Header Ads Widget

MAKAMU WA RAIS AIPONGEZA UDSM KWA USIMAMIZI BORA WA MRADI WA KAMPASI YA LINDI, UJENZI WAFIKIA ASILIMIA 98

                           


NA HADIJA OMARY 

LINDI.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi, ameipongeza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwa usimamizi na utekelezaji mzuri wa mradi wa ujenzi wa Kampasi ya Lindi, akisema ubora wa majengo yaliyojengwa unaonesha matumizi sahihi ya fedha za umma na thamani halisi ya uwekezaji, huku ujenzi wa awamu ya kwanza ya mradi huo ukifikia asilimia 98.

Pongezi hizo zimetolewa wakati wa ziara ya Makamu wa Rais ya kukagua maendeleo ya mradi huo katika eneo la Ngongo, Manispaa ya Lindi, unaotekelezwa kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), unaofadhiliwa na Serikali ya Tanzania kupitia mkopo kutoka Benki ya Dunia.

Mhe. Ndejembi amesema ameridhishwa na usimamizi, ufuatiliaji na ubora wa miundombinu iliyojengwa, akibainisha kuwa uwekezaji wa takribani Shilingi bilioni 14 umeleta matokeo yanayoonekana. Aidha, amezitaka taasisi nyingine za umma kujifunza kutoka UDSM kuhusu namna bora ya kusimamia na kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo.

Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais ameelekeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kutoa kipaumbele kwa Kampasi ya Lindi katika awamu ya pili ya mradi wa HEET, hususan katika ujenzi wa nyumba za makazi kwa ajili ya wahadhiri na watumishi wa chuo hicho, ili kuboresha mazingira ya kazi na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma za kitaaluma.


Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, ameipongeza UDSM kwa hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa kampasi hiyo, huku akisisitiza umuhimu wa kukamilisha miundombinu muhimu, ikiwemo barabara za kuifikia kampasi na nyumba za watumishi.


Dkt. Kikwete amesema kukamilika kwa miundombinu hiyo kutaiwezesha kampasi kufanya kazi kama jumuiya kamili ya kitaaluma na kuwapa watumishi mazingira bora ya kuishi na kutekeleza majukumu yao.


Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Naibu Mratibu wa HEET wa UDSM, Prof. Liberato Venant Haule, amesema mkandarasi anatarajiwa kukabidhi majengo kabla ya Novemba 30, 2026, baada ya kuongezwa kwa muda wa utekelezaji ili kukamilisha kazi zilizobaki.


Prof. Haule amefafanua kuwa mradi huo unahusisha ujenzi wa majengo sita katika eneo la Ngongo, Manispaa ya Lindi, pamoja na majengo mengine matatu katika Kituo cha Utafiti cha UDSM kilichopo Wilaya ya Ruangwa. Mradi huo una gharama ya jumla ya Shilingi 14,795,722,687.72.




Amesema katika eneo la Ngongo, miundombinu iliyojengwa inajumuisha jengo la utawala na taaluma lenye ofisi na vyumba vitano vya mihadhara vyenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 390 kwa pamoja, maktaba, karakana yenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 30, maabara tatu zitakazotumiwa na wanafunzi 125, pamoja na mabweni mawili yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 200.


Kwa upande wa Kituo cha Utafiti cha Ruangwa, majengo yaliyojengwa yanajumuisha bweni, darasa na ukumbi wa chakula vyenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 50.


Mbali na uwekezaji wa miundombinu, Kampasi ya Lindi inatarajiwa kupanua fursa za elimu ya juu katika fani mbalimbali zinazohusiana na kilimo na uzalishaji. Tayari kampasi hiyo imetambuliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), na programu nne zimeidhinishwa, ambazo ni Shahada ya Sayansi ya Teknolojia ya Sayansi ya Mazao, Shahada ya Sayansi ya Teknolojia ya Nyuki, Stashahada ya Afya na Uzalishaji wa Mifugo, pamoja na Stashahada ya Teknolojia na Usimamizi wa Uzalishaji wa Mazao.


Shughuli za kitaaluma katika kampasi hiyo zitatekelezwa kupitia idara tano. Katika hatua ya awali, chuo kinatarajia kudahili wanafunzi 360 kuanzia Machi 2027 katika programu mbili za shahada ya kwanza, kabla ya kuanzisha programu nyingine mbili zitakazoongeza nafasi 120 za udahili.


Kwa mujibu wa mpango wa muda mrefu, Kampasi ya Lindi inalenga kuhudumia wanafunzi 1,320 ifikapo mwaka wa masomo 2029/2030.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI