Header Ads Widget

VIONGOZI 18 WA AMCOS WAVULIWA NAFASI ZAO KWA TUHUMA ZA UFUJAJI WA FEDHA KIASI CHA SHILINGI MILIONI 68.

Viongozi 18 wa vyama vya msingi  vya ushirika (Amcos) 9 katika wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu wamevuliwa nafasi zao kufuatia tuhuma za ufujaji wa pesa za wakulima kiasi cha shilingi milioni 68 katika msimu wa pamba uliopita wa mwaka 2020/2021. mwandishi wa matukio daima Bahati Sonda anaripoti kutokea Simiyu.

Kafulila amesema kuwa mara nyingi sana changamoto hizo zinajitokeza kutokana na baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu wanaotumia fursa hiyo kwa manufaa yao na kusisitiza kuwa ndani ya siku 14 fedha hizo ziwe zimerejeshwa .

Maamuzi hayo yametolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu David Kafulila kwenye kikao cha mpango mkakati wa kuongeza uzalishaji wa zao hilo na kusema kuwa hatokuwa na aibu wala hatamhurumia kiongozi yeyote ambaye anafuja fedha za umma.

Aidha amewataka afisa ushirika wilayani humo kuhakikisha wanafanya utaratibu wa kupata viongozi wengine huku akiongeza  kuwa katika msimu wa mwaka 2020/2021 changamoto kwenye Amcos hazikuwa nyingi ikilinganishwa na 2019/2020 licha ya kukiri kuwepo.

"Kwenye msimu uliopita sarakasi hazikuwa nyingi ikilinganishwa na ule uliotangulia lakini sarakasi zipo hivyo wito wangu kwenu viongozi wa Amcos msimame sawa sawa kwenye kutekeleza majukumu yenu ,ushirika ni sera ya CCM na ni mkakati wa serikali na kwamba changamoto kubwa iliyojitokeza ni baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu kutumia fursa hiyo kujinufaisha"Amesema Kafulila

Katika hatua nyingine Kafulila ameongeza kuwa wadau wa pamba hususani Kampuni zinazojishughulisha na ununuzi na usambazaji wa mbegu ambazo haitashirikiana na Mkoa huo kwenye maandalizi ya msimu mpya wa kilimo haitaruhusiwa kununua pamba Mkoani Simiyu.

"Wadau wa pamba ambao ni wanunuzi na wasambaji wa mbegu wito wangu kwenu kampuni ambayo haitashirikiana na sisi kwenye maandalizi ya msimu huu katika majukumu mbalimbali ukweli ni kwamba haitopata nafasi ya kununua pamba katika Mkoa wa Simiyu atakaye subiri kudandia mwisho hayupo, hata kama angekuwa nani na kumbukumbu tutakuwa nazo " Alilisitiza Kafulila

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Maswa Aswege Kaminyonge amesema kuwa mahitaji ya mbegu ni tani elfu tatu(3,000) ambapo mpaka sasa wamepokea tani mia saba (700) na kubainisha kuwa  kasi ya ununuzi wa mbegu kwa wakulima ni ndogo.

Hata hivyo Meneja shughuli wa Kampuni ya Alliance Ginery limited Ernest Edward iliyopo katika wilaya ya Bariadi ambao pia wanasambaza mbegu Mkoani wameilalamikia bodi ya pamba kutokana na ucheleweshaji wa mbegu hali inayopelekea magari kukaa muda mrefu bila kupakia jambo linalowatia hofu juu ya namna ambavyo watavifikia vijiji visivyoweza kufikika kwa urahisi pindi mvua zitakapoanza kunyesha na kuuomba uongozi wa Mkoa kushughulikia suala hilo.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI