Naibu waziri wa katiba na sheria Geofrey Pinda akitoa maelezo ya kuhamishwa kwa mahakama ya Mwanzo Kiponzero kutoka Ifunda kwenda Kiponzero , kutoka kushoto ni diwani wa kiponzero Veny Mnyinga na mbunge wa Kalenga Jackson Kiswaga
.................................
NAIBU Waziri wa Katiba na Sheria Geofrey Pinda ameagiza ndani ya mwezi mmoja mahakama ya mwanzo ya tarafa ya Kiponzero wilaya ya Iringa iliyokuwepo kijiji cha Kiponzero kisha kuhamishiwa kijiji cha Ifunda kata ya Ifunda kurudishwa kata ya Kiponzero ambako inatambulika na si vinginevyo .
Akizungumza na wananchi wa Kiponzero wakati wa mkutano wa hadhara mara baada ya kutembelea majengo ya yaliyokuwa yakitumiwa na mahakama ya mwanzo kiponzero kabla ya kuhamishiwa Ifunda ,Pinda alisema utaratibu uliotumika kuhamisha huduma za mahakama hiyo haukufuata taratibu za kiserikali hivyo hadi sasa mahakama inayotambuliwa ni ya Kiponzero na sio ya Ifunda .
Pinda alisema amefika katika eneo hilo la Kiponzero kujifunza zaidi juu ya uamuzi uliotumika kuhamisha huduma za mahakama katika eneo hilo na hadi sasa amebaini kuwa hakuna taratibu zozote za kiserikali zilizofuatwa kuhamisha mahakama hiyo kwani majengo yaliyopo Kiponzero ni majengo yenye sifa zote za kuendelea kutoa huduma za kimahakama katika eneo hilo .Naibu waziri wa katiba ya sheria Geofrey Pinda akiwa jirani na mlango wa mahakam ya Mwanzo Kiponzero iliyopo Ifunda ,kulia ni katibu tawala wa wilaya ya Iringa Stomen Kyando
Alisema amekagua jengo linalotumiwa kama mahakama kwa sasa lililopo kijiji cha Ifunda kuwa ni ni jengo lisilo la sifa hata moja ya kutoma huduma za kimahakama kwani ni jengo ambalo halina hadhi ya kimahakama tofauti na jengo la Mahakama lililopo Kiponzero ambalo limejengwa kwa sifa za kimahakama .
Pia alisema kabla ya huduma za kimahakama kuhamishwa katika eneo hilo ilipaswa kutolewa tangazo kwenye gazeti la serikali ila kwenye zoezi hilo la uhamishaji wa mahakama hiyo halijafanyika na hadi sasa wizara inatambua kuwa mahakama ya mwanzo tarafa ya Kiponzero ipo kijiji cha Kiponzero na sio kijiji cha Ifunda kama ilivyo sasa .
Alisema kinachohitajika katika majengo ya mahakama Kiponzero ni kujenga kituo cha polisi pamoja na kufanya ukarabati za jengo husika kwa kupaka rangi zoezi ambalo halitachukua muda mrefu .
" hata katika mpango wa serikali wa kuboresha majengo ya mahakama hatuwezi kuleta fedha kuja kukarabati jengo hilo la Ifunda ambalo ni jengo la udongo na kuacha kwenda kufanya ukarabati jengo la Kiponzero ambalo limejengwa kisasa mimi nafikiri kama ni hitaji ya mahakama eneo hilo ni kukaa kuangalia ni wapi kwenye tarafa hiyo ya kiponzero kujengwe mahakama nyingine mpya ila sio kuhamisha huduma za kimahakama katika eneo la Kiponzero"
Alisema lengo la serikali ni kuhakikisha kila kata inapata mahakama yake ila mpango wa sasa kuelekea 2021/2026 wamepania kuona kila makao makuu ya tarafa kuna kuwa na mahakama za mwanzo .
Kuhusu changamoto ya usafiri katika mahakama hiyo alisema serikali inajipanga kuboresha huduma za usafiri katika maeneo yenye changamoto ya usafiri .
Awali diwani wa kata ya Kiponzero Veni Myinga alisema kuwa wananchi wa Kiponzero wamekuwa wakilalamikia suala hilo muda mrefu kwa zaidi ya miaka 15 sasa toka mahakama hiyo huduma zake zilipohamishwa .
Diwani huyo alisema uamuzi wa kurejesha huduma za kimahakama makao makuu ya tarafa ni uamuzi mzuri ambao utaondoa kero kwa wananchi ambao walikuwa wakilazimika kutembea umbali wa zaidi ya kilometa 150 kutoka kijiji cha pembezoni kabisa mwa tarafa ya Kiponzero kwenda kijiji cha Ifunda kufuata huduma za kimahakama .
Myinga alisema mahakama hiyo ya Kiponzero ni mahakama ya kihistoria kwani ndio mahakama ya mwanzo kabisa kujengwa na Chifu Mkwawa miaka ya 1922 iliyopita na hadi sasa kwenye jengo hilo wamehama watu ila nyaraka zote za kimahakama zikiwemo nakala za hukumu za miaka hiyo zipo kwenye jengo hilo .
Huku mbunge wa Kalenga Jackson Kiswaga akiomba serikali kuharakisha ujenzi wa mahakama kwa wananchi wa kata ya Ifunda kutokana na idadi kubwa ya watu kwenye mji wa Ifunda na Joghorafia ya kutoka Ifunda kwenda Kiponzero .
Wananchi wa kijiji cha Kiponzero wakitoa zawadi ya kuku kwa naibu waziri wa katiba ya sheria Mhe Pinda
Mheshimiwa naibu waziri wa katiba ya Sheria Geofrey Pinda akizungunza na wananchi wa Kiponzero
Ukaguzi wa jengo lilokuwa likitumika kama mahakama ya Mwanzo tarafa ya Kiponzero
Nyaraka za mahakama ya Mwanzo Kiponzero zikiwa zimeachwa kwenye jengo la awali
Msasfara wa naibu waziri wa katiba ya sheria ukitembelea iliyokuwa mahakama ya mwanzo Kiponzero





0 Comments