Header Ads Widget

WADAU WA MAENDELEO WATAKIWA KUPUNGUZA SHUGHULI ZINAZOZALISHA KABONI

SERIKALI na wadau wa maendeleo wakiwemo wawekezaji wametakiwa kuchukua hatua madhubuti ili  kupunguza au kuondoa shughuli za kimaendeleo ambazo zinazalisha hewa ya kaboni inayosababisha mabadiliko ya tabianchi. 

Akizungumza na waandishi wa habari Mjini Kibaha Rehema Peter ambaye ni mwasisi na mkurugenzi wa taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Partnership Green for Future (PGF) ya Jijini Dar es Salaam ambayo inapambana na vitendo vya uharibifu wa mazingira vinavyosababisha mabadiliko ya Tabianchi alisema mabadiliko hayo ya hewa yamesababisha kuwe na joto na jua kali.

Peter alisema kuwa wanapinga uwekezaji wa kwenye uzalishaji wa gesi ya ukaa na uchimbaji makaa ya mawe ambavyo ndiyo vyanzo vikuu vya uzalishaji wa hewa hiyo ya kaboni na uzalishaji wa bidhaa za plastiki.

Aidha alisema kuwa uchimbaji wa makaa ya mawe utaratibu na uzalishaji wake unaharibu hali ya hewa na kusababisha mabadiliko ya tabianchi hivyo watunga sheria na sera watunge sheria kali kupunguza uzalishaji wa hewa hiyo mbaya.

Kwa upande wake ofisa sera na uragbishi kutoka shirika la WWF Nuhu Salasala alisema moja ya kundi linaoathirika na mabadiliko ya tabianchi ni watoto na akina mama hivyo wao wakipata elimu itasaidia kudhibiti taka ngumu zikiwemo plastiki.

Naye mratibu wa shirika la Extinction Rebellion Tanzania Shamim Nyanda alisema kuwa tuna uwezo wa kutunza na kuhifadhi mazingira kwa kufanya usafi wa bahari na urejeshaji wa uoto wa asili kwa kupanda miti na kuwashirikisha wanafunzi ili waweze kuyatunza mazingira.

Naye Salma Ramadhan ambaye ni mlemavu wa ngozi alisema joto na jua kali linaathiri ngozi zao na kupata madoa pamoja na kansa hivyo jamii inapaswa kuhakikisha inatunza mazingira na kupanda miti.

Awali akisoma taarifa ya PGF James Mhanga alisema madhara ya plastiki ni mengi ikiwa ni pamoja na vifo vya wanyama wanapokula plastiki hizo na husababisha magonjwa ya kansa inapotumika kubebea chakula hasa cha moto, magonjwa ya mapafu kwa watoto, kuharibu makazi ya chakula cha samaki huku kwenye udongo hubadili uhalisia wa udongo hivyo kupata chakula hafifu na kuharibu mifumo ya uzazi kwa wanaume na wanawake.

Pia taasisi hiyo na nyingine pamoja na wanafunzi wa shule za sekondari Kibaha,Tumbi na shule ya Msingi Tumbi walishiriki shughuli hiyo na waliunga mkono mkutano wa kimataifa unaopambana na mabadiliko tabianchi cop 26 unaofanyika Glasgow Scotland. 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI