Wilaya ya Mufindi imeadhimisha miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania kwa kuwafariji Wagonjwa katika Hospitali ya Mji wa Mafinga iliyopo Mjini Mafinga mapema leo Disemba- 09.
Tukio hilo la kibinadamu limeongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Saad Mtambule, likiwajumuisha pia viongozi waandamizi wa Serikali, viongozi wa dini, Taasisi ya Msalaba Mwekundu, watumishi wa umma sanjari na wananchi waliojitokeza.
Wakiwa Hospitalini hapo, wametembelea Wodi ya Wazazi, Wodi ya Watoto, Wodi ya Wanawake pamoja na ile ya wanaume ambapo katika wodi hizo zote wametoa mkono wa pole kwa kukabidhi vitu mablimbali ambavyo ni Sabuni na Fedha kwa baadhi ya Wagonjwa.
Aidha, katika kuthamini zawadi ya uhai na kuwajali wengine, Mkuu wa Wilaya Mhe. Mtambule, amewangoza Waadhimishaji katika zoezi la kuchangia benki ya damu ya Hospitali hiyo ili iweze kusaidia kuokoa maisha wa wagonjwa pindi inapohitajika.
09 Disemba 1961 ya kila mwaka ni kumbukizi ya kihistoria kwa Taifa la Tanzania kwani ndiyo tarehe ambayo Baba wa Taifa Mwal. Nyerere, aliwangoza Watanzania kujitwalia Uhuru kutoka kwa Mkoloni Mwingereza ikiwa ni kilele cha harakati za muda mrefu za kudai Taifa huru.
MIAKA 60 YA UHURU; TANZANIA IMARA , KAZI IENDELEE.
Taarifa Na Ofisi ya Habari na Mawasiliano kwa Umma ya Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi.
0 Comments