Kwa hiyo bwana fundi aliniuma sikio juu ya namna kazi hiyo itakavyokuwa kubwa na kazi hiyo itakavyokuwa bora ilimradi zawadi hiyo ya miwani ya mpingo nimpatie Mheshimiwa wetu.
Kuliibuka hoja ya vipimo vya Mheshimiwa, lakini fundi aliniambia kuwa suala hilo tayari ameshalifanyia kazi kwa wajihi wa Mheshimiwa, wala hakutakuwa na shida yoyote.
Nilijiuliza swali, eti pale ningeambiwa lazima upate hivyo vipimo vya wajihi wa Mheshimiwa ingekuwaje? Nikiulizwa swali ndugu wewe unataka kuipima Jamhuri ili uitengenezee miwani suala hilo lingewezekana? Nitajibiwa yakhe Jamhuri huwa haipimwi yakhe! Labda hizo Jamhuri zenu ndogo ndogo.
Lakini bwana fundi, hilo amelimaliza vizuri kazi hiyo inaendelea na amenihakikishia kuwa muunganiko kati ya flemu ya kuwekea vioo na vishikio vya miwani patawekwa kitu kama mpira hivi ambacho kitasaidia sana Mheshimwa miwani yake imkae vizuri sana. Duuu Mheshimiwa atapendeza huyo! Wale wenye gere na Mheshimiwa na miwani yake naomba kaeni kando.
Juzi tu, Mheshimiwa alivalia zile kombati zamabakamabaka, duu Mheshimiwa alipendeza sana na mie nikaona gere, nilitamani sana na mie niwe yule mkuu wa magwanda aliyekuwa kando akapiga picha, huku akimpigia salute Mheshimiwa.
Walipendeza sana nakwambia, sasa Mheshimiwa atavunja rekodi pale atakapotiwa miwani yangu ya mpingo akivaa na zile kombati za juzi, duuu Mheshimiwa atapendeza sana.
Fundi wangu aliniuma sikio kuwa miwani ya Mheshimiwa itatakiwa kuwa katika jozi nne za kwanza, ndugu yangu fundi amenijulisha pia kutatakiwa kumtengenezea Mheshimiwa huyu jozi nyengine za miwani mitano.
Mie pangu pakavu tia mchuzi hiyo gharama ya mti wa mpingo ni kubwa na lazima mti huo uwe umekauka vizuri. Lakini nguvu imekuja baada ya kuupata mpingo uliokauta kutoka huku kwetu mikoa ya pwani ya Tanzania kwenye pori letu la urithi ambapo nilishamkabidhi fundi wangu.
Kwa hiyo, kwa sasa maandalizi yangu ni kukamilisha jozi nne ambazo mahitaji yote yapo tayari kukamilisha jozi tano zilizosalia na nitayaanda kwa utaratibu panapo majaliwa nitakamilisha hapo baadae ilimradi nikamlishe zawadi hii ya miwani kwa Mheshimiwa.
Miwani hii ya mpingo nilikutajia sharti la kwanza, leo nakutajia masharti mengine mawili Mheshimiwa anapaswa kuivalia na na suti ya rangi ya samawati. Natambua Mheshimiwa anapendelea suti zile zenye sarawili na koti la juu lefu. Mheshimiwa sasa atatakiwa kuvaa suti za rangi hiyo tu, duu Mheshimiwa atapendeza sana.
Fikiria Mheshimiwa pale anapokwenda kulikagua gwaride na suti ya samawati na miwani ya mpingo wacha wee, wenye gere shauri yao, mheshimiwa atapendeza sana.
“Sasa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan analikagua gwaride la miaka 62 ya Muungano wa iliyokuwa Tanganyika na Zanzibar pale, Mheshimiwa amevalia miwani ya mpingo inayopendeza sana ambayo ina lenzi mbili mbonyeo na mbinuko, huku Mheshimiwa amevalia suti zake azipendeza zenye koti lefu na sarawili, Mheshimiwa amependeza sana naona Mkuu wa Majeshi pale akimuongoza Mhesmiwa rais…”
Haya ni fikria tu ya maneno yanasemwa na mtangazaji atayatangaza tukio hilo. Suti hii ya rangi ya samawati itakuwa ndiyo signature suit ya Mheshimiwa wetu.
Sharti la tatu la miwani yangu ya mpingo haitatakiwa Mheshiwa wetu kuvalia suti yenye maua maua yaani suti ikiwa na maua na miwani yangu ya mpingo hapo itakuwa tabu maana nyuki wasijemvamia Mheshimiwa. Yaani jamhuri iumwe na nyuki? Hilo halikubaliki.
Kuwa makini kama unapenda kuvaa nguo zenye maua maua ndege na nyuki wana desturi ya kuyafuata maua hayo.
Maana kuna siku niliwahi kulala katika hoteli moja kubwa kwa kuwa nilikuwa safarini niliona kupitia dirisha la chumba changu cha hoteli hiyo kilichokuwa na pazia lenye maua maua ndege walijaa sana wakidhani kuwa ni maua halisi ya kweli, kumbe walikuwa wakigonga kioo, siku hiyo usingizi ulikata mapema sana kwa kelele za kukigongagonga kioo cha dirisha langu.Mie mwana wa kabwela mambo haya nilikuwa siyafahamu maana madirisha yetu ya miti na majani ndege wakitaka kuingia ndani ya nyumba wanaingia na kutoka, ofa ya kulala kwenye nyumba za wageni za kifahari nilijifunza ndege walivyo wasumbufu sana.
Kwa hiyo ili kuepusha ndege na nyuki kumsumbua Mheshimiwa hatatakiwa kabisa kuvaa suti zenye maua maua. Kwa hiyo naendelea na kazi ya kuikamilisha zawadi ya miwani ya mpingo ya Mheshimiwa Rais.
makwadeladius@gmail.com
0717649257
0 Comments