Header Ads Widget

M/KITI WA HALMASHAURI YA WILAYA MULEBA AWAAGIZA WATENDAJI NA MAAFISA ELIMU KATA KUTUNZA MALI ZA SHULE.

 



Na, Titus Mwombeki,Kagera.


Zoezi la kukabidhi madawati kwa shule tatu za msingi ambazo ni shule ya msingi Bugara, Shule ya msingi Kagondo na shule ya msingi Kalimalimo limefanyika katika shule ya Msingi Ngenge iliyopo kata ya Ngenge wilaya ya Muleba ambapo Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Magongo Justus amewataka Watendaji na Maafisa elimu kuhakikisha wanatunza vizuri mali zote za Shule.


Akizungumza katika zoezi la ugawaji wa madawati hayo Mhe. Magongo pia amewataka walimu nao kuhakikisha wanashirikiana na watendaji wa Vijiji, Watendaji wa kata na Maafisa Elimu Kata madawati na vifaa vingine vinavyopelekwa katika shule zao viweze kusimamiwa na kutunzwa kwa ubora ili viwe endelevu katika kutoa huduma kwa wanafunz.


"Tunapopata madawati haya ni jukumu letu kuendelea kuyatunza sitegemei kama nitakabidhi madawati halafu baada ya wiki moja yaharibike hapo tutakuwa tunaharibu rasilimali fedha ambayo ni michango na kodi za wananchi wa Muleba. Ni vizuri tukatunza madawati haya kwa ajili ya matumizi ya wanafunzi wanaoendelea kusoma", amesema Mhe. Magongo.



Kwa upande wake Afisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya wilaya Muleba Mwl. Seveline Msyangi amesisitiza walimu na wanafunzi kutunza madawati na vifaa vingine kama vitabu kwa manufaa ya vizazi hadi vizazi. Ameeleza kuwa kwa dawati moja wanakaa wanafunzi watatu ili waweze kuandika vizuri. Na pia madawati hayo yanaweza kutumika kutunza vifaa vya wanafunzi.


Kwa upande wao walimu wakuu wa shule za msingi tatu zilizopata mgao wa madawati kwa nyakati tofauti wameishukuru Halmashauri ya wilaya Muleba kwa kutekeleza zoezi la mgao wa madawati hayo jambo ambalo litaenda kupunguza uhaba wa madawati katika shule zao na kutoa ombi kwa wadau wa elimu kuendelea kusaidia kwani uhitaji bado ni mkubwa. Sambamba na hilo wameiomba jamii kuona ni kwa namna gani wanaweza kusaidia kuondokana na upungufu wa madawati katika shule zao.



Shule zilizopata mgao wa madawati ni shule ya msingi Bugara  madawati 45, shule ya msingi Kagondo madawati 60 na shule ya msingi Kalimalimo madawati 20.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS