Header Ads Widget

BARAZA LA MADIWANI LAWEKA MIKAKATI YA KUONGEZA MAPATO NA WANAFUNZI WA KIKE KUTOKOSA MASOMO SHULENI


Baraza la madiwani la halmashauri ya Meru limeomba uwepo wa chumba cha kubadilishia taulo za kike katika shule za sekondari ili kusaidia wanafunzi wa kike kutokosa masomo pindi wanapokuwa katika kipindi cha  hedhi.....Na Teddy Kilanga Arusha


Akizungumza katika baraza hilo jana,Mwenyekiti wa halmashauri hiyo,Jeremia Kishili alisema uwepo wa chumba hicho  katika shule zote za kata kuanzia ngazi ya sekondari kutasaidia wanafunzi wa kike kutokosa masomo darasani  pamoja na kupunguza utolo wa baadhi ya wanafunzi kwa kusingizia kuwa wapo katika hali hiyo.


"Inabidi na sisi tuangalie kwenye shule zetu za kata kujenga chumba kimoja kwa ajili ya binti zetu sababu nao wanaposikia kuwa wenzao wapo katika mazingira mazuri lakini huku kwetu hamna tujitahidi na huku kwetu kuwepo na jengo  la kuwasaidia kubadilishia taulo za kike,"alisema Mwenyekiti.


Aidha alihimiza suala la ukaguzi za mapema katika miradi ya maendeleo ya halmashauri hiyo ili kusaidia kutatua changamoto  hasa tatizo la kitaaluma katika zoezi la ukamilishaji.



Kishili aliongeza kuwa ni vyema madiwani na wataalamu wa halmashauri hiyo wakashirikiana  katika ukusanyaji wa mapato kwa kupeana mikakati mbalimbali ili kuongeza mapato yatakayosaidia kukamilisha miradi ya maendeleo kama vile vituo vya afya .




"Ukiangalia kuna baadhi ya kata hazina hata zahanati moja ni vyema zikaangaliwa kwa jicho la tatu,"alisema Mwenyeliti Kishili.


Naye Mkurugenzi wa halmasahuri hiyo,Mwalimu Zainabu Makwinya aliwaomba madiwani hao kushirikiana katika kuweza kufanikisha maendeleo mbalimbali katika kuzingatia ukusanyaji wa mapato


"Sisi kama halmashauri tumejipanga na wakuu wangu wa idara na tulishaendesha zoezi la ukusanyaji  taarifa  kutoka kwa wafanyabiashara mbalimbali kuanzia ngazi ya vijiji ,vitongoji  hadi kata,"alisema Mkurugenzi Makwinya.


Makwinya alisema katika kudhibiti upotevu wa mapato katika halmashauri wameanza oparesheni za usiku baada ya kubaini mazao mengi kutoroshwa nyakati za usiku ambapo wiki kadhaa zilizopita walikamata lori lenye  kreti  80 za nyanya pamoja na magari yenye kuni ambapo walifanikiwa kuwatoza faini.


Mwalimu Makwinya alisema  katika soko la Tengeru na Msolongo wamekuwa wakijitahidi  katika kuhakikisha mapato hayapotei kwani wamekuwa wakiweka kambi kuanzia saa kumi jioni hadi 12 alfajiri kutokana na kubainika kuwa kuna mazao ambayo yanaingizwa kwenye masoko hayo mapema hivyo wakichelewa hukuta wameshauza.


Mkurugenzi huyo alisema ni vyema wakaendelea kushirikiana pamoja na madiwani ili kuondoa changamoto ndogondogo zinazowakuta za ukosefu wa fedha.



Hata hivyo Mwalimu Makwinya alisema hadi sasa fedha za uviko zimeshaingia takribani sh.bilioni 1.4 pia waliongezewa sh.milioni 17 ambazo ziliingia wiki iliyopita na fedha za tozo ni sh.milioni 300 ambapo utekelezaji wake unaendelea ukiwemo shule ya sekondari Patandi ya elimu maalumu ambapo walipeleka sh.milioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa maabara na nyumba za watumishi.


Kwa upande wake Afisa elimu vifaa na takwimu,Mwalimu Angela Urassa alisema mikakati ya halmashauri katika ujenzi wa madarasa kupitia fedha za uviko ni pamoja na  vyumba hivyo  kwa ajili ya wanafunzi wa kike kubadilishia taulo zao za kike kipindi wanapokuwa katika kipindi chao cha hedhi.


"Pia tumeshaongea na wadau wengine kujitokeza kusaidia wanafunzi wa kike taulo la kike ili kuepusha utolo shuleni kwa lengo la kuongeza ufaulu katika masomo yao ,"alisema Afisa elimu huyo.


Nao baadhi ya madiwani hao walisema kutokana wao kuwa wawakilishi wa wananchi wanahaidi watashirikiana na Mkurugenzi katika suala la ukusanyaji wa mapato ili kuweza kusaidia kukamilisha  miradi ya maendeleo na fedha hizo husaidia pia kutatua changamoto za wananchi kwa wakati.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI