MWILI wa mwanamke mkazi wa kijiji cha Mfyome wilaya ya Iringa Salome Kisayo (43) umekutwa porini huku shingoni kukiwa na alama za kucha na nguo yake ya ndani ikiwa kando ya mwili huo pamoja na kamba za miti ya asili huku mume wake akituhumiwa kuhusika na mauwaji hayo .
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Mfyome Richard Alyoce alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 3 asubuhi baada ya kijana mmoja kijijini hapo kuona mwili huo wakati akiwa katika harakati za kusafisha shamba.
''Majira ya saa 3 asubuhi nikiwa nyumbani kwangu alikuja kijana akaniambia kuna eneo fulani nilikuwa nafanya usafi wa shamba nimemuona mtu jinsia ya kike kama kalala chini, nikamuuliza unahisi atakuwa amekufa akasema ndio nahisi ameshafariki, nikamuita mwenyekiti wa kitongoji husika maana ndio eneo lake, tukaambatana mpaka eneo la tukio na tukamkuta aliyelala pale ni mwananchi aitwaye Salome Kisayo(43) huku pembeni kukiwa na kamba pamoja na nguo zake za ndani huku maeneo ya shingo kukiwa na kucha pamoja na alama za kukabwa'' alisema Richard
Mwenyekiti huyo alisema kufuatia tukio hilo walilazimika kutoa taarifa polisi ambao walipofika kuchukua mwili mpaka hospitali ya mkoa kwa ajili ya uchunguzi zaidi na baada ya hapo walikabidhiwa kwa ajili ya kwenda kuzika.
Hata hivyo alisema mume wa marehemu aitwaye Belatus Kindole(60) alitoweka walipokuwa mochwari ambapo mpaka sasa hajulikani alipo na simu zake hazipatikani.
''Huyu mume kwanza kabla ya mimi kupata hizi taarifa alikuja kwangu juzi jumapili majira ya saa 9 alasiri kuwa anamtafuta mkewe Salome na alikuwa na barua ya kitongoji na mimi nikamuandikia barua nyingine ili aweze kwenda vijiji vingine na polisi kutoa taarifa, lakini mpaka inafika hiyo saa tatu asubuhi siku ya Jumanne niliyopata taarifa kuja kushuhudia hili tukio nilimpigia simu baada ya kuona ni mke wake yule aliyekuwa anamtafuta, lakini ilimchukua kama saa hivi hivi kufika hapa eneo la tukio tukawa tupo wote mpaka tunaenda mochwari pamoja lakini kufika kule alikaa kidogo na akaondoka , tulipojaribu kumpigia simu zake zilikuwa hazipatikani mpaka muda huu tunaozika hayupo na hatujui yupo wapi'' alisema Mwenyekiti
Alisema kabla ya tukio hilo la mauwaji marehemu mara kwa mara walikuwa wanaishi kwa ugomvi na hata siku mbili kabla ya tukio hilo walikuwa wamefarakana na mwanamke alikimbilia kwa mama yake mzazi .
Mwanaume huyo alikwenda kumfuata mkewe kwa mzazi wake kwa kumuazima ili kwenda naye bustanini ila ajabu mchana alirudi kijijini kudai anamtafuta mkewe hajarejea nyumbani jambo ambalo lilishangaza wengi kwa hajawahi kumtafuta mke mchana kama huo .
" Kama viongozi wa kijiji tulichobaini mhusika wa mauwaji hayo ni mume wake mwenyewe maana hata kwa ndugu yake waliooa pamoja nyumba moja alidai siku ya tukio alifika nyumbani kwake na kumweleza kuwa amemuua mke wake shambani chanzo ni wivu wa kimapenzi "
kwa upande wake Diwani wa kata ya Kihwele Felix Waya alisema kuwa hilo ni tukio la kwanza kutokea katika eneo hilo na limewashangaza sana na amewataka wananchi kutoa taarifa kwa uongozi kama kuna jambo lolote linawakwaza hata kama ndani ya ndoa na sio kujichukulia sheria mkononi.
Kwa upande wake dada wa marehemu Matrida Kisayo alisema kuwa shemeji yake mara kwa mara alikuwa na ugomvi na mdogo wake na kuwa kufuatia mauwaji hayo shemeji mtu ametoweka na kuwa marehemu ameacha watoto sita.
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Iringa Juma Bwire alipotafutwa kuzungumzia tukio hilo alisema yupo nje ya ofisi kikazi na kuwa kesho atatoa taarifa kamili.
0 Comments