MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania
(TMA) imetoa tahadhari ya vipindi vya mvua kubwa vinavyotarajiwa kunyesha
katika maeneo machache ya mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe na Ruvuma pamoja na
kusini mwa Mkoa wa Morogoro, kuanzia Jumatatu, Novemba 16, 2026.
Kwa mujibu wa
taarifa iliyotolewa leo Jumapili, Novemba 15, 2026, uwezekano wa kutokea kwa
mvua hiyo ni wa wastani, huku kiwango cha athari zinazoweza kujitokeza
kikielezwa kuwa cha wastani.
Miongoni mwa
athari hizo ni mafuriko kuathiri baadhi ya maeneo. Kwa sababu hiyo, wananchi
katika maeneo yaliyotajwa wametakiwa kuchukua tahadhari.
Hata hivyo, kwa
siku ya leo Jumapili, hakuna tahadhari yoyote ya hali mbaya ya hewa
iliyotolewa. Vilevile, hakuna tahadhari inayotarajiwa kuanzia Jumanne hadi
Alhamisi, Novemba 17 hadi 19, 2026.
UTABIRI KWA SAA 24 ZIJAZO
Katika utabiri
wa saa 24 zijazo kuanzia saa 3.00 usiku wa leo, mikoa ya Morogoro na Ruvuma,
Rukwa, Iringa, Njombe, Songwe na Mbeya, pamoja na mikoa ya Mtwara na Lindi,
inatarajiwa kupata hali ya mawingu, mvua na ngurumo katika maeneo machache,
ikichanganyika na vipindi vifupi vya jua.
Hali kama hiyo
inatarajiwa pia katika visiwa vya Unguja na Pemba, mikoa ya Dodoma na Singida,
Tanga na Dar es Salaam, Kigoma, Tabora na Katavi, Manyara, Arusha na
Kilimanjaro, Pwani ikiwemo visiwa vya Mafia, pamoja na mikoa ya Kagera, Mara,
Simiyu, Shinyanga, Mwanza na Geita.
Kwa upande wa viwango vya joto,
miji ya Dar es Salaam na Tanga inatarajiwa kuwa na joto la juu zaidi la nyuzi
32, ikifuatiwa na Zanzibar nyuzi 31 na Kigoma nyuzi 30.
Mji wa Mwanza
unatarajiwa kuwa na nyuzi 29, huku Dodoma na Tabora zikiwa na nyuzi 28. Arusha
na Mbeya zinatarajiwa kuwa na nyuzi 27, Iringa nyuzi 25, huku Njombe ikiwa na
joto la chini zaidi la nyuzi 24.
Viwango vya
chini vya joto vitaanzia nyuzi 12 Njombe hadi nyuzi 23 Tanga na Zanzibar.
Kwa upande wa
upepo, pwani inatarajiwa kuvuma kwa kasi ya kilomita 20 kwa saa kutoka
Mashariki, huku kusini mwa pwani ukivuma kwa kasi ya kilomita 30 kwa saa kutoka
Kaskazini Mashariki. Bahari inatarajiwa kuwa na mawimbi madogo hadi makubwa
kiasi.
TMA imesema
matarajio ya siku ya Jumanne, Novemba 17, 2026 ni kuendelea kwa vipindi vya
mvua katika maeneo mengi hapa nchini.








0 Comments