Mkuu wa Mkoa wa Iringa Queen Sendiga ameipongeza Kampuni ya uzalishaji na uuzaji wa nguzo za umeme ya New Forest kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya kwa kusaidiana na serikali katika uzalishaji wa nguzo za umeme.
Akiongea na waandishi wa habari hapo jana alipotembelea kampuni hiyo amesema kuwa lengo la ziara hiyo ni kukutana na wawekezaji ili kujadili, kusikiliza maoni yao mawili matatu pamoja na changamoto walizonazo ili serikali ipate kuwasaidia.
''lengo la ziara zangu hii, mbali ya kwenda kuona kwa macho namna ambavyo wanafanya kazi zao, lakini pia wakiwa kama wawekezaji waliopo ndani ya mkoa wanaweza wakawa wana maoni mawili matatu ama changamoto kadhaa ambazo wangehitaji sisi kama serikali tuweze kusaidiana nao kwa pamoja, na hapa tulipo leo New Forest Company ni kampuni kubwa Tanzania ambayo inazalisha nguzo za umeme, kwa hiyo kwa zaidi ya asilimia kubwa ya nguzo za umeme zinazoonekana katika nchi yetu hii zinatoka new forest, pia wafanyabiashara wa nguzo za kawaida na wakulima wanaolima miti ya nguzo wanauza nguzo zao hapa'', amesema Sendiga
Amesema kuwa kampuni ya Forest imeweza kudumisha ubora katika nguzo wanazozitengeneza pia imetoa ajira kwa vijana wengi sana, imesaidia pato la uchumi kwa kulipa kodi na pia kusaidia maswala ya kijamii katika mkoa wa Iringa kwenye masuala ya elimu, afya pamoja na ufugaji wa nyuki.
''nimepita kwenye namna ambayo wanazitreat hizi nguzo ambazo zinakwenda sokoni baadae kwa ajili ya matumizi, kikubwa ambacho nimejifunza hapa ni wanamantain ubora wa nguzo tumekuwa tukiona na kusikia mara kadhaa baadhi ya nguzo zilikuwa zikionekana hazina ubora labda kutoka kwenye maeneo mengine, new forest wanatengeneza nguzo zao vizuri lakini kizuri zaidi ambacho nimekiona hapa, serikali inafanya kazi sambamba na hii kampuni wataalamu wa Tanesco wako hapa sasahivi kwa ajili ya kujilizisha na ubora wa nguzo ambazo zimeshapigwa kutoka pale kwenye mashine tayari kwenda sokoni, kwahiyo ni jambo jema sana kwa serikali kujiridhishia ubora wa bidhaa kabla hazijaenda sokoni'' Amesema.
Sendiga amesema kuwa Serikali itaendelea kuwapa sapoti wawekezaji wote waliopo ndani na hata kwa wale watakaokuwa wametoka nje ya Nchi ili waweze kupata fursa ya kufanya shughuli zao zilizowaleta vizuri na pia watashirikiana katika kutatua changamoto zilizopo ili Tanzania iweze kuwa sehemu bora zaidi kwa uwekezaji Duniani.
''naomba niendelee kuwakaribisha wawekezaji mbalimbali wafike hapa Nchini lakini pia waje kuwekeza Iringa katika maeneo mbalimbali, pia tumezindua kongamano ambalo tunategemea kulifanya muda sio mrefu litakalohusiana na mazao ya misitu moja wapo ni kama hilo kwahiyo fursa za misitu na uwekezaji katika ardhi kwa lengo la kupanda miti na kufanya huduma za misitu katika mkoa huu bado ni pana na kubwa sana kwa hiyo tunawakaribisha sana'', amesema
Na kwa upande wake Meneja Idara ya Maendeleo ya Jamii Bahati Sosthenes amesema kuwa vitu wanavyovifanya ni miradi ya upandaji na utunzaji wa miti, masoko, kusaidia wananchi katika maswala ya uvunaji wa asali na kuuza katika masoko mbalimbali pia kwa jamii wamejenga hospitali katika baadhi ya vijiji ambavyo vipo katika Wilaya ya Kilolo, vyoo na baadhi ya madarasa pia wamesaidia Wilaya nzima katika maswala ya madawati.
0 Comments