Header Ads Widget

HOJA YA MAKWEGA :MIZENGWE YA SHERIA KWA MWANAHABARI V

 

Na Adeladius Makwega,Mbagala    

Redio Country FM ya Mkoani Iringa ni miongoni mwa baadhi redio za awali kuanzishwa hasa kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini. Redio hii miaka ya 2000 walikuwa na utaratibu wa kujiunga na Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) kila baada ya taarifa ya habari ya saa saba mchana, saa kumi jioni na hata saa nne usiku.



Hili lilikuwa ni jambo jema na redio hii ilikuwa tu miongoni mwa redio za FM ambazo zilikuwa zikifanya hivyo kwani RTD katika maeneo mengi ilikuwa ikisikika usiku tu. Jambo hili lilikuwa likifanyika kwa hisani wala hawakuwa na makubaliano yoyote na RTD na baadaye TBC.


Baada ya minara ya RTD ya Amplitude Modulation (AM) na Short Wave(SW) kuharibika usikivu ulidolola kabisa. Kumbuka kipindi hicho hicho na harakati za kuanzishwa kwa FM redio ukashika kasi.


Nafasi iliyokuwepo ya RTD kusikika nchi nzima ikapotea na FM redio zikaziba pengo hilo. Ndiyo maana nasema kwa Iringa hawa Country FM wakaziba nafasi. Iringa wakati huo TBC walikuwa na mwakilishi wao Malima Ndelema na baadaye Adolf Mbata. Walikuwepo pale lakini taarifa za Iringa hazikusikika Iringa kwa kuwa ilikuwa vigumu redio kukamata matangazo hayo.


Baadaye Redio la kimatiafa ambazo ziliendelea kurusha matangaza yao kwa AM, SW na salalite kwa saa ambazo taarifa zao zilikuwa hewani walibaini fursa ya kuzitumia FM Redio kwa mataifa kama Kongo, Malawi, Burundi, Rwanda, Kenya, Uganda na hata Tanzania.


Kwa kuwatumia wawakilishiwa wa redio hizo za kimataifa waliopo katika mataifa haya wakajenga ujirani na FM redio maana hawa wawakilishi walikuwa wakifanya kazi pia na redio za FM.


“Vipi huko ni redio gani ya FM inasikilizwa ili wajiunge na matangazo yetu?” Mawasiliano yalifanya na ushirikiano ukaanza.


Makubaliano ya pande zote mbili yalifanyika na kila upande kuona matunda ya kushirikiana na jambo hili mie binafsi nilivyoliona ni jambo jema.Ukilitazama kwa kina jambo hili utabaini kuwa hata vyombo vya kimataifa walikuwa wakifanya utafiti juu ya chombo cha kushirikiana nacho katika kila eneo. Ndiyo maana baadhi ya redio hadi leo japokuwa zinasikika maeneo makubwa za binafsi hazikupata nafasi ya kuwa redio washirika.


Ngoja nikutajie manufaa machache sana ya kushirikiana na vyombo vya kimataifa. La kwanza kabisa, kupata baadhi ya vifaa vya kisasa vya kurushia matangazo. Jambo hili limesaidia kuyafanya matangazo ya redio za FM kuwa bora sana.


Pili, Redio hizo washirika zimeweza kupata hata ushauri wa kiufundi wa namna bora ya mitambo ili kuweza kufanya matangazo ya FM yasikike lakini pia redio za kimataifa matangazo yao yasikike vizuri.


Tatu, wanahabari wameweza kupata nafasi ya kwenda kujifunza katika vyombo vya kimataifa wakibadilishana uwezo na ujuzi wa utangazaji. Kwa mfano  akina Grace Kabogo kutoka redio Tumaini ya Dar es Salaam, Charles Mwebeya akitokea redio Kwizela na baadaye alijiunga na TBC, Fatuma Matulanga akitokea TBC Taifa na Salma Said akitokea Zanzibar waliweza kwenda kujifunza zaidi taaluma hii huko DW Kiswahili kwa vipindi tofauti.


Nne, kumekuwa na ushauri hata ya uboreshaji wa kurasa za tovuti za redio washirika. Maana zamani redio ilikuwa ni kurusha matangazo hewani wamemaliza lakini sasa kila redio la kimataifa zina kurasa bora za tovuti ambazo unaweza kusoma, kusikiliza na hata kutazama kinachofanyika zikiwano ripoti za maandishi, ripoti za sauti na ripoti za video pamoja na picha mnato.Ukiweka kando ripoti hizo hata maktaba za vipindi, taarifa za zamani za redio za kimataifa zinapatikana katika tovuti hizo kwa nia ya kujifunza.


Tano vyombo vya habari vya Tanzania hasa redio zimekuwa na ujirani mkubwa wa kimawasiliano na vyombo vya kimataifa kuliko hata vyombo vya nyumbani vya umma.


Mathalani ukitembelea Newsroom (vyumba vya habari) za magazeti na FM redio nyingi kurasa karibu zote za tovuti za vyombo vya kimataifa zinatembelewa sana na habari zao kunakiliwa kuliko tovuti za vyombo vya habari vya serikali.


Ushirikiano mkubwa baina ya vyombo vya habari vya kimataifa na washirika wao mathalani mkuu wa idhaa ya Kiswahili DW anaweza kumfahamu Maneja ya Country FM ya Iringa kuliko hata Mkurugenzi wa Habari-Maelezo au TSN anavyomfahamu mtu huyo.


Kwa Tanzania yetu redio za kimataifa zinazofanya vizuri DW Kiswahili na BBC KISWAHILI lakini jambo la kushangaza hakuna ujirani wa karibu kama ule wa FM Redio na vyombo hivyo vya kimataifa. Natambua upo shirikiano na baadhi ya vyombo vya kimataifa na taasisi hizo za umma lakini vyombo hivyo havina wasikilizaji wa kutosha kama DW Kiswahili na BBC Kiswahili.


Binafsi ninaona ujirani na urafiki wa taasisi za kihabari za umma na binafsi unapaswa kuwa mkubwa zaidi na kujifunza namna vyombo vya kimataifa zilivyoweza. Swali la kujiuliza TBC, TSN na hata Habari Maelezo wanashindwa kufanya ushirikiano wa kimafunzo na vyombo binafsi vya habari vya Tanzania? 


Waandishi wanaojifunza kazi wanaweza kufanya mafunzo kwa miezi hadi 6 wakiwapo katika majengo ya TBC, TSN na Habari Maelezo huku wakilipwa posho ya kuishi angalau kila mwaka waandishi 100 hawa wakimaliza mafunzo wanakuwa mawakala wazuri wa vyombo vya serikali, hata wanakuwa ni miongoni mwa watumishi wa akiba pale panapotokea upungufu wa watumishi kwenye taasisi hizo za serikali. Hauwezi kupata wakala mzuri wakati haukumuandaa katika kumtengeneza.


Tunaposimama na kuvifungia vyombo hivyo haina msaada wowote bali ni kujenga chuki ambayo haina maana.


Inawezekana vyombo vya habari vikawa vinafanya makosa na makosa ya vyombo huwa ni makosa ya wanahabari unapofungia chombo, mwenye mali ambaye ametoa pesa yake kuwekeza atatii agizo lakini tambua kuwa kufungia chombo hicho tayari umeshapoteza kazi ya mhariri na wasimamizi wote wa chombo hiko.Lakini pia sheria na kanuni za kufungia fungia vyombo vya habari zinaweka mashaka kwa wawekezaji wapya katika tasnia hii.


Kuna makosa ambayo yanahitaji mazungumzo baina ya pande mbili mnaweza hata mkafanya mazungumzo yasiwe kwa siri yawe wazi wazi na jamii ione kama wamekosea wapi katika hilo na mwisho mnaafikiana. Kwa kuwa serikali inavihitaji vyombo vyote viwe vya umma na binafsi ili kuweza kuyafikia malengo yake.


Chombo cha kimataifa kikikosea basi hata chombo kinachorusha matangazo hayo kinawajibika kwa kosa hilo, jambo hilo halina mantiki ni sawa na kumpa adhabu mtoto kwa kwa kosa la baba/mama.


Kwa mfano Asah Andrea Mwambene ambaye aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji wa Serikali wakati huo aliondoka katika nafasi hiyo na huku akiacha mchakato wa muswada wa Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari.


Tunaoshiriki kuandaa sheria hizo tunapaswa kuvaa viatu kuwa na siye tunaoshiriki kuziandaa ni watumiaji tarajali wa sheria na kanuni hizo. Kama tunaweza na siye tuanzishe redio, blog, televisheni na magazeti yetu binafsi na tutakuwa mashuhuda wazuri wa jambo hili. 


Kama kutakuwa na ushirikiano mwema na kuaminiana baina ya vyombo vya umma vinavyosimamia sheria za habari, vyombo vya umma na binafsi nina imani hata serikali itatumia fedha kidogo sana kwa kazi zake kwa umma mathalani kutoa elimu ya ufugaji, elimu ya kilimo bora, elimu za uvuvi na hata masuala ya afya kuifikia jamii ya Watanzania popote walipo.


Kwa leo naweka kalamu yangu chini nikikutakia siku njema.


makwadeladius@gmail.com

0717649257.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI