Header Ads Widget

MAELFU YA SAFARI ZA NDEGE MAREKANI ZAKWAMA KWA SIKU TATU

Maelfu ya safari za ndege nchini Marekani zilifutwa au kucheleweshwa siku ya Jumapili, wakati mfumo wa udhibiti wa safari za ndege ukiendelea kurejeshwa katika hali yake ya kawaida kufuatia hitilafu ya kiufundi iliyosababisha kusitishwa kwa safari za ndege kote nchini humo.

Waziri wa Uchukuzi wa Marekani, Sean Duffy, amesema huenda shughuli za usafiri wa anga zisirejee katika hali ya kawaida Jumatatu.

"Tuna ndege na wafanyakazi ambao hawapo katika maeneo yao yaliyopangwa, hivyo inahitaji muda kidogo kurejesha hali ya kawaida," aliiambia CBS, mshirika wa BBC nchini Marekani.

Zaidi ya safari 8,800 za ndege zilichelewa huku nyingine 2,400 zikifutwa siku ya Jumapili.

Rais Donald Trump ameitaka Bunge la Marekani kuidhinisha fedha zaidi kwa ajili ya kuboresha mfumo wa udhibiti wa safari za ndege.

Hatua ya kusitisha safari zote za ndege zilizokuwa zimepangwa kuondoka Marekani siku ya Ijumaa ilisababisha vurugu katika viwanja vya ndege kote nchini.

Zaidi ya ndege 3,500 zilikuwa angani wakati Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Marekani (FAA) ilipotangaza saa 15:54 kwa saa za Marekani (20:54 GMT) kwamba safari za ndege zingesitishwa hadi itakapotangazwa vinginevyo.

Baadhi ya ndege zilielekezwa katika viwanja vingine vya ndege, huku nyingine zikiendelea na safari zake hadi zilipofika kwenye vituo vilivyokusudiwa.

Kwa mujibu wa tovuti ya ufuatiliaji wa safari za ndege ya FlightAware, baada ya tangazo hilo, safari 8,500 zilicheleweshwa na nyingine 8,000 zikafutwa.

Kusitishwa kwa safari hizo kuliwaacha baadhi ya abiria wakiwa wamekwama ndani ya ndege zilizokuwa kwenye njia za kurukia na kutua, bila uwezo wa kuruka wala kurejea kwenye maeneo ya kuegesha ndege.

Abiria wengine walikwama ndani ya viwanja vya ndege, wakilala sakafuni na kujaribu kwa kila hali kuwasiliana na mashirika ya ndege.

Hatua hiyo pia iliathiri ratiba za safari za ndege katika maeneo mengine duniani, huku baadhi ya safari kutoka Uingereza na Ulaya zikifutwa.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI