WAZIRI wa Madini Dotto Biteko amesema serikali itatuma wataalamu kutembelea eneo linalochimbwa Madini ya Caolin (Dongojasi) baada ya kampuni ya Pugu Kaolin Mines Ltd kutopata kibali cha uchimbaji kwa kipindi cha miaka sita.
Akizungumza baada ya kutembelea eneo hilo ambalo liko kwenye kata ya Kisarawe wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani ndilo lenye utajiri mkubwa wa Kaolin na linakisiwa kuwa na tani milioni 800 ambazo ni nyingi sana na haziwezi kumalizwa kwa haraka.
Biteko alisema kuwa baadhi ya maeneo ya uchimbaji yako kwenye hifadhi za misitu lakini kuna taratibu ambazo zinapaswa kufuatwa ili kufanya uchimbaji.
"Hoja kuwa machimbo yako kwenye hifadhi ya msitu wa hifadhi ya Pugu Kazimzumbwi inabidi iangaliwe kwani baadhi ya machimbo makubwa mfano GGM, Tulawaka Biharamulo , Saadan Bagamoyo wanakochimba chumvi kwenye hifadhi ya wanyama shughuli zinafanyika Kisarawe shida ni nini"alisema Biteko.
Naye mkuu wa wilaya ya Kisarawe Nickson Simon alisema kuwa wanasubiri tamko ili kujua hatma ya eneo hilo kwani mbali ya kuingiza mapato pia litatoa ajira kwa vijana.
Kwa upande wake Douglas Mwela ofisa Mazingira wilaya ya Kisarawe alisema kuwa wilaya hiyo ina migodi sita ya machimbo ya Madini hayo ambapo kwenye bajeti ya mwaka 2019/2020 Madini hayo yaliingizia Halmashauri kiasi cha shilingi milioni 270 na mwaka 2021yaliingiza milioni 288 ambapo madini ya Kaolin yanayotumiwa kwenye viwanda vya Keda cha Chalinze na Mkuranga vyote vya marumaru ndiyo vinatumia Madini hayo ambayo ni bora duniani.
0 Comments