MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma ya Nishati na Maji Tanzania (EWURA)imetoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wafanyakazi wa Tanesco wa mkoa wa Ruvuma ili yawasaidie kufanya kazi kwa weredi zaidi pamoja na kujenga uelewa wa pamoja. mwandishi wa matukio daima Amon Mtega anaripoti kutokea Ruvuma.
Akizungumza kwenye mafunzo hayo mwakilishi wa mkurugenzi mkuu wa Ewura Titus Kaguo alisema kuwa kumekuwepo na baadhi ya wafanyakazi wa Tanesco kutokuzingatia taratibu za utendaji kazi jambo ambalo limekuwa likisababisha madhara katika utoaji wa huduma za umeme.
Kaguo ambaye pia ni meneja mawasiliano wa Ewura alisema kuwa kufuatia mafunzo hayo kwa wafanyakazi wa shirika la Tanesco yatawafanya waweze kubadilika na kufanya kazi kwa weredi zaidi ikiwemo na kuwatambua wakandarasi au mawakala ambao wenye leseni za Ewura wanaostahili kutoa huduma za wayaringi kwenye Nyumba za watu na kuwabana wale ambao hawasatahili .
Alisema kuwa kumekuwepo kwa baadhi ya hasara zilizokuwa zikitokea ikiwemo kuwaka majumba moto kwa sababu ya kutumia mafundi ambao hawana leseni za utambulisho wa kazi hizo.
Aidha alisema kuwa licha ya kuwapatia mafunzo haya kwa wafanyakazi wa Tanesco mkoani Ruvuma lakini Ewura itatoa mafunzo pia kwa mawakala wa Tanesco wanaotoa huduma za wayaringi kwenye majengo mbalimbali ya Serikali na Wananchi ili waweze kufuata taratibu.
Kwa upande wake meneja wa Tanesco mkoa wa Ruvuma mhandisi Florence Mwakasege aliipongeza Ewura kwa kutoa mafunzo hayo kwa wafanyakazi wa Tanesco ili kujenga uelewa wa pamoja.
Meneja Mwakasege pia alieleza changamoto ambazo ofisi yake inakutana nazo kwa baadhi ya mawakala kugonga mihuri kwenye fomu za wateja wanaotakiwa kuingiziwa umeme bila hata kwenda kuangalia mazingira ya nyumba hizo jambo ambalo limekuwa likiibua migogoro baina ya wateja na ofisi ya Tanesco pindi savea anapoona kuna makosa kwenye nyumba hizo.





0 Comments