Header Ads Widget

AHUKUMIWA KIFO KWA KUMUUA MKEWE NA KUNYOFOA VIUNGO VYAKE


Mahakama ya Hakimu mkazi  Mkoa wa Mbeya imemhukumu kunyongwa hadi kufa Mateso Shantiwa(34), mkazi wa Kitusi wilayani Mbeya baada ya kupatikana na hatia namba 18 ya mwaka 2017 ya kumuua mke wake aitwaye Zaina Mela na kunyofoa viungo mbalimbali kwa ajili ya kujipatia utajiri. mwandishi wa matukio daima kutoka Mbeya anaripoti.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka mshtakiwa Shantiwa alidaiwa kutenda kosa hilo Aprili 22, 2017 akishirikiana na wenzake wawili, jambo ambalo ni kinyume cha kifungu namba 196 na 197 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kilichofanyiwa marekebisho mwaka 2002. 

Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu mkazi Mfawidhi Mkoa wa Mbeya, Zawadi Laizer mwenye mamlaka ya nyongeza kutoka mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Mbeya ya kusikiliza mashauri ya mauaji baada ya kuridhishwa na ushahidi wa upande wa Jamhuri bila kuacha shaka yoyote kuwa mshtakiwa alimuua mkewe.

Hakimu Laizer amesema mshtakiwa alikuwa akituhumiwa pamoja na wenzake wawili ambao hawakukamatwa alishirikiana nao kumuua mke wake na kunyofoa viungo kadhaa vikiwemo masikio na matiti yote mawili, macho na sura ya marehemu kisha kupeleka kwa mganga aliyewaahidi kupitia vitu hivyo angewatengenezea utajiri wa kudumu.

Hakimu Laizer amesema alizingatia maelekezo ya pande zote mbili na maoni ya wazee washauri wa mahakama, lakini zaidi mahakama imeridhika mshtakiwa kuhusika moja kwa moja kumuua mke wake na watu alioshirikiana nao kwa tamaa ya kupata utajiri licha ya kwamba mshtakiwa alikuwa akikana kutenda kosa hilo.

Mshtakiwa akiwakilishwa na wakili Hilda Mbele,  kabla ya hukumu aliomba mteja wake kupunguziwa adhabu lakini upande wa Jamhuri kupitia wakili aliyekuwapo mahakamani Davice Msanga akaiomba mahakama kutoa adhabu stahiki ili iwe fundisho kwa wengine ambao wanakubali kudanganywa na waganga wa kienyeji.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI