Ni swali ambalo limeanza kutua katika vichwa vya Watanzania kutaka kujua ni nani ataweza kurithi nafasi ya Uenyekiti wa chama cha ACT Wazalendo ambayo ipo wazi kutokana na aliyekuwa ameshikilia nafasi hiyo marehemu Maalim Seif Sharif Hamad kufariki dunia Februari 17 mwaka huu.
Akizungumza na vyombo vya habari leo Oktoba 17,2021, Dar es Salaam Naibu Katibu wa Habari,Uenezi na Mahusiano ya Umma wa chama hicho, Janeth Rite amesema, Halmashauri Kuu itakayoketi Oktoba 31,2021 itatangaza mchakato wa uchaguzi wa kujaza nafasi ya Mwenyekiti Taifa.
Amesema mbali na hilo, Halmashauri Kuu ya Chama cha Taifa cha ACT Wazalendo itaketi kwenye kikao chake cha kawaida katika Ukumbi wa Hoteli ya Landmark Dar es salaam na kitatanguliwa na Kikao cha Kamati Kuu itakayoketi tarehe 30 Oktoba 2021 katika Ukumbi huohuo.
"Halmashauri Kuu ya Chama Taifa ni kikao cha pili kwa ukubwa baada ya Mkutano Mkuu Taifa. Halmashauri Kuu ya Chama inajumuisha wajumbe wote wa Kamati Kuu, Wajumbe wa Halmashauri Kuu wa Kuchaguliwa, Wajumbe wa Halmashauri Kuu wa Kuteuliwa, Makatibu na Wenyeviti wa Mikoa, Wawakilishi wa Makundi Mbalimbali kama vile Wanafunzi wa Vyuo Vikuu, Wabunge, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Madiwani, Watu Wenye Ulemavu pamoja na Ngome za Chama za Vijana, Wazee na Wanawake.
"Hii ni Halmashauri Kuu ya kwanza kuketi baada ya Uchaguzi Mkuu 2020 ambao uligubikwa na udanganyifu, hila na hujuma kubwa.
"Hivyo basi, pamoja na mambo mengine, Halmashauri Kuu ya Chama Taifa itapokea Taarifa ya Uchaguzi Mkuu 2020 na kuijadili.amesema Rithe.
"Pia, kutokana na nafasi ya Mwenyekiti wa Chama Taifa kuwa wazi kufuatia kufariki kwa Mwenyekiti wetu Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad, Halmashauri Kuu hii itatangaza mchakato wa uchaguzi wa kujaza nafasi ya Mwenyekiti wa Chama Taifa.
"Taarifa zaidi ya mchakato mzima wa uchaguzi wa kujaza nafasi hiyo, itatolewa baada ya kikao cha Halmashauri Kuu.
"Halmashauri Kuu ya Chama Taifa itapokea pia Taarifa ya Hali ya Kisiasa ndani ya Chama, Nchi na Kimataifa, kuijadili na kutoa mwelekeo wetu wa kisiasa wa ndani na nje ya nchi" alisisitiza mwenezi huyo.
0 Comments