Mkurugenzi wa Alliance Ginnery Boaz Ogolla, ameyasema hayo juzi Jijini Dodoma, wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye mkutano wa Wadau na Wakulima wanaojishughulisha na Kilimo hai, mkutano ambao ulifanyika katika ukumbi wa St. Gasper.
“Nchi yetu ya Tanzania inaongoza Afrika kama mzalishaji mkubwa duniani ambapo inashika namba tano, kwa uzalishaji wa Pamba isiyotumia madawa ya viwani, hivyo nina uhakika kama wadau wote wataunga mkono jambo hili la kulima Kilimo Hai, nina uhahika nchi yetu inaweza kushika nafasi ya kwanza kwenye soko la Kimataifa,”alisema.
Ogola, ambaye pia ni mdau mkubwa wa Kilimo Hai cha zao la Pamba, hapa nchini , amesema shughuli ya kuanza Kilimo Hai, waliianza toka mwaka 2017 na kusema kuwa kwa sasa dunia nzima inakwenda kwenye kilimo Hai, na kutoa wito kwa wadau wote kuitumia fursa hiyo.
“Soko la Pamba ambayo haijatumia dawa za viwandani lipo la kutosha na bei yake ambayo tunauzia ni bei nzuri hivyo kwenye mnyororo wa thamani kwa wakulima kwa sasa watanufaika, kuanzia wakulima, watengenezaji wa nguo na bidhaa zote zitokanazo na kilimo hai cha pamba, kwanza watakuwa wametunza afya zao lakini pia na mazingira,’alisema.
Amesema wakati wanaanza kilimo hai, walianza na wakulima 1,500 hadi sasa tayari tumewasajili wakulima 28,000, ambayo wanajuishughulisha na kilimo hai, jambo ambalo limepata msukumo mkubwa kutokana Serikalini.
“Tunaishukuru Serikali kwa kutuunga mkono katika kuhamasisha wakulima kuanza kulima kilimo hai kisichotumia madawa ya viwandani, licha ya kwamba juhudi bado zinahitajika zaid,”alisema Ogola.
Amesema “Sisi kama Alliance Ginnery tumeona hii kama fursa kubwa baada ya nchi ya India na Uturuki kufutiwa kuuza Pamba yao kwenye soko la dunia jambo ambalo limewezesha Tanzania kupata soko la Kimataifa,”alisema.
Aidha Ogola, amesema changamoto iliyopo kwa sasa bado elimu inahitajika zaidi kwa wakulima kulima kilimo ambacho hakitumii madawa ya viwani, lakini pia ameiomba Serikali kuwaongezea mafunzo zaidi maafisa ugani ili waweze kufanya kazi kama timu kwa ajili ya kutoa elimu ya kilimo hai.
“Tunaiomba Serikali kuwapeleka kozi maafisa ugani ili waelewe namna ya Kilimo Hai, kinahitaji nini ili wanapokwenda kwa wakulima kuwahamasisha kilimo Hai waweze kuwa na uelewa mpana zaidi,”alisema.
MWISHO.





0 Comments