Header Ads Widget

VIONGOZI WA AMCOS WANAOFANYA UBADHIRIFU WA FEDHA ZA WAKULIMA KUFIKISHWA MAHAKAMANI

Na Bahati Sonda,MDTV  Simiyu.

Serikali Mkoani Simiyu imesema kuwa itawachukulia hatua kali za kisheria kwa kuwafikisha mahakamani na kuwashtaki viongozi wote wa vyama msingi vya ushirika(Amcos) watakaobainika kufanya ubadhirifu wa fedha za wakulima wa pamba.


Aidha imesema kuwa haitaishia kuwavua uongozi na kuwataka kurudisha fedha tu badala yake kufunguliwa kesi za wizi lengo ni kukomesha tatizo hilo ambalo limezoeleka na limekuwa likifanywa na viongozi wengi wa Amcos mara nyingi bila hofu yeyote.


Hayo yamebainishwa jana na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu David Kafulila wakati akizungumza na watendaji wa vijiji, kata na tarafa wa wilaya ya Maswa kwenye kikao cha mpango mkakati wa kuongeza uzalishaji wa zao la pamba msimu wa mwaka 2021/2022 na kusema kuwa tabia hiyo imekuwa sugu kutokana kutokuchukuliwa hatua kali za kisheria hali inayopelekea ubadhirifu wa fedha za wakulima mara kwa mara.



Kafulila amesema kuwa mara nyingi sana viongozi wanaofanya ubadhirifu wamezoea kuona wakiambiwa kurudisha fedha na kuvuliwa madaraka na kesi kuishia hapo jambo linalowafanya kuona wizi ni kitu cha kawaida na kwamba ili kukomesha tatizo hilo lazima sheria zitumike .


"Nafasi ya kuendelea kufanya mlivyozoea kwenye Amcos mnaiba kisha unatokomea kusikojulikana ukikamatwa unarudisha na unaendelea nafasi hiyo imefutika, lazima niwaambie ukweli napenda sana ushirika kwa sababu unaunganisha watu wasio na mitaji kupata mitaji lakini ninachukia sana wizi" Alieleza Kafulila 


"Amcos ikikutwa imefanya ubadhirifu ni mambo matatizo(3) wanarudisha pesa ndani ya wiki 2 yaan siku 14 na baada ya kurudisha washitakiwe na uongozi waupoteze , utamaduni wa kufikiri kwamba kwenye ushirika unachukua hela ukikamatwa unarudisha na biashara inaishia hapo ,"kwa hiyo zile ambazo hukamatwi unakuwa unakula kwa sababu huna hofu hivyo Takukuru mtu anayekamatwa amefanya wizi ni mambo yote matatu " Alisema Kafulila


Kafulila ameongeza kuwa wakianza kufikishwa kwenye vyombo vya kisheria na kuhukumiwa itasaidia kuondoa tatizo hilo ambalo litawafanya wawe na hofu na kuhisi kwamba mali ya ushirika siyo rahisi kuiba huku akiagiza kupatiwa taarifa ya ubadhirifu wote uliofanyika Mkoani humo katika msimu wa mwaka 2020/2021.


"Wale ambao wanadhan watapiga katika msimu huu ambao tumepanga kuzalisha kwa wingi wote mtaishia jela, sina huruma na kiongozi yeyote wa Amcos anayefanya ubadhirifu na taarifa ya michezo yote iliyofanyika katika msimu uliopita Mkoa mzima nataka niipate sina tatizo la kufunga Amcos zote kwa sababu wakulima wanaweza kuendelea bila ya ninyi kuwepo kwa sababu mnakula hela zao tu hivyo kaeni sawa sawa" Alilisitiza Kafulila 


Katika hatua nyingine amewaagiza watendaji wa vijiji na kata kwenda kufanya operesheni kwa wakulima ya kuchukua hatua kwa za kisheria wakulima wa pamba ambao bado wameshindwa kutoa masalia ya pamba ya msimu uliopita na operesheni ya kusambaza samadi .


Hata hivyo Mkuu wa Wilaya ya Maswa Aswege Kaminyonge amemhakikishia Mkuu wa Mkoa kusimamia maelekezo yote yaliyotolewa hususan mpango mkakati ili kufanikisha adhma ya serikali kuongeza tija na uzalishaji wa zao la pamba hali itakayosaidia kuinua kipato cha wakulima.


      Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI