Imeelezwa kuwa vifo vya wanandoa vitokanavyo na wivu wa mapenzi Kwa kipindi cha Januari – Oktoba mwaka huu 2021 mkoani Shinyanga vimefikia watu 12. mwandishi wa matukio daima Mapuli Misalaba anaripoti kutokea Shinyanga
Takwimu hizo zimetolewa na kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga kamishna msaidizi wa Polisi George Kyando alipozungumza na Matukio Daima Media.
Kamanda Kyando alisema idadi kubwa ya matukio hayo yanatekelezwa na wanaume na kwamba chanzo ni wanandoa kutuhumiana kuhusu suala la uaminifu.
“Kipindi cha Januari hadi Oktoba 2021 kwa mkoa wa Shinyanga kumekuwa na ongezeko kubwa la mauaji yanayotokana na wivu wa mapenzi kwa mwaka huu jumla ya mauaji 12 yametokea ambayo chanzo chake ni wivu wa mapenzi na kati ya hayo ni moja tu ambalo mwanamke alimuua mwanaume kwa wivu wa mapenzi na wengiwao wanawatuhumu wenzi wao kwamba siyo waminifu wa ndoa ambapo mwaka jana matukio kama haya yalikuwa 4 tu ya wivu wa mapenzi”. Alisema
Hata hivyo kamanda Kyando alisema Mkoa wa Shinyanga umefanikiwa kukomesha mauaji ya vikongwe, albino na vifo vinavyosababishwa kulipiza kisasi.
Wakati huo huo kamanda Kyando alisema licha ya kupungua kwa matukio kama hayo lakini hali ya usalama katika Mkoa wa Shinyanga ni shwari ambapo ameonya pia kuelekea mwisho wa mwaka Jeshi hilo limejipanga kuhakikisha hali ya amani, utulivu, usalama wa raia na mali zao inaendelea kuwepo.
“Tabia ya matukio mbalimbali kuongezeka Jeshi la Polisi tumejipanga kukabiliana na hali hiyo hatutaruhusu hata kidogo tumejipanga kwa upande wa usalama barabarani hata kwa waharifu ambao wanategemea mwisho wa mwaka nawaonya wajue Jeshi lao tukoimara hatutaruhusu matukio mabaya mkoa wetu ole atakae jaribu kitakachompata atakuwa fundisho kwa wengine waliokuwa na mawazo kama hayo”.
Kwa upande wake mchungaji wa kanisa la AICT Kambarage mjini Shinyanga Charles Lugembe alisema baadhi ya ndoa zinakuwa zikiteteleka kutokana na wahusika kutokuwa makini katika mahusiano yao.
“Matokeo ya anguko la mwanadamu taasisi ya ndoa imekuwa ikishambuliwa sana hata wakristo katika kanisa wanashida hiyo jinsia au mapenzi yanapotumika vibaya lazima ugomvi, wivu, watoto nje ya ndoa na mauaji yatokee haya yote ni matokeo ya dhambi na hii ni kwa sababu tu watu wameshindwa kujua matumizi mazuri na sahihi ya mapenzi”.
Mchungaji Lugembe alisema watu wanaoishi katika ndoa wanatakiwa kuwa waaminifu,waadilifu na wenye kumshirikisha Mungu katika maisha yao, hali ambayo itachangia kuimarisha mahusiano yao na kudhibiti migogoro inayosababisha vifo pamoja na madhara mengine.
Aliwaasa wanandoa kuzingatia viapo na mafundisho ya dini katika imani zao kwani ndiyo silaha ya kulinda na kuimarisha mahusiano katika ndoa.
“Msaada mwingine kwa wanandoa ili wabaki katika nafasi nzuri ya mzunguko wa maisha ni kuheshimu viapo vinavyotolewa kanisani vinaweka mhuri katika moyo wa mtu sasa unapokiuka unatafuta mhuri mwingine tayari inaleta shida yakutokuaminika wivu wa Mungu unaweza kutufundisha namna ya kuwapenda wake zetu au waume zetu lazima uwe na wivu na hali ya kumpenda mke wako lakini wivu wa kumchukia ni mbaya na inapelekea vifo hivyo mke wako au mme wako ikitokea amekiuka basi uwepo msamaha kuombeana msamaha ni jambo la msingi kwa sababu msamaha unaweza kutoa hali ya mauaji”.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi katika Manispaa ya Shinyanga walisema kuporomoka kwa maadili na jamii kukosa hofu ya Mungu ni moja ya sababu ambayo imekuwa ikisababisha migogoro baina ya wanandoa na baadaye vifo vinavyotajwa kuwa chanzo chake ni wivu wa mapenzi.
Wananchi hao walishauri kwamba ili kudhibiti vifo vinavyotajwa kusababishwa na wivu wa mapenzi ni wajibu wa wanandoa kuishi maisha ya uadilifu na kumshirikisha Mungu ili kujenga familia bora yenye amani, na upendo.
0 Comments