Nilipewa barua yangu na kuelekea huko Isimani Tarafani, kwa kuwa nilikuwa natokea Dar es Salaam nilifunga mizigo yangu likiwamo sanduku langu la nguo na nilitoa kopi vyeti vyangu na kuchukua kompyuta yangu ya desktop na kuifunga katika boksi maalumu na kuanza safari ya kwenda Iringa.
Kwanza nilipanda basi la Scandinavia kituo cha Kamata- Gerezani na kuelekea ubungo kwenda huku Lilinga kwa Chifu-Mkwawa. Nilifika Iringa Mjini jioni sana huku nikipigwa na baridi na sikuwa na sweta la kujifunika, hapa nilikumbuka maneno ya Shaban Robert kuwa mzizimo wa baridi mara zote humpata kondoo mwenye manyoya haba. Sikuwa mgeni Iringa Mjini kwani nilishawahi kufika huko mwaka 1998 nikielekea Kiwele kwani huku kulikuwa jamaa zangu tuliowahi kuoleana nao na sasa ilikuwa kama miaka sita baada ya mwaka huo yaani 2004.
Niliposhuka niliwauliza vijana wa stendi waliniambia kuwa kama naenda Isimani Tarafani natakiwa kulala alafu kesho nianze safari ya kwenda huko Iringa Vijijini.
Kulala hapo niliona gharama lakini kijana mmoja mbeba mizigo alinishauri kwenda Kihesa hapo kuna lori za mizigo zinazoenda Mtera, Migori na Dodoma kwa hiyo nitapata usafiri tu. Kweli nilipanda Hiace hadi Kihesa na kushusha mizigo yangu sanduku langu na boksi la Kompyuta, sasa ilikuwa saa moja na robo usiku.
Kwa bahati nzuri nikiwa Kihesa ilitokea Lori moja kubwa likanichukua na mizigo yangu kuelekea isimani Tarafani. Nilifika hapo kama saa nne usiku. Kwa bahati nzuri niliposhuka ilikuwa ni njia panda ya kuekea parokiani. Palikuwa na nyumba mbili nilienda nyumba hizi jirani nikajitambulisha kuwa mimi ni mwalimu mgeni wa Isimani Sekondari, naombeni mniekeze shule ya sekondari ilipo.
Mzee wa kaya hii alisema mwalimu hauna mizigo? Nikasema ninayo, akasema basi wanangu hawa watakupeleka hadi shuleni.
Sasa ilikuwa kama saa nne na nusu usiku na wakati huo barabara ya Iringa Dodoma Ilikuwa ya vumbi na giza kubwa hakukuwa na umeme. Umeme ulikuwa unaishia kiwanja cha ndege ya Nduli tu. Mwanga uliokuwepo ulikuwa ni wa wadudu wanaamulika mulika mithili ya nyota angani au vibatali vya nyumba za wakaazi wa Isimani Tarafani.
Nilipokuwa kwenye lori njiani nilibaini kuwa huko niendapo ni kijijini hakuna umeme nikawa najilaumu kwanini nimebeba kompyuta tena ya desktop si nimekuja kuiharibu bure?
Kumbuka kuwa vijana hawa wananipeleka kwa mkuu wa shule niliwauliza maswali na nilibaini kuwa wengine watakuwa ni wanafunzi wangu. Nikapokelewa vizuri nikapata pa kulala, nikaanza rasmi kazi siku iliyofuata. Mtazamo wangu wa Tanzania ninayoifahamu ni ile ya Mbagala ya kuona umeme tangu enzi.
Hata walimu walionipokea walishangazwa na mwalimu mgeni kuja na kompyuta shuleni wakati hakuna umeme. Lakini baadaye niliamua kuirejesha kompyuta yangu nyumbani. Nilipofika ofisini nilikutana na walimu vijana wawili Lilian Mwamanda na Boniface Kihatura lakini hawa wezangu walikuwa wenyeji wa Iringa kwa kuwa Mwamanda alikuwa akitokea Ifunda na Kihatura alikuwa akitokea Iringa Mjini.
Nakumbuka, Mbunge wa jimbo hili alikuwa ni Ndugu Wiliam Lukuvi ambaye alikuwa akifika shuleni hapo na kuzungumza na walimu huku akizungumza mambo kama ya kufika umeme na hata barabara ya Iringa Dodoma kuweka lami. Ilikuwa kama ndoto kubwa kwa wakati huo. Kwa kuwa nilikuwa namuuliza maswali sana Ndugu Lukuvi alininunulia baiskeli ambayo nilipokea kupitia kwa katibu wake wa jimbo ambayo ilinisaidia kufika kazini mapema.
Swali langu la leo je japokuwa mimi ninatokea mjini, je sina asili ya kijijini? Jibu lake ni kuwa babu yangu alitokea kijijini na kwenda mjini kutafuta maisha kama walivyo wengi wetu.
Nachotaka kusema kuwa watu hawafahamu jambo moja kabla ya uhuru na mara baada ya uhuru watu wengi waliosoma walikimbilia mijini kutafuta kazi. Walipata hizo kazi kwa kuwa walisoma walifahamu umuhimu wa elimu na wakasomesha watoto wao.Watoto hao na wao wakasomesha watoto ambao ni wajukuu.
Hawa watoto na wengine wajukuu hawafahamu lolote juu ya vijijini. Kama wanakwenda wanakwenda likizo kwa babu na wengine hata babu na bibi na zao wako mijini. Kijijini hakuna kilichobakia ni mahame na makaburi ya mababu ambayo mengine hata alama za kuyaambulisha hayana. Wachache sana wanaotambika kama ndugu zangu Waluguru kidogo walikuwa wakiendaenda.
Sasa hawa wanaozaliwa mjini na kusoma wanapomaliza shule wanatafuta kazi hata kazi zikitangazwa watu wakijijini waliosoma wanapata hizo kazi lakini hawawezi kuzijaza wenyewe kwa kuwa huko waliosoma na wenye sifa ni wachache sasa wa Dar es Salaam wanaingia na tena wanakuwa wengi sana. Wanapangiwa kazi vijini wanakwenda kukutana na mazingira mapya kabisa kama yale ya kubeba kompyuta hadi watu wanashangaa.
Ukitangaza kazi wenye sifa wengi ni wa mjini na hata usaili watafaulu sana watapata ajira watapangiwa wakishaanza kazi wanakutana na mazingira magumu ambayo hawayafahamu. Jambo hili ndilo linaleta malalamiko makubwa kuwa vijijini watumishi hawakai iwe zahanati nyingi za serikali zina wahudumu wa afya, waganga na wauguzi wenye sifa wanabaki mjini ukimpeleke kijijini sana anatafuta hosipitali binafsi.
Ndivyo walivyo walimu, shida kwa walimu ajira hakuna kwa hiyo mwalimu akipata kazi kijijini anakaa huko kwa miaka miwili anafanya analofanya anapata uhamisho iwe kwa halali hata haramu anaondoka anarudi mjini ambapo anasema kwako. Pengine kwao kwa asili ni Shinyanga lakini kwa kuwa amekulia Dar es Salaam, sasa huko ni kwao.
Ili kumshawishi mjanja kama huyu wa Dar es Salaam akae kijijini unatakiwa kutumia akili kubwa, kwanza akifika mhakikishie uhakikia wa kukaa huko kijijini kwa muda mfupi na iwe kweli siyo maneno. Pili haki zake zote apatiwe kwa wakati. Hata kama shule aliyepangiwa ni mbali namna gani wapo ambao watapenda kuishi huko hasa wale wajasiriamali, wapenda kilimo na wafugaji. Hapa sasa anaweza akaoa huko au akaolewa na hilo litasaidia kuongeza nguvu vijijini.
Kumbuka kutenda haki kwa wote bila kuwapendelea wengine maana hawa ni wajanja wa mjini wanauliza ehee vipi Mkurungezi? Watu watawaambia yupo kadhaa wa kadhaa bila ya kumficha.
Watumishi hawa kwa kuwa wanafanya kazi katika mazingira magumu jenga urafiki nao na wakija kupata huduma ofisini hawa wawe wa kwanza kusikilizwa na hata wakiwa na shida watakwambia, na hata huko mitaani na vijijini watasema aha mkurungezi ni mtu wetu.
Kama wakishaishi katika maeneo hayo kwa muda mliokubaliana wape uhamisho na walipwe haki zao zote.Sasa wale waliomjini waende kijijini kwa mzunguko
Kumbuka kuwa hawa waliosoma zamani wakistaafu pia wanarudi vijijini, hawa kwa kuwa ni wasomi baadhi yao wenye nguvu wanarudi kufanya siasa wanakuwa madiwani , wenyeviti wa vijiji . Wengine ambao hawataki usumbufu sana wanakuwa wenyeviti wa Bodi/ Kamati za shule, Vituo cya Afya na Zahanati. Kuwa makini hawa wasomi wa zamani wanaporudi makwao wanarudi na watoto wao wa mwisho mwisho na pengine wajukuu. Watoto hawa wa mwisho na hawa wajukuuu ndiyo wanaohamia katika shule za kata na kutibiwa katika zahanati na vituo vya afya.
Hawa ni wasomi wamefaya kazi serikalini na wanaijua serikali vizuri sana. Mathalani miongozi ya utoaji wa elimu bure pengine wao ndiyo walioshiriki kuiandaa, ndiyo walioshiriki kuichapa, ndiyo walioshiriki kukusanya maoni na wana uzoefu mkubwa kuliko hata wewe unayesimamia elimu.
Unapowaambia kwa mmezuia masomo ya ziada lazima kuwe na hoja nzito. Sasa kuna swali je huyo anayetoa kibali shule kufungwa ambaye ni Kamishina wa Elimu Tanzania, je yeye anaye mtoto anayesoma katika shule za kata?
Serikali Kuu haipaswi kuyaingilia mambo ya chini, mambo haya yaachwe kama yalivyo ili watoto hawa wasome na ufaulu uweze kuongezeka ili mradi hakuna sheria inayovunjwa
Labda nishauri mambo haya la kwanza, Uteuzi wa Wakuu wa shule za Sekondari unafanywa na Katibu Tawala wa Mkoa kwa mapendekezo ya Afisa Elimu Mkoa. Jambo hili lifanyike ngazi ya wilaya kwa kuwahusisha Afisa Elimu Wilaya na Wadhibiti Ubora wa Elimu , Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya na Katibu Tawala wa Wilaya wanatosha kuifanya hiyo kazi vizuri kabisa. RAS, Afisa Elimu Mkoa wanapofanya kazi hiyo inatoa nafasi ya majungu tu na umbea na wako mbali na Wilaya.
Pili, hawa Wadhibiti Ubora wa Elimu wote wawe chini ya Mkuu wa wilaya na mapendekezo yao yaishie kwa Mkurungezi tu kufanyiwa kazi na Katibu Tawala wa Wilaya na Mkuu wa Wilaya wasimamie hilo.
Tatu Wadhibiti Ubora wa Elimu wapatiwe vitendea kazi kama usafiri ili weweze kutembelea shule zote kwa wakati.
Nne,Wizara ya Elimu ishughulikie mambo ya sera na mpango haya mambo ya wilayani shule kufungwa ibaki chini ya Maafisa Elimu, Wakurungezi na Wakuu wa Wilaya maana shule zikifanya vibaya wao ndiyo wanaowajibika kujibu siyo Kamishina wa Elimu.
Mwsho naweka kalamu yangu chini nikisema bayana kuwa suala la kuzuia masomo ya saa za ziada siyo sahihi na halikubalikia kabisa. Nakutakia siku njema.
IMEANDIKWA NA ADELADIUS MAKWEGA
Makwadeladaius@gmail.com
0717649257
0 Comments