Nina jirani yangu mmoja, bibi wa miaka kadhaa ambaye Mungu amemjalia kuwa na ng’ombe kati ya 10-15. Bibi huyu yupo mita kama mianne na ukuta wa Chamwino-Ikulu. Katika eneo hili, yeye ni miongoni mwa watu wachache wenye ng’ombe wa asili na siyo wale wa kisasa. Na Adeladius Makwega Dodoma
Kwa mazingira yalivyo inaonekana wazi kuwa bibi huyu mtu mzima, ng’ombe hawa wanamsaidia sana sana kuendesha maisha yake ya kila siku. Kwa kuuza maziwa, mbolea na hata kwa kuuza nyama. Kwa bahata njema bibi huyu amejaliwa pia kuwa na eneo linalokaribia hekari mbili ambazo kila mwaka amekuwa akilima mahindi na kujipatia chakula cha kutosha. Jambo hilo nimelishuhudia kwa miaka mitatu sasa tangu 2019, 2020 na hata mwaka huu 2021.
“Nina mahindi mengi lakini wajukuu ndiyo wanaokula sana na ndiyo wanaomaliza ugali wangu, ningekuwa mwenyewe wala siyo tatizo.Unaona sufuria hili lote wanamaliza” Nilimwambia kuwa sawa, wacha wale ugali wa bibi yao lakini na wewe ukiumwa watakubeba ma kukupeleka hospitali.
“Ahh wapi, hawana chochote wamemaliza shule hapa Chamwino sekondari hawana lolote, wanahangaika tu, nikienda hospitali pesa watatoa wao? Natoa pesa yangu mwenyewe!” Alisema bibi huyu kwa kujinasibu, huku akisonga ugali huo wa mchana ili awahi kuzika. Nikiwa pale sikufahamu ugali huo wa bibi huyu unaliwa na mboga gani. Lakini ulipoiva wajukuu zake walikuja na kuubeba na kuingia nao ndani. Mimi sikupata mualiko, hata ule wa kinafiki.
Nyumba ya bibi huyu ambayo ni ya tembe, kwa mbele ana zizi la ng’ombe, kwa hiyo nilifika kununua mbolea ili niweze kuiwekea katika mimea yangu nyumbani kwangu. “Bei ya kiloba cha shanga mbili ni shilingi 2000/- wewe unataka viloba vingapi?” Nilimwambia bibi huyu kuwa mie nataka viloba viwili lakini kwa bei ya 1500/-kila kimoja.
Aliniambia kuwa nipe pesa hiyo ili nikatoe huko msibani, hapo utamkuta mwanangu Hamisi atakupimia. Nikalipa 3000/- nikaanza kazi ya kuisomba mbolea hiyo.
Kitendo cha kutafuta mbolea hiyo ya samadi ambayo ni ya bei nafuu kinatokana na mimi majuma mawili yaliyotangulia nilienda Dodoma Mjini kutafuta mbolea ya kukuzia, huko niliuziwa kilo moja shlingi 2500/-ni nilinunua kilo 10 na nililipa 25,000/-. Ndiyo kusema kiloba cha kilo 50 kitakuwa ni 125,000/- kwa Dodoma kwa bei ya rejareja. Ukijumuisha na nauli kutoka Dodoma mjini hadi Chamwino Ikulu itakuwa karibu 130,000/-. Kwa ukweli wa Mungu, sifahamu bei ya jumla ya kiloba hicho cha kilo 50 maana kilo hamsini nitazipeleka wapi? Hayo ni mambo yaliyonizidi kimo.
Mara ya yangu mwisho kujua bei ya kiloba cha mbolea cha kilo 50 ilikuwa ni wakati Josephat Hasunga akiwa Waziri wa kilimo, nakumbuka bei yake ilikuwa kati ya 55,000/-60,000/- kwa mikoa ya Songwe na Mbeya, pia kulikuwa na malalamiko kwa wakulima juu ya bei hiyo.
Kumbuka nipo nyumbani kwa bibi huyu wa Kigogo nasomba mbolea yangu. Nikiwa hapa nilibaini kuwa bibi huyu alifika Kijiji cha Ujamaa Chamwino (Chamwino Ikulu) mwaka 1971 akitokea eneo linalofahamika kama Talama, anasema huko kulikuwa na mlima unaitwa Finga ambapo sasa ni sehemu ya eneo la Ikulu ya Chamwino.
“Mwaka huo 1971 Nyerere alipotuhamisha mashambani kwetu, tulipofika hapa kila familia ya baba, mama na watoto tulipewa hekari tatu za kulima. Lakini sasa unahamishwa unapewa karatasi(pesa) ukizitumia zinakwisha unakuwa hauna ardhi tena. Baba! Mimi heka tatu zangu ndiyo hizi unazoziona hapa ninapolima kila mwaka.” Alieleza bibi huyu.
Bibi huyu aliniambia kuwa katika eneo lake hilo tayari ameshapanda mahindi kwa kutumia mbegu za asili na sasa anamwagia eneo hilo mbolea ya samadi kutoka katika zizi lake.
Nikiwa na huyu mdala(bibi) aliniambia kuwa yeye hafahamu alizaliwa lini lakini aliambiwa kuwa alizaliwa wakati wa njaa kubwa(NZARA MBAHA).
Kwa kuwa bibi huyu alitaja njaa kubwa, nikasema kuwa mwakani isije ikawa njaa kubwa na watoto watakaozaliwa wakapewa majina ya Nzara Mbaha bure, lakini nilijifariji baada ya kukumbuka kuwa mvua imeshaanza kunyesha katika maeneo kadhaa ya taifa letu shida ni suala la mbolea kushuka bei bado kitendawili kilichokosa wa kukitegua. Natambua kitendawili hicho kinaweza kuteguliwa bila hata ya kuwapa mji hao wanaopaswa kutegua lakini wanaweza kutegua wakati tushachelewa.
Maana kuna mbolea ya kupandia na mbolea za kukuzia. Kama imeshindikana, basi kila wilaya tupatiwe ujuzi wa kuitengeneza vizuri mbolea ya samadi na kuitumia wakati wa kupandia na kukuzia kwa kutumia kipimo maalumu ili isiyaunguze mazao yetu maana hilo litaondoa kazi ya kupeana vitendawili, kutegua na kupeana miji.
makwadeladius@gmail.com
0717649257
0 Comments