JUMUIYA ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma wameishukuru kampuni ya ukandarasi ya Ovans Construction LTD kwa kutoa msaada wa taulo za kike zenye thamani zaidi ya Sh milioni mbili (2,000,000)kwa wanafunzi wa Sekondari ya Mkinga na Sekondari ya wasichana ya Mbinga kwa lengo la kuwapunguzia adhaa wanafunzi hao wanapokuwa na uhitaji wa taulo hizo.MWANDISHI WA MATUKIO DAIMA AMON MTEGA ANARIPOTI TKA MBINGA
Akitoa pongezi hizo katibu wa Jumuiya hiyo Angelo Madundo wakati wa kugawa taulo hizo kwa wanafunzi wa shule hizo ambapo shule ya Sekondari ya wasichana ya Mbinga imepata taulo 932 na Sekondari ya Mkinga taulo zaidi ya 300 amesema kuwa kampuni ya Ovans Construction Ltd ,ilipokea ombi kutoka kwenye Jumuiya ya Wazazi wa CCM Wilaya ya Mbinga juu ya uhitaji wa taulo za kike kwa wanafunzi na kampuni hiyo ikakubali kutoa msaada huo.
Madundo amesema kuwa Jumuiya ya Wazazi baada ya kufanya utafiti juu ya baadhi ya wanafunzi wa kike kutokufanya vizuri kwenye masomo yao ni kutokana na baadhi ya changamoto ikiwemo ya kukosa taulo hizo.
"Kwa moyo wa dhati Jumuiya ya Wazazi tunaikushukuru kampuni hiyo ambayo inaongozwa na mkurugenzi wake Valence Urio kwa msaada huo ambao utawafanya watoto wetu wanafunzi wa kike kumpunguza changamoto ya uhitaji wa taulo hizo"amesema Katibu Angelo Madundo.
Kwa upande wake mkuu wa shule ya Sekondari ya wasichana ya Mbinga Efigenia Nzota ameishukuru Jumuiya hiyo kwa kutambua changamoto za wanafunzi wa kike hao na kuwa kutokana na msaada huo utawafanya wanafunzi kuhudhuria masomo yao kikamilifu.
Nzota pia ameipongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongonzwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za kuboreshea miundombinu mbalimbali ikiwemo ya shule na kuzifanya shule hizo ziendelee kuwa katika mazingira rafiki ya kusomea.
Naye mwanafunzi wa kidato cha Nne katika Sekondari ya Mkinga Desidelia Chazi akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake amesema kuwa wanafunzi wa kike wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya taulo hizo sasa changamoto hiyo itapungua huku akiishukuru Jumuiya ya Wazazi wao ambayo ndiyo inayomiliki shule ya Sekondari ya Mkinga ambayo inawanafunzi toka kidato cha kwanza hadi cha sita(HIGH SCHOOL)na inawanafunzi zaidi ya 200.
Hata hivyo mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM Wilaya ya Mbinga Erenest Mjirima amesema kuwa kazi ya Jumuiya hiyo ni kuhakikisha wanafunzi wanapatiwa Elimu bora pamoja na kutatua changamoto ambazo huwakabili wanafunzi hao hasa wa kike.
Mjirima pia amewataka wanafunzi hao wakazane kusoma kwa bidii ili waweze kufanya vema kwenye masomo yao na hatimaye kuweza kuwa na taifa bora lenye wasomi wakutosha.
Aidha Naibu Mkurugenzi wa Kampuni ya Ovans Construction Ltd,Agatha Urio ambaye naye ameambatana na wajumbe wa Jumuiya hiyo kwenye kugawa taulo hizo amesema kuwa kampuni hiyo imetoa msaada huo baada ya kupokea maombi kutoka Jumuiya ya Wazazi na kuwa itaendelea kushirikiana na jamii kuona namna ya bora ya kutatua changamoto ambazo zipo.
Kwa mjibu wa wahitaji hao inadaiwa kuwa taulo hizo watagaiwa kila mhitaji zaidi ya mbili na kuwa zinauwezo wa kudumu kwa mwaka mmoja na zimezingatia viwango bora vya kwa mtumiaji.
0 Comments