Header Ads Widget

VITALIS MAEMBE NA KIBONZO KATIKA UKUTA WA KANISA





Tulikuwa wanafunzi kama 200 wa mafundisho hayo na mwanzoni tukifundishwa na mwalimu mmoja akifahamika kama Katekista Mbunda. Mwalimu huyu alikuwa mkali sana hasa kwa wale waliokuwa wakichelewa mafundisho hayo ya Komuniyo ya Kwanza nakumbuka bakora zilichapwa mno kwa wachelewaji........Na ADELADIUS  MAKWEGA DODOMA



Kwa Ukatoliki Komuniyo ya Kwanza ni miongoni mwa sakramenti saba za Kanisa hilo ikitanguliwa na ubatizo.


Kisingizo cha kuchelewa mafundisho kilikuwa “ahaa sie tulichelewa kutoka shuleni” Hapa Katekista Mbunda alikuwa akiuliza nani anasoma shule ya Msingi Mnazi Mmoja? Kweli katika kundi la watoto 200 walikuwepo watatu wanne waliosoma huko na wao wenzako kama waliwahi bakora lazima uchapwe. 


Katekista huyu alikuwa akiita majina ya mahudhurio kila siku ya mafunzo hayo, kwa hiyo majina ya wenzako utayajua tu hata kama si rafiki zako kwani utalisikia tu. Kwa kuwa darasa hilo lilikuwa na watoto wengi tulisikia tu tumegawanya katika makundi mawili, moja A akifundisha Sista Getruda (Mchaga) na lingine B akifundisha Sista Theresia (Mmakonde).


Mafunzo ya masista hawa yaliendelea vizuri kwani bakora zilikuwa hazipo ikawa tofauti na Katekista Mbunda lakini masista hawa walikuwa wakifinya watoto watundu. Maana katika darasa la watoto wa umri wa miaka 10-15, A wako 100 na B wako 100 lazima watundu na wakorofu walikuwepo.


Mafunzo haya yaliendelea vizuri sana na mara tulipokuwa tunakaribia kuhitimu ili kupata Komuniyo ya Kwanza ilibuka balaa kuwa kuna mmoja wetu amechora picha ya masista wanaotufundisha na kusema kuwa hawa ni masista shetani. Mchoro huo ulichorwa katika ukuta wa nje ya kanisa dogo ambapo mafundisho yalikuwa yanafanyika na ndipo tulipokuwa tunasali kila siku.


Swali lililoibuka ni nani amechora picha hizo ukutani kwa kutumia kalamu ya risasi na kuandika maneno hayo? Maneno haya yaliwakwaza mno watawa hawa wa kike ambapo walikuwa ni mabinti labda wa miaka kama 19 au 20. Wakati walikuwa wakifundisha mafundisho ya kiroho ya dini yetu alafu wanaofundishwa wanasema masista shetani?


Sasa kazi ikawa ni kumsaka aliyefanya hivyo. Kazi ya kwanza ilikuwa ni kumtambua nani anayependa kuchora au anayeweza kuchora miongoni mwetu watoto 200? Katika kundi hilo la watoto wa Mbagala na Mtoni Mtongani mchoraji maarufu alikuwa Vitalis Maembe ambapo wakati huo alikuwa akifahamika kama Matias Vitalis. Kwa hiyo kwa anayesoma matini hii pale ninapomtaja Matias Vitalis Kumbuka ndiye Vitalis Maembe.


Kwa hiyo mtuhumiwa nambari moja alikuwa Matias Vitalis, Lakini kweli yeye ndiye alichora na kuandika maneno hayo yaliyowakwaza watawa hawa wawili? Sista Getruda aliyependa kuvaa miwani alikuwa mkubwa zaidi ya Sista Theresia, hawa walikuwa watawa wa mwanzo mwanzo wa Shirika la Dada Wadogo ambalo lilianzishwa na Marehemu Kadinali Laurian Lugambwa mwishoni mwa miaka 1980.


Watawa hawa wa kike walitokwa na machozi kwa tukio hilo lakini watoto watundu na watukutu walifurahi sana kuona matone ya machozi ya masista hawa, kumbe na wao wanalia?


Kosa hilo kwa kuwa liliwakwaza watawa hawa wa Shirika la Dada Wadogo walimshirikisha Padri wa eneo hilo Padri Fidelis ambaye alikuwa babu wa Kiitaliano mwenye ndevu nyingi. Padri huyu alisema bayana kuwa kwa kosa hili basi mwaka huu 1988 hatutapata Kumoniyo ya Kwanza, itasogezwa mbele au tusipate kabisa. Labda tuumtaje nani alifanya kosa hilo.


Hoja hiyo ilikuwa mtihani maana unatoka shuleni kwenda kanisani kila Jumanne, Jumatano, Jumamosi na Jumapili ibada ya watoto jioni upo kanisani, alafu mnaambiwa hamtopata Komuniyo ya Kwanza, daa ilikuwa balaa maana tulishasoma kwa mwaka sasa.


Kauli hiyo ya Padri iliweza kuwaibua wale walioshuhudia baada ya kuanza kuitwa mmoja kwa padre na watawa hawa kweli kila mmoja wetu aliulizwa na tamati ya yote alitajwa mhusika kwa ushahidi na siku aliyofanya tukio hilo.


Katika kutajwa huko Je alitajwa Matias Vitalis? Hapana, alitajwa ndugu mmoja ambaye alikuwa akifahamika kama Angetile huyu alikuwa kijana anayetokea Mtoni Relini kama unaelekea Tandika.


Ilibainika kuwa siku moja tukiwa tunasali Angetile na wadada wawili mmoja akiitwa Keti na mwingine jina silikumbuki walitoka nje ndipo wakaifanya kazi hiyo ya kuwakwaza watawa hawa, kwani walikuwa wakilipiza kisasi kutokana na kufinywa na masista hao. Angetile, Keti na dada mmoja wa tatu walipoitwa waliomba msamaha na kuungama kwamba ndiyo waliofanya kosa hilo na kusema siyo Matias Vitalis.


Kwa hiyo ndugu yangu Matias Vitalis aliingia katika shida hiyo kwa kuwa ujuzi wake tu ulimponza na kuhusishwa kuwa ndiye aliyechora katuni/kibonzo hicho katika ukuta wa kanisa. Kesi hiyo ilikwisha kwa watoto wote kuwaomba msamaha watawa hawa, padre na kwa Mungu. Tukaendelea na mafundisho yetu hadi tukapata sakramenti hiyo mwaka 1988.


Ninalikumbuka tukio hili leo hii ikiwa ni miaka kama 33 na sina hakika kama ndugu yangu Matias Vitalis anakumbuka balaa hili. Nalitaja tukio hili leo kwa sababu, Novemba 27, 2021 nilipata ujumbe kutoka kwa mtu mmoja mwenye namba hii 0754747570 akiniambia kumbe Vitalis Maembe ni jamaa yako, hivi sasa ana shauri huko Polisi Chalinze mwambie abadilike, mimi ninachukiwa sana na mtu kuwa mpingaji (Critics) bila ya kupumzika. Ndugu huyu aliendelea kutoa maelezo mengi marefu. 


Nilimjibu kuwa ni kweli ni rafiki yangu na kama ndugu yangu, tunaongea vizuri, pale panapokuwa na jambo nikimshirikisha anashiriki, liwe binafsi au hata la kikazi. Kisiasa yeye anaamini katika upinzani na mie naamini katika CCM, haya yalikuwa majibu yangu.


Ndugu huyu aliendelea akasema kuwa amemwambia rafiki yake mwingine wa Vitalis Maembe ambaye ni mdhamini wake kuwa si mara zote anatakiwa kupinga, nyimbo zake zote ni kupinga tu aache tabia hiyo.


Ndugu huyu alitolea mfano tukio lililotokea huko TASUBA tamasha la 2021 akiwa ametanguliwa na makundi kama Rod Eyes, Vitalis Maembe aliropoka kuwa watu wa mjini wamekula muda weo. Huku kukiwepo waheshimiwa kadhaa.


Mimi binafsi siku hiyo sikuwepo katika tukio hilo lakini, Je ni kweli VItalis Maembe ni Mkorofi? Je ni kweli nyimbo zake nyingi zinaikosoa serikali? Kama ni kweli, Je kufanya hivyo kisanaa ni kosa? Je Vitalis huwa hashirikiani na serikali katika kazi mbalimbali za maendeleo?


Kwa ukweli wa Mungu Vitalis Maembe si mtu mkorofi ila baadhi ya watu wanashindwa kumuelewa kwa kitu kimoja tu namna anavyoufanya muziki wake. Muziki wake ni wa wanyonge na mara zote ajenda zake si za mabwenyenye. Ifahamike wazi kuwa Vitalis ni mchoraji mzuri katuni lakini aliacha kuchora katuni akaamua kuimba nadhani ili kuwa na uwanja mkubwa wa kuisemea hii jamii ya wanyonge.


Hili msomaji wa matini hii kumfahmu vizuri Vitalis Maembe nimeeleza juu lakini fahamu pia makazi ya familia ya Maembe(alipokuli) ambao ni Wafipa yalikuwa Mtoni Relini wakati huo walikuwa na nyumba tatu, mbili ziko jirani na Msikiti wa Maboksi na kutoka kwao ni umbali usiozidi mita mia tatu na Kituo Kidogo cha Polisi Mtongani, sina hakika kama hata kituo hicho cha polisi kina rekodi ya ukorofi wa ndugu huyu. 


Huyu ni Mtanzania mwezetu, ambaye anafanya kazi ya Sanaa ya muziki kwa namna ya kipekee hivyo hatupaswi kumkatisha tamaa bali kumtia moyo. Vitalis Maembe ana nyimbo nyingi ambazo zinatumia lugha ya picha kama vile Majamvi, Afrika Shilingi Tano, Sumu Teja, Vuma, Kaizari, Kudu, Nchi Yangu na nyingine nyingi. 


Kazi hiyo ya sanaa inaweza kuonekana kumgusa mtu fulani lakini kumgusa mtu ni mawazo ya yule anayeisikiliza au kuitazama kazi hiyo. Kwa kuwa hii ni sanaa wapo wasanii wengine wanaotunga mashairi, wengine vitabu na wengine michezo ya kuigiza hatuwezi kusema kuwa ukitunga jambo fulani wasomaji wakulihusisha na kundi fulani la watu kuwa ni kosa au huo ukorofi.


Kuna ndugu anaitwa Mohamed Seif Khatibu alitunga Kitabu cha Wasaka Tonge kuna mambo mengi ya ukosoaji wa serikali ndani yake. Hakukamatwa na kutiwa ndani na huyu alikuwa kiongozi wa UVCCM wa nagzi za juu wakati huo, hii ilikuwa ni kazi ya sanaa tu. 


Vitalis Maembe amekuwa akishirikiana na serikali za maeneo mbalimbali hasa kwa ngazi za wilaya na amekuwa ni msanii mwepesi kupokea wito na mwepesi kuelewa kwa kuwa serikali haifanyi biashara mara nyingi amekuwa akishiriki katika kazi za kuelimisha jamii ambazo kwa hakika ni kwa ustawi wa binadamu na kwa maslahi ya binadamu mathalani kutoa Elimu ya Afya. Rushwa, Elimu ya Kilimo na Ufugaji.


Naweka kalamu yangu chini kwa siku ya leo, kwa kusema kuwa kitendo cha kupata misukosuko Vitalis Maembe ni sawa na kitendo kile alichofanyiwa tukiwa wadogo kusingiziwa kuwa ndiye aliyechora kibonzo cha watawa katika ukuta wa kanisa.


Kitendo cha kuheshimu sanaa yake na kumuacha afanye kazi hii vizuri na kumshirikisha katika matamasha mbalimbali kitakuwa sawa na kile kitendo cha Padre Fidelis na watawa wale wa kike walipochunguza na kubaini kuwa VItalis Maembe hakufanya kosa hilo bali ni Angetile. 


Kibinadamu kila mmoja wetu ni mkosaji kama kuna jambo ambalo halijakaa sawa ni vizuri kukaa na ndugu huyu na kulimaliza bila ya kumuumiza. Nakutakia siku njema.


makwadeladius@gmaiil.com

0717649257

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI