Tatizo la uchakavu wa miundombinu wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro ni moja ya changamoto inayosabaisha uhaba wa maji safi na salama katika baadhi ya maeneo. mwandishi wa matukio daima Rehema Abraham anaripoti kutokea Kilimanjaro
Hayo yalisemwa na Mkuu wa wilaya ya Mwanga Abdallah Mwaipaya wakati akizungumza katika mkutano wa kwanza wa uzinduzi wa jumuiya ya watumia maji mto gonna , uliofanyika katika ukumbi wa chuo cha mifugo Kilacha iliyopo Himo mkoani Kilimanjaro .
Mwaipaya alisema kutokana na changamoto hiyo Serikali inaendelea na utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji Same Mwanga korogwe ambao utakuwa mkombozi wa upatikanaji wa maji safi na salama wilayani humo.
Alisema moja ya mikakati inayofanywa wilayani humo ni kuhakikisha miradi 12 ya maji iliyopo katika wilaya hiyo inaendelea vizuri ili kufikisha maji maeneo ya vijijini.
Sambamba na hilo alisema katika kuhakikisha vyanzo vya maji vinalindwa hakuna mtu yoyote ataruhusiwa kufanya shughuli za kibinadamu katika mabonde ili kusaidia jitihada za vyanzo kwa kutunza mazingira.
Akizungumza katika uzinduzi wa jumuiya ya 23 ya watumia maji mji mdogo wa Himo ,mkurugenzi wa bodi ya maji bonde la pangani Segule Segule alisema njia endelevu ni kushirikisha ngazi ya jamii katika kusimamia,kutunza na kulinda vyanzo vya maji.
Segule alisema moja ya mikakati iliyopo katika bonde ni kudhibiti uharibifu dhidi ya vyanzo vya maji unaofanywa kwenye jamii lengo likiwa ni kuhifadhi vyanzo hivyo kwa manufaa ya vizazi vijavyo.
Naye Leonard Ngowi mdau wa mazingira katika mji mdogo wa Himo alisema changamoto inayorudisha nyuma udhibiti vyanzo vya maji ni kutokuzingatia utaratibu wa mita 60 zilizowekwa na Serikali uliokua na lengo la kuzuia wananchi kufanya shughuli za kibinadamu kando ya vyanzo vya maji.
Alisema kwa sasa wananchi walio wengi wamesogea katika vyanzo hivyo hadi mita 10 jambo ambalo ni hatarishi kwa vyanzo hivyo, huku akisema kwa jumuiya iliyoundwa na bodi ya maji bonde la Pangani itasaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa adha hiyo.
0 Comments