Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imepokea msaada wa vigae pamoja na masinki ya choo kutoka kampuni ya Twyford wenye thamani ya shilingi milioni 24, ikiwa ni sehemu ya mchango wa kampuni hiyo katika kuunga mkono juhudi za kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma za afya.
Akizungumza mara baada ya kupokea msaada huo, Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga wa MNH, Bi. Redempta Matindi, ameishukuru kampuni ya Twyford kwa kuonesha moyo wa kujali na kushirikiana na hospitali hiyo katika kuboresha mazingira ya kutolea huduma. Amesema msaada huo ni muhimu kwa kuwa utasaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha miundombinu na kuongeza ubora wa mazingira yanayotumiwa katika utoaji wa huduma.
Kwa upande wake, Riz Zhao Mkurugenzi Msaidizi wa kampuni ya Twyford ameeleza kuwa kampuni hiyo inatambua umuhimu wa kushirikiana na jamii pamoja na taasisi mbalimbali katika kuchangia maendeleo ya sekta muhimu nchini, ikiwemo sekta ya afya. Amesema msaada huo ni sehemu ya jitihada za kampuni hiyo kurejesha kwa jamii na kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Muhimbili katika kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma kwa wananchi.
Muhimbili inaendelea kuthamini ushirikiano na michango inayotolewa na wadau mbalimbali katika kuimarisha huduma za afya na kuboresha miundombinu yake. Ushirikiano huo unaonesha umuhimu wa wadau wa sekta binafsi kushiriki katika kuunga mkono juhudi za serikali za kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya katika mazingira salama na rafiki.












0 Comments