Na Scolastica Msewa, Mkuranga
Uongozi wa shule za St.Mathew zilizopo wilayani Mkuranga mkoani Pwani imeahidi kumnunulia Mguu wa bandia mzazi wa mtoto wa kike aliyefaulu vizuri masomo yake (jina limehifadhiwa) katika matokeo ya kumaliza elimu ya msingi mwaka huu Dominic Kamwaya ambaye alikatwa mguu baada ya kupata ajali.
Akihutubia katika hafla fupi ya kumshukuru Mungu na kuwapongeza wanafunzi 42 wa darasa la saba waliomaliza mwaka huu Mkurugenzi Mtendaji wa shule hizo Petter Mutembei alisema mguu huo wa bandia unatarajia kugharimu shilingi milioni tatu na nusu fedha hizo zitakuwa ni sadaka ya shukrani kwa Mungu kwa kuwasaidia wanafunzi hao 42 kufaulu vizuri masomo yao ambapo katika wanafunzi hao 40 walipata daraja A masomo yote na wanafunzi wawili walipata Daraja B.
Alisema mbali na msaada huo kwa mzazi huyo pia watamgharimia mwanafunzi yatima Angelina Tewe wa darasa la tatu anayeishi katika mazingira magumu wa shule ya msingi kipalampakani kwa kumpatia vifaa vya shule na mahitaji mbali mbali ya kila siku hadi atakapohitimu masomo yake ikiwa ni sadaka ya kushukuru Mungu kwa wanafunzi hao kufaulu vizuri masomo yao.
Aidha Petter alisema uongozi huo pia unasaidia wanafunzi wengine 40 wa shule za serikali za wilaya hiyo za msingi na sekondari ikiwa ni mchango wao wa huduma katika jamii.
Alisema Petter "Tunaushirikiano mkubwa kati yetu na serikali hasa katika wilaya yetu hii ya Mkuranga ambapo ni kawaida yetu kushirikiana katika mambo mbali mbali ya kijamii katika shule za serikali kwa kutoa vifaa na mahitaji mbalimbali au shule za serikali kutumia vifaa vyetu hapa
hili la kuhudumia watoto hao zaidi ya 40 ni kuisaidia serikali kwakuwa sasa hivi katika shule za serikali ni elimu bure ambapo sasa watoto kutoka familia zote wamepata nafasi ya kusoma, sasa bahati mbaya unakuta baadahi ya watoto wanatoka katika familia zenye uduni au wanashindwa kupata mahitaji ya msingi"
"Kwahiyo sisi kama shule tumejiwekea mpango wakusaidia kwa kuwezesha watoto hao ambao serikali imefanya kwa upande mmoja kwa kuwapatia elimu sasa sisi kama shule tunawawezesha kwa kuwapatia yale mahitaji ya msingi yatakayowawezesha wao kwenda shule" alisema Petter.
Akizungumzia kuhusu kumsaidia Mtoto Angelina Mkurugenzi huyo alisema wataendelea kumsaidia kwa kumpatia mahitaji yake mbali mbali hadi atakapomaliza elimu yake ya msingi.
0 Comments