Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Sara Msafiri amewataka watu wote wanaofanya biashara zao kwenye maeneo yasiyo rasmi kuacha mara moja kuichokoza serikali kwani wameambiwa waondoke kwenda kwenye maeneo rasmi yaliyotengwa na Halmashauri ikiwemo Soko la Msufini na Lulanzi kwa ajili ya usalama wao
Ameyasema hayo leo akiwa ameambatana na kamati ya ulinzi na usalama Wilaya kwenye soko lisilo rasmi la Picha ya ndege ikiwa ni mara yake ya nne kufika eneo hilo kuwaasa waondoke ili kuepuka ajali zinazoweza kutokea kutokana na miundombinu finyu na ukaribu wa barabara kuu iendayo Morogoro kutoka Dar-es-Salaam kwani serikali haipo tayari kuona ajali zikitokea kama ilivyotokea Mkoani Morogoro miaka miwili michache iliyopita na kupotea maisha ya watu
Aidha, Mkuu wa Wilaya amewataka wafanyabiashara kutovunja sheria za nchi kwa makusudi kwani wamekuwa wakiomba leseni za biashara tofauti na biashara wanazokutwa nazo sehemu zao za kuuzia na kwamba hayo ni makosa ya kujitakia.
Mkana Mohamedi Mkana Mkuu wa Idara ya Usafishaji Mazingira amesema ni kosa kwa mfanyabiashara kuendelea kufanyabiashara eneo lisilo rasmi akiwa tayari ameelimishwa na kwamba adhabu yake ni faini ya fedha kiasi cha shilingi 50,000/-,Kifungo cha miezi sita jela au adhabu zote kwa pamoja na kwamba wafanya biashara hao wa Soko la Picha ya Ndege wanastahili kwani mara nyingi wameelishwa kuhusu kuondoka eneo hilo.
Kwa upande wake afisa biashara wa halmashauri ya Mji Kibaha Adolf Msangi amesema maeneo ya wafanyabiashara ndogo ndogo yapo ya kutosha na kwamba hakuna mfanyabiashara yeyote atakayekosa.
Kitendo cha kuwapanga wafanyabiashara ndogondogo kwenye maeneo rasmi ni agizo la kitaifa linaloendelea nchi nzima ili kuepusha ajali na majanga mengine ambayo yamekuwa yakiwakumba wafanyabiashara hao na kuwafanyawapote maisha pamoja na mitaji yao mitaji yao .
0 Comments