Migogoro ya ardhi ni hali ya kutofautiana kimaslai baina ya pande mbili au zaidi juu ya umiliki, matumizi, upatikanaji na usimamizi wa ardhi na rasilimali zilizopo katika ardhi........NA ADELADIUS MAKWEGA_MBAGALA
Baadhi ya migogoro inayofahamika ni kama ilivyoainishwa ni, ile ya wakulima na wafugaji kugombania rasilimali adimu kama vile maji na malisho, kijiji dhidi ya kijiji wakigombea mipaka, Halmashauri ya kijiji kupitisha maamuzi ya ugawaji ama utoaaji wa ardhi ya kijiji bila ya kushirikisha wananchi.
Taasisi za kiserikali, kidini na kibinafsi dhidi ya wanavijiji hasa pale taasisi hizi zinapotanua maeneo yao hadi kwenye maeneo ya kijiji, Mamlaka za hifadhi dhidi ya wanavijiji kutokana na kupanuka kwa hifadhi hadi kwenye maeneo ya wanavijiji bila mawasiliano wala kufuata taratibu, Vile vile baadhi ya wanavijiji kuvamia maeneo ya hifadhi kwa ajili ya kilimo na ufugaji, Wachimbaji wadogo wa madini dhidi ya wachimbaji wakubwa.
Hii ni kutokana na baadhi ya wachimbaji wakubwa kuingia maeneo ya wachimbaji wadogo bila kufuata taratibu zinazotakiwa zikiwemo kulipa fidia inayostahili vilevile wachimbaji wadogo kuvamia wachimbaji wakubwa, Migogoro baina ya mtu na mtu na Wananchi na wawekezaji wakubwa kwenye ardhi.
Migogoro ya ardhi kwa Tanzania inasababishwa na mambo mengi mathalani Matini hii imejaribu kuainisha baadhi ya vyanzo na viashiria vya migogoro ya ardhi ili kumsaidia msomaji kutambua ni kwa namna gani migogoro ya ardhi hutokea na zipi ni dalili za migogoro ya ardhi kuibuka. Hii itasaidia sana kwa mwananchi kuona chanzo au dalili za kuibuka kwa mgogoro wa ardhi, na kuweza kuchukua hatua stahiki kwa wakati, kwa kuziarifu mamlaka husika kama suala lenyewe limo ndani ya uwezo wa chombo hicho.
USA Aid kwa msaada wa watu wa Marekania katika baadahi ya nyaraka zo walibainisha baadhi tu ya vyanzo na viashiria vinavyoweza kusababisha migogoro ya ardhi kuibuka katika eneo.
“ Sheria za ardhi kutofahamika vizuri miongoni mwa wananchi na viongozi na hivyo kutofahamu haki na wajibu wao juu ya ardhi , Ukiukwaji wa Sheria zinazo simamia ardhi kwa baadhi ya watendaji kwa mfano, kugawa eneo moja kwa watumiaji zaidi ya mmoja, Kuendelea kupanuka kwa Miji na kumeza maeneo ya vijiji, Ongezeko kubwa la wawekezaji katika ardhi kunafanya wananchi wengi kuondolewa kwenye maeneo yao yenye rutuba pasipo kufuata utaratibu wa kuwalipa fidia stahiki, ya haki, na ya wakati, Upanuzi wa barabara na miundo mbinu mingine, husababisha wananchi wengi kuvunjiwa maeneo yao ya makazi, Mitazamo hasi juu ya kundi la watu fulani na utaratibu wao wa kuzalisha mali, mfano wafugaji na wakulima, Uhaba wa rasilimali ardhi katika eneo fulani huweza kuibua migogoro ya ardhi, Mfano kupungua kwa nyanda za malisho kwa upande wa wafugaji, huwalazimisha kuingiza mifugo yao kwenye maeneo yaliyo tengwa kwa ajili ya kilimo, Wananchi kutoshirikishwa na kukosekana kwa uwazi juu ya usimamizi na maamuzi katika masuala yanayohusu ardhi na Kukosekana kwa mpango shirikishi wa matumizi ya ardhi katika eneo husika.”
Katika hoja hizo wilaya ya Handeni Mkoani Tanga kwa sasa kumeibuka kuongezeka kwa wakezaji wa kilimo cha Mkonge, hivyo jambo hilo kuibua uuzwaji wa mara nyingi wa mashamba na kwa kuwa hawa wanaolima mkonge ni matajiri wanao uwezo wa kufanya lolote katika sheria za Tanzania. Kwani wanaweza kupeleka shauri popote na wana uwezo wa kuwalipa wanasheria kinyume na wananchi wa kawaida ambao uwezo wao ni mdogo na kugharmia mashauri mahakamani ni kazi ya nenda rudi nenda rudi katika mabaraza hayo mwisho wake haki zao zinapotea bure.
Siku zote zao la mgogoro wa aina yoyote ni madhara ya aina fulani. Leo hii najaribu kuainisha baadhi tu ya madhara yanayotokana na migogoro ya ardhi, ili msomaji apate kutambua matatizo yanayotokea pindi migogoro ya ardhi inaposhindwa kutatuliwa. Madhara hayo yanaweza kuwa ya kijamii, kiuchumi, na pengine hata ya kisiasa. Kilosa, Kiteto na Loliondo ni sehemu tu ya mifano kwa Tanzania, inayoonesha ni jinsi gani migogoro ya ardhi ilivyo waathiri wazalishaji wadogowadogo (wakulima na wafugaji).
Bi Halima Dedegu aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kilosa kuna wakati na mimi nilikuwa Mtumishi wa MVIWATA Mkoani Morogoro, tuliwahi kufika huko na kushuhudia madhara makubwa ya migogoro hiyo ambayo kuna wakati mwingine inagharimu uhai wa binadamu.
Yafuatayo ni baadhi tu ya madhara yanayoweza kusababishwa na migogoro ya ardhi, Uhasama, chuki na mgawanyiko miongoni mwa jamii na kukuza tofauti baina ya watu au kikundi cha watu walio ndani ya migogoro ya ardhi, Kusababisha majeraha na mara nyingine kupoteza uhai wa binadamu na wanyama pia kama nilivyotolea mfano wa KIlosa ya Halima Dedengu wakati huo, Kupungua kwa uzalishaji mali na mazao ya chakula kutokana na kupoteza muda mwingi kwenye kutatua migogoro ya ardhi, Kupotea kwa amani katika jamii husika, Kudumaza maendeleo kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla, kwa kuwa rasilimali kubwa inatumika katika kutatua migogoro ya ardhi na kuacha sekta zingine zikidumaa, Kukosekana kwa huduma za kijamii kama vile kufungwa kwa zahanati, shule na barabara .
Baadhi ya mbinu au njia ambazo mwananchi hana budi kuzielewa vyema, ili aweze kuziepuka na kuzuia kuibuka kwa migogoro ya ardhi. Kama tujuavyo usemi huu wa Kiswahili usemao “Kinga ni bora kuliko Tiba”, msemo huu unatukumbusha wanajamii hasa sisi wazalishaji wadogo tusisubiri mpaka migogoro ya ardhi iibuke au ifikie hatua ya kuleta madhara ndiyo tuanze kuitatua, bali tuchukue hatua mapema zaidi kabla madhara hayajatokea. Hizi ni baadhi ya njia na mbinu mbalimbali zinazoweza kusaidia kuzuia na kuepuka migogoro ya ardhi Tanzania.
Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi Tanzania inasaidia Kujenga uwezo wa kisheria kwa vyombo/mamlaka zinazohusika na usimamizi wa ardhi ili viweze kusimamia kwa misingi ya haki,. Kuwezesha uundwaji na utekelezaji wa mipango shirikishi ya matumizi ya ardhi vijijini, Watendaji wenye mamlaka ya juu ardhi kufuata sheria na taratibu katika kusimamia ardhi ili kuepusha migogoro ya ardhi isiyo ya lazima, Kuepuka dalili zozote zinazoashiria mgogoro ya ardhi, Sheria zote zinazosimamia ardhi zifundishwe kwa wananchi wote ili waweze kujua haki zao na wajibu wa msingi juu ya ardhi, Kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi katika maeneo mbalimbali ya nchi ili kila eneo litambuliwe kwa kupimwa, Wananchi washirikishwe katika kutoa maamuzi yanayohusiana na mustakabali wa ardhi yao na Kuhimiza ushiriki, ushirikishwaji na uwazi katika usimamizi na maamuzi ya ardhi vijijini.
Mfumo wa utatuzi wa migogoro una manufaa kidogo sana kwa mzalishaji mdogo ukilinganisha na ule usiyo rasmi. Kwa kuwa mfumo huu lazima ufuate sheria za utatuzi wa migogoro ya ardhi ambazo wazalishaji wadogo hawana uelewa nazo sana, pia mfumo huu upo kitaalamu zaidi kiasi cha kumuwia vigumu mzalishaji mdogo kuzifikia haki zake, pia kuna hitajika gharama za uendeshaji mashauri ukiondoa baraza la ardhi la kijiji tu ambalo halina gharama yoyote. Na pia mfumo huu unatumia lugha ambazo wakati mwingine ni vigumu kueleweka kwa mzalishaji mdogo, mfano nyaraka zote kuandikwa kwa lugha ya kisheria.
Ikumbukwe kuwa, katika ngazi ya kijiji kuna usuluhishi wa migogoro ya ardhi unaopitia njia zisizo rasmi mfano wazee wa kimila, Viongozi wa Dini, Wazee Maarufu, au mabaraza ya wazee wa kijiji pamoja na kuwa hawatambuliwi na sheria kuwa ni sehemu ya mamlaka ya utatuzi wa migogoro ya ardhi, bado jamii inaweza kuendelea kutumia mifumo hiyo kwakuwa, ndiyo ipo karibu na jamii zaidi na haina gharama na huchukua muda mchache sana kuifikia maridhiano.
Binafsi ninaona kuwa wazalishaji wadogo wanafikia maridhiano juu ya migogoro ya ardhi kupitia mifumo isiyo ya gharama na isiyotumia muda mwingi kusuluhisha migogoro hiyo ili wananchi waweze kupata muda wa kujihusisha na uzalishaji zaidi kuliko kupoteza muda mwingi katika kutatua migogoro ya ardhi. Naweka kalamu yangu chini kwa leo nasema kuwa viwavyo na iwe mahakama za mwanzo zisiyaonee gere mabaraza ya usuluhishi ya ardhi na nyumba kutatua migogoro hiyo kufanya hivyo kuichochoa migogoro ya ardhi na mahakimu wanaofanya hivyo kwa kigezo cha wananchi kukata rufaa mahakama za juu waondolewe katika mahakama zetu za mwanzo.
Kwani sasa mahakama inapotumia kigezo cha kutokukosea ni kuwanyima haki baadhi ya wananchi wanyonge.
makwadeladaius@gmail.com
0717649257.
0 Comments