Na Mwandishi Wetu, Pemba
Ngome ya Vijana ya chama cha ACT Wazalendo Zanzibar imeandaa mashindano ya mchezo wa soka ikiwa ni kuenzi Siku ya kuzaliwa ya nguli wa siasa Zanzibar, Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad aliyezaliwa Oktoba 22 mwaka 1943.
Akizungumzia mashindano hayo, Makamu Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ACT Wazalendo, Hadija Anuar Mohamed leo Oktoba 20,2021 amesema mashindano hayo maalum ya soka yameandaliwa na ngome za vijana za majimbo na mikoa yote ya Pemba ili kuenzi Siku ya kuzaliwa ya kiongozi huyo.
"Kama tujuavyo kuwa aliyekuwa Kiongozi wetu Mpendwa Almaruhum Maalim Seif Sharif Hamad alizaliwa tarehe 22 October.
Kiongozi wetu huyo licha ya maisha yake ya Kisiasa pia alikuwa ni mshabiki mkubwa wa michezo na hasa mpira wa miguu.
"Ngome ya Vijana Majimbo na Mikoa ya Pemba katika kumuenzi Kiongozi wetu huyo imeandaa Ligi maalum itakayoshindania Kombe la Maalim Seif (Maalim Seif CUP) katika Fainali zitakazofanyika Oktoba 22, 2021 Chake Chake Pemba"amesema Hadija na kuongeza kuwa
Makamo Mwenyekiti huyo wa Ngome ya Vijana kwa Upande wa Zanzibar amebainisha kuwa ligi hiyo inaratibiwa na kudhaminiwa na Ofisi yake imeanza kwa hatua za awali kwa kuzishirikisha timu za vijana wa Majimbo 18 yote ya Pemba ikifuatiwa na hatua ya nusu fainali kwa kuzishirikisha timu nne za Mikoa ya Kichama na hatua ya fainali itazishirikisha timu mbili, moja kutoka kila Mkoa wa Kiserikali Kusini na Kaskazini Pemba.
Amesema katika fainali hiyo mbali na zawadi ya Kombe la Maalim Seif kwa mshindi, zawadi nyengine mbalimbali zitatolewa kwa mshindi wa 1, 2, 3 ambapo pia timu zote zilizoshiriki katika hatua ya awali nazo zitazawadiwa
"Katika kumuenzi Maalim Seif kwa kuwaunganisha, kuwashajiisha na kuwaunga mkono Vijana wa ACT kutoka katika Majimbo na Mikoa, tunatoa wito kwa Viongozi wa Chama ngazi mbali mbali, Viongozi wa Ngome ya Vijana wanachama wa ngazi mbalimbali pamoja na wadau wote wa michezo kujitokeza kwa wingi siku ya tarehe 22/10/2021 saa 9:00 jioni Chake Chake kuja kushuhudia mashindano hayo muhimu na ya aina yake.
0 Comments