Na Doreen Aloyce, Dodoma.
KATIKA kuendelea kupambana na ugonjwa wa Uviko 19 Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Antony Mtaka amezitaka kamati za afya za wilaya zote kuweka mikakati ya kuhakikisha maeneo yote yanafikiwa kwaajili ya kuwapatia wananchi elimu juu ya umuhimu wa uchanjaji.
Kadhalika amewataka wahakikishe kwamba huduma hizo zinawafikia wananchi katika maeneo yote yenye mikusanyiko kama sehemu za ibada misikitini,makanisani, kwenye makongamano sambamba na sehemu za vituo vya mabasi.
Akizungumza jijini hapa katika kikao cha tathmini ya uharakishaji na utekelezaji wa Mpango wa uchanjaji chanjo ya Uviko_19 Mtaka amesema kama ofisi ya Mkoa tayari wameshapokea shehena mpya ya chanjo ya Sinopharm dozi elf 50,390.
"Sasa hizi kamati ziende huko sehemu ambapo watu wapo mkatoe elimu juu ya chanjo hii mpya baada ya ile nyingine kuisha mkawape elimu na wataalamu pia mkatoe elimu juu ya chanjo hii" amesema Mtaka.
Kwa upande wake Mratibu wa Chanjo mkoa wa Dodoma Francis Bujiku amesema Mkoa wa Dodoma awali ulipokea jumla ya dozi 50,000 za chanjo ya Uviko 19 ya JJ na mnamo tarehe 3 Agosti 2021 ulizindua kampeni ya uchanjaji na hadi kufikia tarehe 5 oktoba Mkoa ulikua umemaliza chanjo zote zilizopangwa kwa asilimia 100.
"Baada ya kuona tumemaliza zile zilizopangwa tukaomba chanjo za ziada 6515 kutoka Mikoa ya Geita chanjo 5000,Iringa1515 na mpaka kufikia Oktoba 13 jumla ya wananchi 52,599 walichanja chanjo ya Uviko 19" amesema Bujiku
Amesema kufuatia uanzishwaji wa chanjo ya Uviko 19 katika Mkoa wa Dodoma tarehe 3 Agosti 2021wananchi wamepata elimu na vituo viliongezeka 28 vya kutoa chanjo na badae kuongezeka hadi kufikia 381, ambapo walengwa 52,629 wamepatiwa chanjo hadi kufikia tarehe 14 oktoba 2021sawa na asilimia 93 ya lengo la kuchanja walengwa 56,515.
Akizungumzia kuhusu uanzishwaji wa chanjo mpya Bujiku amesema Serikali imejipanga kuwa na utaratibu wa utekelezaji wa uanzishwaji wa chanjo hiyo mpya ya Sinopharm ambao utaleta matokeo makubwa.
Amesema vituo 381 vitaendelea kutumika kutoa chanjo hiyo pamoja na huduma ya mkoba katika maeneo yote ambapo chanjo hiyo itatolewa Mara 2 dozi hiyo ya pili itatolewa siku 28 baada ya chanjo ya kwanza huku akiwasisitiza wananchi kutopuuzia kurudi kumalizia dozi hiyo ya pili.
0 Comments