Ulevi uliokithiri sambamba na unywaji wa pombe saa za kazi kwa baadhi ya vijana mkoani Kilimanjaro kumetajwa kuwa ni kikwazo kwa vijana kushindwa kupata ajira katika baadhi ya miradi inayondelea kutekelezwa katika maeneo mbali mbali mkoani humo. Mwandishi wa Matukio Daima Gift Mongi anaripoti kutoka Moshi
Baadhi ya vijana hao kwenye maeneo mbalimbali kunakotekelezwa miradi hiyo wameelezwa kudhoofu kutokana na unywaji pombe na wengine wakishindwa kubeba kitu chenye uzito wa kilo kumi jambo linalopelekea vijana kutoka mikoa jirani kuweza kunufaika tofauti na ilivyotegemewa.
Elikunda Msaki ni mwenyekiti wa chama Cha wakandarasi(CATA)mkoa wa Kilimanjaro ambapo alisema suala la ulevi kupiindukia miongoni mwa vijana kumepelekea kushindwa kuwapatia ajira katika miradi mingi hali inayowalazimu kwenda kutafuta vijana mikoa ya Manyara na Arusha.
"Wengi wao asubuhi tayari wamelewa hata kubeba kitu hawezi Kuna kipindi nilikuwa na mradi nikahitaji nguvu kazi ya vijana maeneo ya hapa hapa Kilimanjaro sikupata kila anayekuja kalewa na ni asubuhi ikabidi niende Manyara kutafuta vijana"alisema
Kwa mujibu wa Msaki ambaye pia ni mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Sammy Construction Ltd ni kuwa sio wakandarasi hawapendi kuwaajiri vijana sehemu wanapoenda kutekeleza miradi ila tatizo ni hilo la ulevi na kuwa hali hiyo isipochukuliwa hatua athari mbaya zitajotokeza kwa siku za mbeleni kwa kuwa na watu tegemezi wasio na ulemavu wowote.
"Sisi tunapata miradi lakini pia tunatarajia tunapaoenda kuitekeleza wazawa wa eneo husika nao wanufaike huo ndio mgawanyo wa riziki lakini mambo ni kinyume kama unaweza kwenda sehemu asubuhi unawakuta vijana kama 40 wote wamelewa huoni tayari ni tatizo hili?"alihoji Msaki
Celis Mosha ni diwani wa kata ya Kilema Kati ambapo alisema suala la ulevi katika eneo lake kwa sasa limekuwa ni janga kama yalivyo majanga mengine ambapo nguvu kazi ya taifa imemalizwa na unywaji wa pombe ikiwemo gongo.
Diwani huyo alisema kwa sasa ipo haja kwa serikali kuingilia kati ili kumaliza tatizo hilo linaloonekana kuwaathiri vijana walio wengi na kuwa siku sijazo huenda shule zilizopita eneo lake zikakosa wanafunzi kutokana na vijana kutooana tena.
"Kwenye eneo langu ni ulevi asubuhi Hadi jioni na mbaya zaidi ni gongo Sasa ninachokiona hapa siku sii nyingi hata wanafunzi watakosekana maana hawaoani maana yake hakuna kuzaliana hapa"alisema
Alisema imefikia hatua hata miradi ambayo inatekelezwa kwenye kata yake ambayo inahitaji nguvu kazi ambao ni vijana hulazimika kwenda kwenye kata nyingine za jirani kutokana na vijana waliopo kushindwa kufanya jambo lolote lile.
Katika hatua nyingine diwani huyo alipongeza jitihada zinazofanywa na mkuu wa jeshi la polisi wilaya ya Moshi (OCD)Pilly Misungwi katika kupambana na utengenezaji,uizwaji na unywaji wa gongo na kutaka zoezi hilo kuungwa mkono na kulifanya ni endelevu.
"OCD anatusaidia sana kwenye hizi operesheni zake na naomba viongozi tumuunge mkono ili asikate tamaa hii ni kwa manufaa ya hawa vijana wetu lakini pia kwa maslahi ya taifa kwa siku zijazo"alisema





0 Comments