Na WILLIUM PAUL, ROMBO.
WANAWAWAKE wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro wameonyesha kutoridhishwa na utoaji wa mikopo ya halmashauri kwa vikundi vya wajasiriamali huku wakitupia lawama kwa maafisa maendeleo ya jamii kati kwa kuvitoza fedha vikundi ili visajiliwe kieletroni.
Hayo yamejiri jana wakati Mbunge wa viti maalum (ccm) mkoa wa Kilimanjaro Zuena Bushiri alipokutana na wanachama wa vikundi vya ujasiriamali vya kata ya Kelamfua mokala ambapo alishangazwa na jinsi wakinamama hao wanavyokumbana na changamoto katika upataji wa mikopo.
Anna Robert alisema kuwa, kikundi chao kilianza kuomba mkopo wa halmashauri tangu mwaka 2017 lakini mpaka sasa hawajapata mkopo na kila wanapofika katika ofisi za Afisa maendeleo ya Jamii halmashauri ya Rombo wamekuwa wakipewa matumaini kuwa watapata.
"Tulifika kwa mara ya kwanza katika ofisi za Afisa maendeleo ya jamii pale halmashauri mwaka 2017 ambapo walituambia tufungue kwanza akaunti ndipo tupate mkopo toka tumefungua mpaka leo hatujawahi kupata hata mia kila siku tumekuwa tukitumia gharama kwenda ofisini kwao bila faida yoyote" alisema Anne.
Wakinamama hao walidai kuwa, wanapoenda kwa maafisa maendeleo ya jamii kata kusajili vikundi vyao kwa njia ya kieletroni wamekuwa wakitozwa fedha 27000 kwa kila kikundi hali ambayo iliwashangaza waliposikia usajili wa vikundi ni bure.
Mbunge huyo alishangazwa na kitendo hicho cha wakinamama kunyanyashwa na kubaguliwa katika upewaji wa mikopo na kuomba ofisi ya chama cha mapinduzi wilaya ya Rombo kukaa chini na mkuu wa wilaya hiyo pamoja na Mkurugenzi ili kutafutia ufumbuzi wa changamoto hiyo.
Mbunge huyo alisema kuwa, lengo la serikali kutenga fedha hizo ni kuwainua kiuchumi wanawake, vijana na walemavu hivyo kitendo cha kuwabagua katika utoaji wa mikopo hiyo ni kinyume na lengo la serikali.
"Keki ya Rais Samia Suluhu Hasani ni ndogo lakini lengo lake ni kuhakikisha kila mwananchi anaionja hivyo niwatake watumishi wa halmashauri mkiwamo Maafisa maendeleo ya jamii acheni ubinafsi tekelezeni majukumu yenu kwa mujibu wa sheria" alisema Mbunge Zuena.
Mbunge Zuena aliwataka watumishi wa Serikali kutambua kuwa wakiharibu katika majukumu yao anayekuja kuadhibiwa na wananchi ni chama cha mapinduzi.
Kwa upande wake Katibu wa ccm wilaya ya Rombo, Mary Sulle alisema kuwa, kitendo wanachokifanya Maafisa maendeleo ya jamii kuvinyanyasa vikundi vya wajasiriamali ni kutaka kuwaonyesha wananchi kuwa chama kimeshindwa kuongozi na kudai kuwa hawatakubaliana na jambo hilo hivyo watahakikisha wale wote wasiotimiza wajibu wao wanachukuliwa hatua.
"Hawa wakinamama wanalipa kodi ambapo nyinyi watumishi wa serikali ndipo mnapopata mishahara yenu na mnapaswa kutambua kuwa hizi nafasi ambazo mmezipata ni kwa sababu ya hawa wananchi acheni ubinafsi watumikieni wananchi kwa moyo" alisema Mary.
Mwisho..
0 Comments