Header Ads Widget

HIFADHI YA TAIFA TARANGIRE YATUMIKA KAMA JUKWAA LA KUCHANGISHIA FEDHA KUOKOA MAISHA YA MAMA NA MTOTO

 


Na. Calvin Katera - Babati.


Wageni 86 kutoka mataifa tisa duniani ikiwemo Ujerumani, Uingereza, Uholanzi, Poland, Marekani, Kenya na Ireland wameendesha kampeni ya kuchangia huduma ya mama na mtoto kupitia utalii wa baiskeli ndani ya Hifadhi ya Taifa Tarangire, zoezi lililofanyika leo Novemba 26, 2026.

Mbio hizo za baiskeli zimeratibiwa na Shirika lisilo la kiserikali la kimataifa liitwalo CHILD.ORG likihusisha kampeni iendayo kwa jina la RIDE AFRICA kwa lengo la kukusanya fedha ili kuchagiza usalama wa huduma za afya kwa mama na mtoto katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki.

Akizungumza katika uzinduzi wa mbio hizo Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo Bi. Martina Gant alisema kuwa shirika hilo limejikita kuokoa maisha ya mama na mtoto kwa kutoa huduma na mafunzo kwa wanawake, wahudumu wa afya za jamii, serikali za mitaa ili kuboresha ubora wa huduma za afya wanazozipata ndani ya maeneo yao.

Pia, aliongeza kuwa Shirika hilo limefanikiwa kuchangisha kiasi cha Paundi Laki Mbili na Ishirini Elfu (220,000/=) fedha ambazo zitatumika kugharamia miradi ya afya na Hifadhi ya Taifa Tarangire ni miongoni mwa maeneo yenye urithi wa Maliasili unaowakutanisha watalii wengi kutoka mataifa mbalimbali wanaoweza kuunga mkono jitihada hizi za afya mama na mtoto.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Tarangire, Afisa Uhifadhi Mkuu Edison Chongolo alieleza kuwa zoezi hili la utalii wa baiskeli haliishii ndani ya mipaka ya Hifadhi pekee bali kupitia kumbukumbu za picha binafsi na za waandishi wa habari, mandhari ya kuvutia zitasambazwa na kuvutia watalii wengi kuitembelea hifadhi hii inayosifika kwa kuwa na tembo wenye maumbile makubwa Afrika Mashariki. 

Zoezi hilo limefanyika kwa mara ya kwanza ndani ya mipaka ya Tanzania ambako waendesha baiskeli wameweza kupita eneo la Hifadhi lenye takribani kilometa 45 huku Hifadhi ya Taifa Tarangire ikichagiza zoezi hilo kwa shangwe na kulipa jina zao hilo " Visit Tarangire, Pedal the Wild Experience ".









Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI