HUDUMA ya utengenezaji wa viungo bandia imeanza kutolewa mkoani Iringa baada ya kampuni ya ASAS Ltd kutoa msaada uliowezesha ujenzi wa jengo la karakana ya kutengeneza viungo hivyo katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa, mjini Iringa.
Jengo hilo lililozinduliwa juzi na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo Salim Asas, umeelezwa kugharimu takribani Sh Milioni 400 zinazojuimuisha mashine na baadhi ya vifaa mbalimbali vya kutengenezea viungo hivyo bandia.
Kuanza kutolewa kwa huduma hiyo kumeelezwa na Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, Dk Iddy Omary kwamba; “kutaleta nafuu kubwa ya gharama kwa wahitaji wa huduma hiyo.”
Kabla ya huduma hiyo kuanza kutolewa katika hospitali hiyo, Dk Omary alisema waliokuwa wanahitaji kufanyiwa upasuaji kwa ajili ya kuwekewa viungo bandia walilazimika kutumia gharama za ziada kusafiri kwenda katika hospitali kubwa zaidi ikiwemo Muhimbili, Mbeya, KCMC na Benjamini Mkapa.
“Hatua hii imepunguza gharama kwa wateja kutoka kati ya Sh Milioni 2.5 hadi zaidi ya Sh Milioni tatu hadi kati ya Sh 600,000 na sh Milioni moja. Tumshukuru sana Asas kwa msaada huu mkubwa,” alisema.
Alisema kampuni ya ASAS ilikubali kujenga jengo hilo baada ya kupokea maombi kutoka hospitali ya Vicensa ya Italia ambayo imeingia ushirikiano na hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa tangu mwaka 2004 kwa ajili ya kuboresha huduma zake.
Mratibu wa hospitali ya Visenza katika hospitali hiyo ya rufaa ya Mkoa wa Iringa, Agusto Zambaldo alisema sekta binafsi na sekta ya umma zinapaswa kuendelea kushirikiana ili kuboresha huduma mbalimbali za afya mkoani Iringa na nchini kwa ujumla.
Akiishikuru kampuni ya Asas kwa ushirikiano huo, Zambaldo alisema mzunguko wa huduma nzima ya ushauri na utengenezaji wa viungo bandia utakuwa umekamilika na kuvutia zaidi pale kutakapokuwa na jengo bora la mazoezi ya viungo.
“Jengo lililopo sasa ni dogo na limechakaa. Nitumie fursa hii kuiomba tena kampuni ya Asas itujengee jengo la mazoezi ili kukamilisha mzunguko wa utoaji wa huduma hii hospitalini hapa,” alisema.
Akizindua jengo hilo, Asas ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa alisema kwa kupitia karakana hiyo, ni furaha kuona viungo mbalimbali bandia ikiwemo miguu na viungo vingine vya mwili kama mikono na vidole, inatolewa.
“Kwa kupitia karakana hii na uwepo wa wataalamu wabobezi katika utoaji huduma ya viungo bandia, tuwakaribishe wananchi wa Iringa na mikoa ya jirani kutembelea na kupata ushauri na huduma hii katika hospitali yetu ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa,” alisema.
Asas alisema kampuni yao iliamua kujenga jengo hilo kwa kuzingatia hali ya ajali hasa zinazosababishwa na bodaboda katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Iringa.
“Changamoto ilikuwa kubwa, watu wetu walikuwa wanalazimika kwenda hospitali kubwa nje ya mkoa wa Iringa na kuingia gharama kubwa. Kwa kuzingatia hilo na mahitaji ya viungo bandia tumejenga karakana hii,” alisema.
Pamoja na ujenzi wa karakana hiyo, Asas amekubali ombi la kujenga jengo la kisasa la mazoezi ya viungo akisema ujenzi wake utaanza mara tu atakapopatiwa ramani yake na uongozi wa hospitali hiyo.
“Tuataendelea kushirikiana na hospitali ya mkoa na serikali kuharakisha baadhi ya miradi yake ya maendeleo. Nchi hii ni yetu sote kwahiyo kila mmoja kwa nafasi yake anawajibu wa kuchangia maendeleo yake,” alisema.
0 Comments