Header Ads Widget

PONGEZI ZA THBUB KWA SERIKALI KUHUSU WANAFUNZI WALIOKATIZA MASOMO KUREJEA SHULENI

NOVEMBA 24 mwaka huu, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako na kupitia Waraka wa Elimu Na. 2 wa mwaka 2021 uliotolewa siku hiyo hiyo ilitoa tamko kuhusu kurejeshwa shuleni kwa wanafunzi waliokatiza masomo katika elimu ya msingi na sekondari kwa sababu mbalimbali.

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) kama mdau katika masuala ya haki za binadamu imefurahishwa sana na uamuzi huo na inapenda kutumia fursa hii kutoa pongezi zake za dhati kwa Serikali kwa hatua yake hii muhimu inayowahakikishia watoto wote nchini haki yao ya msingi ya kupata elimu bila ya ubaguzi wa aina yoyote.

Kwa mujibu wa tamko la  Waziri na Waraka uliotolewa, watoto watakaokatiza masomo kutokana na utoro, utovu wa nidhamu, kupata ujauzito na wale waliofeli shule ya msingi sasa wanayo fursa ya kurejea katika mfumo rasmi wa elimu na kuendelea na masomo yao kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa.

Hatua hii ni ya kupongezwa kwa sababu inazingatia matakwa ya kisheria ya kimataifa kwa Serikali zote kutoa elimu kwa watoto wote bila ya ubaguzi wowote. Pia, inaiondoa Tanzania kutoka katika kundi la mataifa machache wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) zinazoendelea kuwatenga wasichana wajawazito kupata elimu.

Uamuzi huu pia ni hatua nzuri ya utekelezaji wa Mkakati wa Maendeleo ya Kiuchumi na Kijamii wa Bara la Afrika (Ajenda 2063) unaodhamiria kujenga mtaji wa rasilimali watu kupitia uwekezaji endelevu katika elimu.

Vilevile ni utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs) yanayolenga kuhakikisha kuwa hakuna anayeachwa nyuma katika maendeleo na kuhakikisha elimu jumuishi na bora kwa wote.

Pamoja na hatua hii nzuri ya kuondoa vikwazo vya upatikanaji wa elimu kwa watoto nchini, Tume inapendekeza yafuatayo:

1. Serikali ikae pamoja na wadau mbalimbali wa elimu kuandaa na kupitia sera, sheria, mikakati na miongozo itakayosimamia utekelezaji wa azma hii kwa madhumuni ya kuihuisha mifumo yote ili iweze kuendana na Waraka wa Elimu Na. 2 wa 2021;

2. Serikali iweke mazingira wezeshi kwa watoto wanaorejea shuleni kuendelea na masomo baada ya kujifungua. Hii inajumuisha kutokuwepo na unyanyapaa na ubaguzi na kuwaruhusu wanafunzi waliojifungua kuchagua shule mbadala ya kuendelea na masomo;

3. Serikali kwa kushirikiana na wadau waielimishe jamii na hususan wanafunzi walioko shuleni kutowanyanyapaa watoto wanaopata ujauzito wakiwa shuleni na waliojifungua;

4. Wazazi, viongozi na jamii kwa ujumla, waongeze nguvu katika kutoa na kusimamia malezi bora ili kutokomeza mimba katika umri mdogo;

5. Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali waendelee kuielimisha jamii kuhusu madhara ya mimba katika umri mdogo pamoja na umuhimu wa wasichana wajawazito na waliojifungua kuendelea na masomo;

6. Wadau wa Elimu na Wananchi kwa ujumla waongeze jitihada katika kusimamia utekelezwaji wa Sheria katika kuwalinda watoto ili waweze kumaliza masomo yao shuleni.


Imetolewa na:

(SIGNED)


Mohamed Khamis Hamad

Makamu Mwenyekiti


TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA


Novemba 29, 2021

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI