MKURUGENZI wa Kampuni ya LOHE Tanzania Limited ,Longinus Komba amewataka wahitimu wa kidato cha Nne wa shule ya Sekondari ya Ngwilizi iliyopo kata ya Kitanda Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma ,kwenda kutumia vema Elimu waliyoipa shuleni hapo ili kufanikisha kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo ya ajira. mwandishi wa matukio daima Amon Mtega anaripoti kutoka Mbinga.
Wito huo ametolewa na mkurugenzi wa Kampuni hiyo yenye makao yake makuu Wilaya ya Mbinga wakati wa mahafali ya kumi na Nne (14)ya shule hiyo alipoalikwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe hiyo iliyohudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo Viongozi wa vyama vya siasa na Serikali.
Komba amesema kuwa kumekuwepo kwa baadhi ya wahitimu kushindwa kutumia Elimu walizozipata ipasavyo jambo ambalo hupelekea kuona maisha magumu na hatimaye hujiingiza kwenye vitendo viovu na mwisho wa siku maisha yao huharibika.
Mkurugenzi wa Kampuni hiyo inayojishughulisha na mambo mbalimbali ikiwemo uchakataji wa unga wa sembe ya mahindi licha ya kuwaasa wahitimu hao lakini kampuni yake imetoa msaada wa Komputa sita(06) ambazo zimeunganishwa na mtandao (Internet) ili kuwafanya wanafunzi waweze kuwa na uelewa zaidi katika ulimwengu wa Sayansi na Teknolojia.
Mgeni rasmi huyo ambaye naye alisoma shule hiyo licha ya kutoa msaada wa Komputa hizo lakini ameahidi kuongeza miche ya miparachichi ili iweze kuongeza kasi ya upandaji wa matunda hayo kwenye eneo la shule na kisha kuyafanya mazingira yaendelee kuhifadhiwa.
Hata hivyo kampuni yake pia imeahidi kutoa msaada wa runinga(TV) ya kisasa kwa matumizi ya Walimu na shule ili kuwaondolea adha ya kwenda umbali mrefu kwenda kupata huduma ya upataji wa habari mbalimbali za kitaifa na kimataifa.
Kwa upande wake mkuu wa shule hiyo Giliadi Mabena awali akisoma taarifa ya shule hiyo amesema kuwa shule hiyo licha ya kuwa na ufaulu mzuri lakini inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa thamani za ofisini katika ofisi ya mwalimu mkuu na ofisi ya mwalimu.
Mabena licha ya shule hiyo kukabiliwa na changamoto hizo lakini ameipongeza kampuni ya LOHE Tanzania Limited kupitia mkurugenzi wake Longinus Komba kwa msaada mkubwa anaoutoa shuleni hapo ambapo hadi sasa ameshatoa msaada wa zaidi ya kilo 700 za unga wa sembe kwaajili ya chakula cha wanafunzi shuleni hapo jambo ambalo hupelekea kupunguza utoro kwa wanafunzi hao.
Naye diwani wa kata ya Kitanda Aureus Ngonyani wakati wa mahafali hayo ametumia nafasi hiyo kuwataka Wananchi waendelee kuchukua tahadhari juu ya ugonjwa wa Corona pamoja na kujiandaa kuhesabiwa kwenye Sensa itakayofanyika mwakani 2022.





0 Comments