Sekta hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa ukuaji katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, viwanda sanaa, mawasiliano pamoja na utalii.

Aidha, ameitaka Sekta binafsi kuendelea kushiriki katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya kimkakati, pamoja na kuhakikisha wanawekeza katika maeneo ya vijijini kwa kuanzisha viwanda katika maeneo hayo ili kupunguza idadi ya watu wanaosafiri kuja maeneo ya mjini kutafuta ajira.

Ameongeza kuwa, Serikali itaendelea kuishirikisha sekta binafsi katika ziara za Serikali nje ya nchi kama alivyofanya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwenye ziara za nchi za Kenya, Burundi, Marekani, Malawi, Msumbiji na Uganda.

Hata hivyo, ameitoa wito kwa sekta binafsi kupanua wigo wa uwekezaji katika kuongeza thamani za bidhaa ikiwemo bidhaa za madini, kilimo, misitu, uvuvi na mifugo, Sambamba na kuwekeza katika uzalishaji wa mashine na teknolojia nafuu za urutubushaji vyakula pamoja na uzalishaji wa virutubishi nchini.

Akizungumza kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji Geoffrey Mwambe amesema licha ya uwekezaji kuendelea kukua nchini Watanzania wameendelea kuwa wadau muhimu kwani hadi sasa usajili wa zaidi ya asilimia 43% uliosajiliwa ni wa wawekezaji wazawa.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya TPSF Angelina Ngalula, kwa niaba ya Sekta Binafsi alitoa pongezi kwa Serikali ya awamu ya sita kwa jinsi ilivyoboresha ushirikiano na Sekta binafsi sambamba na kuboresha mazingira na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje na kuimarisha mahusiano na nchi za nje.

"Tayari jitihada za kuboresha mahusiano na nchi za nje zimeanza kuzaa matunda na katika kipindi kifupi kumekuwa na mafanikio makubwa kwani uwekezaji kutoka nchi ambazo Rais amezitembelea umeweza kuongezeka"amesema  Ngalula.

Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Ummy Mwalimu, amesema Wizara yake kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda tayari imepeleka mapendekezo ya kuanzisha Idara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji katika kila halmashauri ili kuongeza ufanisi na kutengeneza mazingira bora ya kiutendaji na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wawekezaji kuanzia ngazi ya chini.

Waziri wa Viwanda na Biashara Profesa Kitila Mkumbo amesema licha ya  Serikali kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, itaendelea kuhakikisha kunakuwa na taasisi imara katika kuwasaidia wawekezaji pamoja na kuboresha Sera za Uwekezaji na Biashara nchini ili kupata Sera nzuri  ambazo zinarahisisha biashara na uwekezaji.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI