SHIRIKA la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa( FAO) limetoa mafunzo kwa waandishi wa habari kwa kutoa elimu ya uelewa juu ya usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya madawa . mwandishi wa matukio daima Hamida Ramadhani anaripoti kutokea Dodoma
Akiongea mara baada ya kumalizika kwa mafunzo hayo Jijini hapa Dkt Elibariki Mwakabeje Kutoka shirika la kilimo chakula la umoja wa mataifa FAO na Mratibu wa Kitaifa wa masuala ya kuzuia usugu wa vimelea vya magonjwa alisema mafunzo hayo ni muhimu kwa wanahabari kwani duniani kote tarehe 18 hadi 24 ni wiki ya kutoa elimu na uelewa katika jamii juu ya usugu wa vimelea vya Magonjwa dhidi ya dawa kwa ujumla wake.
"Sisi Shirika FAO tumeamua tukae na waandishi wa habari na tuzungumze masuala haya ili tunapoanza hiyo ya usugu wa vimelea vya Magonjwa dhidi ya dawa basi wandishi wa habari waweze kuelewa usugu wa vimelea vya Magonjwa dhidi ya dawa ni nini," Alisema.
Aidha alisema katika Wiki hiyo kutakuwa na kazi mbalimbali ambapo kutakuwa na uelimishaji wa umma kupitia magari yanayotembea katika mitaa juu ya usugu wa vimelea vya Magonjwa dhidi ya dawa ambapo wananchi watapata elimu kupitia magari hayo yanayotembea karibu maeneo yote.
Hata hivyo alisema Waziri wa Afya Dkt Dorothy Gwajima atatoa tamko juu ya ukubwa wa tatizo hili na nini jamii iweze kufanya katika kuunganisha nguvu na kumaliza tatizo hilo.
"Katika wiki hiyo pia kutakuwa na wataalamu kutoka sekta mbalimbali ambao wataenda kwenye vyombo vya habari mbalimbali kwa ajili ya kuelimisha jamii kwani tatizo la usugu wa vimelea vya Magonjwa dhidi ya dawa ni suala tambuka ambapo sekta ya afya ,Sekta ya Mifugo, sekta ya kilimo ,pamoja na sekta ya Mazingira ni lazima zifanye kazi kwa pamoja,"alisema.
Pia amesema wataalamu kutoka kwenye sekta hizo watakuwa wanakwenda kwenye vyombo vya habari na kueleza nini kifanyike kukabilina na tatizo hilo na Maadhimisho hayo yatafanyika nchi nzima ambapo kazi za Fao walizozifadhili zitafanyika mkoa wa Dodoma,Morogoro,Lindi,Mtwara pamoja na Zanzibar .
Naye Mkurugenzi Msaidizi Ofisi ya Waziri Mkuu idara ya Menejimenti ya Maafa, Charles Msangi alisema usugu wa vimelea vya magonjwa hutokea pale ambapo virusi vya vimelea hivyo kushindwa kutibika hususani kwa dawa maalumu na kusababisha kuongeza kasi kwa magonjwa na makali ya ugonjwa na kupelekea vifo vingi kwa watu.
Alisisitiza kuwa usugu huo wa vimelea vya magonjwa unahitaji wataalamu katika sekta mbalimbali kuweza kufanya kazi kwa pamoja ili kushughulikia kwa kasi suala hilo kwani kumekuwa na kasumba duniani juu ya suala hilo ambalo husababisha vifo katika mataifa mbalimbali duniani.
“Siyo Tanzania tu ambao tunashughulika na Kupambana na suala la usugu wa vimelea bali duniani kwa ujumla lakini pia tunaona juhudi za Taasisi mbalimbali katika kuweka mchango wao kuhakikisha wanaendelea Kupambana na usugu huo pia FAO nao hawako nyuma katika kuendelea kutoa semina za elimu ya mapambano ya usugu wa vimelea vya magonjwa," Alisema Msangi.
Naye Summa Jairo Mfamasia kutoka Wizara ya Afya kitengo cha huduma za dawa alitoa ushauri katika kuelekea wiki ya usugu wa vimelea vya Magonjwa dhidi ya dawa wananchi waache kununua dawa kiholela .
Pia aliwakumbusha wale wanahudumia maduka ya madawa wahakikishe hawatoi dawa kwa mgonjwa mpaka awe na cheti kutoka kwa Daktari.
0 Comments