Waziri wa kilimo, Prof Adolf Mkenda amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita kuanzia mwaka 2016/2017 hadi 2020/2021 uzalishaji wa mazao ya chakula umeongezeka kutoka tani milioni 15.9 hadi kufikia tani 18.4 milioni. mwandishi wa matukio daima Teddy Kilanga anaripoti kutokea Arusha
Akizungumza jijini Arusha katika kikao cha wadau wa kilimo, Prof Mkenda alisema uzalishaji wa mazao ya nafaka umeongezeka kutoka tani milioni 9 hadi kufikia takribani tani milioni 10 hivyo kwa kuzingatia uzalishaji na mahitaji ya chakula nchini katika kipindi hicho ziada ya chakula imeongezeka kutoka tani 2.6 kwa mwaka 2016/2017 hadi tani takribani milioni 3 kwa mwaka 2020/2021.
Aidha Prof. Mkenda aliongeza kuwa kutakuwa na changamoto ya hali ya hewa nchini hivyo inatarajiwa kuwa na changamoto ya uzalishaji wa hapa na pale hivyo wakuu wa mikoa nchini wamepewa taarifa hiyo na kuwapa maelekezo ya namna ya kuwasaidia kuwapa elimu wakulima kulima mazao yanayoendana na hali ya hewa.
"Pamoja na Changamoto hiyo,wataalamu wanatuambia bado tutakuwa tunajitosheleza kwa chakula hapa nchini ila ni muhimu kwa wananchi kuzingatia maelekezo yatakayotolewa na wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kulima kilimo ambacho watashauriwa ili kuzalisha mazao yanayohimili upungufu wa mvua,"alisema Prof.Adolfu Mkenda.
Sambamba na hilo alisema upatikanaji wa mbegu bora nchini umeongezeka kutoka tani elfu 10946 kwa msimu wa 2014/2015 hadi kufikia tani 77252.45 kwa msimu wa 2019/2020 ambapo ni sawa na ongezeko la asilimia 86.8, upatikanaji huo umechangiwa na kuongezeka kwa uzalishaji wa mbegu zilizothibitishwa ubora ndani ya nchi kutoka tani 4337 hadi 61893.23 sawa na ongezeko la asilimia 80.
Pia alisema serikali imeendelea kuwezesha vituo vyake vya utafiti kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa aina mpya wa mbegu bora za uzalishaji hivyo mpango wa kuendeleza kilimo awamu ya pili unasisitiza masuala ya uendelezaji wa kilimo chenye tija katika kilimo biashara kwa kuboresha mapato ya mkulima kitachomuhakikishia uhakika wa chakula na lishe.
"Ni wajibu wetu sisi sote kuendeleza juhudi hizo na hapa natoa wito kwa halmashauri zote kutenga maeneo kwa ajili ya uzalishaji mbegu kwani bado sekta hiyo inahitaji kushikwa mikono,"alisema Waziri huyo.
Hata hivyo mbunge wa jimbo la Madaba ambaye ni mdau wa kilimo katika sekta ya mbegu, Dkt. Joseph Mhagama alisema changamoto wanazozipata katika maeneo mengi ni pamoja na matumizi sahihi ya mbegu ambayo hupelekea kuzalisha mazao machache kwani hutumia gharama kubwa.
"Lakini kwa kuboresha mbegu zenye tija itawasaidia kutumia ardhi ndogo na kuvuna mazao mengi ,"alisema.





0 Comments